Na Faraja Masinde, Dar es Salaam
MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imesema ni kinyume cha sheria namba 17 ya Bandari ya mwaka 2004 kwa taasisi au mtu binafsi kuendeleza, kusimamia na kuendesha bandari yoyote nchini bila kibali chao.
Kauli hiyo imekuja huku kukiwa na taarifa za kupotosha kuwa shughuli za TPA katika eneo la Mwambani zitafanywa na Kampuni ya Mwambani Port and Railway Corridor Company (MWAPORC).
Taarifa hizo zilihusisha mradi huo na shughuli za MWAPORC kuwa TPA imetoa zabuni ya ujenzi wa Bandari ya Mwambani kwa kampuni binafsi bila kufuata taratibu za ununuzi.
Akitoa ufafanuzi Dar es Salaam jana, Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano wa TPA, Janeth Ruzangi, alisema taarifa hizo si za kweli, kwa kuwa sasa hivi inaandaa zabuni ya ujenzi wa Bandari ya Mwambani baada ya wawekezaji kutojitokeza mwanzo.
“Pamoja na neno mwambani kujitokeza katika mradi wa bandari wa TPA na katika Mwambani Economic Corridor Project, lakini hivi ni vitu viwili tofauti na kwa sasa shughuli za MWAPORC hazina uhusiano wowote na mradi wa TPA wa kujenga bandari mpya katika eneo la Mwambani, Tanga,” alisema Janeth.