25.4 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

TPA yajivunia mafanikio lukuki 2023

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), imesema Bandari ya Dar es Salaam imekuwa ikiendeshwa kwa ubora kwa kuhudumia wateja na wadau hadi kutoka nchi jirani, hivyo kutokana na kuwa na jukumu hilo, bandari hiyo ilijiwekea malengo ya utoaji huduma kuanzia Julai hadi Desemba mwaka 2023 ambapo imetimiza malengo yake.

Pia, imetaja mafanikio waliyoyapata katika kipindi cha Julai hadi Desemba mwaka jana na kuainisha mikakati saba wanayotarajia kuitekeleza mwaka huu ikiwemo wa kuanza kwa matumizi ya bandari ya Kavu ya Kwala.

Hayo yamebainishwa leo Januari 9, 2024 jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa wakati akizungumza na Waandishi wa habari ambapo pia amejata bandari kubwa sita ikiwa tatu za mwambao wa bahari(Dar es Salaam, Mtwara na Tanga) na tatu zikiwa maziwa makuu yaani ziwa Victoria, Tanganyika na Nyasa.

Jengo la Mamla ya Bandari Tanzania (TPA).

Amesema kwa kipindi cha Julai hadi Desemba, mwaka jana, TPA ilijiwekea lengo la kuhudumia meli 792 na hadi kufikia Desemba, mwaka jana ilikuwa imevuka lengo na kuhudumia meli 979 sawa na asilimia 123.6.

“Kwa upande wa ukubwa wa meli zilizohudumiwa, TPA ilikuwa na lengo la kuhudumia meli zenye ukubwa wa tani 15,576,000 katika kipindi cha Julai hadi Desemba mwaka 2023 ambapo hadi kufikia mwezi Desemba, 2023, TPA ilikuwa tayari imehudumia meli zenye ukubwa wa kiasi cha tani 17,200,692 sawa na asilimia 110.4,” amesema Mbossa.

Amesema TPA ilikuwa na lengo la kuhudumia kiasi cha tani 10,993,000 katika bandari ya Dar es Salaam na hadi kufikia Desemba, mwaka jana ilihudumia tani 12,052,682 sawa na asilimia 109.6 za lengo.

Mbossa amesema katika kipindi hicho, TPA iliweza kuhudumia kiasi cha makontena 509,594 sawa na asilimia 102.8 za lengo lililowekwa la kuhudumia kiasi cha makontena 495,600 kwa kipindi cha Julai hadi Desemba, mwaka jana.

ABIRIA

Amesema idadi ya abiria waliohudumiwa katika bandari ya Dar es Salaam hadi kufikia Desemba mwaka jana ilikuwa 987,228 sawa na asilimia 98.3 ya lengo lililowekwa la abiria 1,004,167.

Vilevile amesema mafanikio hayo yametokana na uhusiano mzuri uliopo kati ya nchi na nchi.

“Rais Dk. Samia Suluhu Hassan amefanya mahusiano mazuri katika nchi nyingi hali iliyosababisha hata sisi TPA tunapata mizigo mingi katika bandari zetu ikiwemo bandari ya Dar es Salaam,”amesema.

MKAKATI

Mbossa akizungumzia kuhusu mikakati ya maboresho ya bandari amesema TPA imeendelea kutekeleza jukumu la kuhudumia meli na shehena ambapo kati ya mwaka wa fedha 2023/2024 kumekuwa na ongezeko kubwa la idadi ya meli na shehena katika bandari ya Dar es Salaam.

Amesema ongezeko hilo ni matokeo ya mikakati ya maboresho ya huduma za bandari ikiwa ni pamoja na kufanya kampeni za kimasoko na kuonana ana kwa ana na wateja wa ndani na nje ya nchi.

Aidha, amesema kuboresha huduma kwa wateja, kutoa tozo shindani, kuimarisha ofisi za kimasoko zilizopo nje ya nchi na kufungua mpya, ushirikiano na wateja na wadau wa bandari na kusomana kwa mifumo.

Akizungumzia kuhusu bandari ya Kwala amesema mikakati mingine ni kuanza kwa matumizi ya Bandari kavu ya Kwala, kwani mamlaka iliweka mikakati tofauti ikiwemo kuongeza muda huru hadi kufikia siku 30 kwa makasha ya ndani na siku 60 kwa makasha ya nchi jirani.

Vilevile punguzo kwa gharama za usafirishaji wa mizigo kwa njia ya reli ya Shirika la Reli Tanzania(TRC) kutoka bandari ya Dar es Salaam, kwenda Kwala.

BANDARI YA BAGAMOYO

Mbossa amesema TPA imeamua kutenganisha utekelezaji wa mradi wa bandari ya Bagamoyo na mradi wa eneo maalumu la kiuchumi Bagamoyo.

Awali imeelezwa ujenzi wa mradi wa bandari ya Bagamoyo utahusisha ujenzi wa eneo maalumu la kiuchumi.

“Tunaanzia na gati mbili ndefu na hizo zitajengwa na sisi TPA tupo tayari kupokea mwekezaji kutoka sekta binafsi atakayeijenga bandari hiyo kushirikiana na serikali,” amesema.

Amesema awali mpango wa ujenzi wa mradi ulikuwa uhusishwe na eneo maalumu la uchumi, lakini wameamua kutekeleza miradi hiyo kwa nyakati tofauti.

CHANGAMOTO

Mkurugenzi huyo alitaja changamoto zinazoikabili bandari hiyo kuwa ni uchache wa magati, miundombinu isiyotosheleza ya reli na barabara ambayo ingerahisisha uondoshaji wa shehena bandarini kwa haraka.

Ameeleza changamoto nyingine ni kuharibika mara kwa mara kwa midaki, mitambo ya kuhudumia shehena, ongezeko kubwa la meli kulinganisha na uwezo wa bandari, utoaji wa huduma kusimamishwa na mvua za El-Nino, baadhi ya gati kutumika katika shughuli za kijamii na uchimbaji wa gati namba nane hadi 10.

Mbossa ametaja mikakati ya kutatua changamoto hizo kuwa katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati ni ujenzi wa gati jipya la kuhudumia makasha, ujenzi wa eneo maalum la kuhudumia shehena zinazotoka au kuelelekea bandari ya Dar es Salaam katika eneo la Kurasini.

Mikakati mingine ni usimikaji wa maboya mapya ya kupakulia mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam, ujenzi wa bandari ya Bagamoyo eneo la Ras Mbegani, ujenzi wa matenki ya kupokelea na kuhifadhi mafuta na ujenzi wagati lenye urefu wa mita 500.

Mikakati mingine ni kuzishirikisha sekta binafsi kwa kupunguza muda wa meli kusubiri nangani kutoka siku tano hadi saa 24, kupunguza muda wa kupakia na kupakua makasha kutoka siku nne hadi siku mbili, kupunguza gharama za usafirishaji wa shehena kutoka USD 12,000 hadi kati ya USD 6000 na USD 7000 kwa kasha linalokwenda Malawi, Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Pia kuongeza mapato ya serikali ya kodi ya forodha kutoka trilioni 7.76 za mwaka 2021/2022 hadi trilioni 26.7 mwaka 2032/2033 na kuchochea ukuaji wa sekta zingine za kiuchumi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles