25.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

TMDA yanasa wachepushaji dawa za Serikali

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba(TMDA),imefanya ukaguzi katika maduka ya dawa na  kunasa wachepushaji wa dawa za serikali,  huku  ikiwaonya wasambazaji na wauza dawa bandia.

Imetaja  mikoa vinara kwa uchepushaji wa dawa za serikali kuwa ni Dar es Salaam, Lindi na Simiyu.

Akizungumza wakati WA kutoa taarifa ya operesheni ya ukaguzi waliofanya  mbele ya waandishi wa habari leo Desemba 20,2023 jijini Dar es Salaam  Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Adam Fimbo, amesema dawa na vifaa tiba bandia ni hatari kwa afya ya jamii.

Amesema  opereshemi maalumu ya kukamata dawa bandia, vifaa tiba na vitendanishi  vya serikali,  zisizo na usajili na dawa za kulevya  iliyofanyika Novemba 20 hadi 24,2023.

“Operesheni hii ilifanyika kwa wilaya mbalimbali zilizopo katika mikoa 13 ambayo ni Dar es Salaam, Dodoma, Morogoro, Kigoma, Katavi, Mwanza, Simiyu, Arusha, Kilimanjaro, Mbeya, Songwe, Lindi na Ruvuma,” amesema.

Amesema ukaguzi huo  ulilenga   bidhaa bandia za afya katika hospitali, vituo vya afya zahanati, maghala, maduka ya jumla  na rejareja ya watu binafsi  na maeneo mengine yasiyo rasmi.

Ameeleza kuwa  bidhaa za serikali zilizokutwa zinauzwa  katika maduka ya dawa na vituo binafsi  vya kutolea huduma  ni dawa za mseto ya kutibu malaria ya vidonge aina ya ALU, dawa la mseto ya kutibu kifua kikuu, dawa za uzazi wa mpango.

Amesema dawa hizo zilikutwa katika maduka yaliyoko mikoa ya Dar es Salaam, Lindi, Ruvuma na Simiyu.

“Vifaa tiba vya serikali  vinavyokadiliwa  kuwa na thamani ya Sh milioni 11.297 vilikamatwa  katika vituo na maduka  binafsi na baadhi ni   vifaa vya kupima  malaria na virusi vya ukimwi,” amefafanua.

Amesema katika operesheni hiyo walikamata dawa zilizokwisha muda wa matumizi zenye thamani inayokadiriwa kuwa Sh milioni 9.5 ambazo zilikamatwa zikiwa hazijatengwa kwa mujibu wa utaratibu  katika kanda ya Kati, Kanda ya Ziwa Mashariki na Nyanda za Juu Kusini.

Amesema dawa bandia  za binadamu zenye thamani ya Sh milioni 5.9 zilikamatwa Kanda ya Kaskazini, Nyanda za Juu Kusini na Kanda ya Magharibi na Kanda ya Juu Kusini ndiyo inaongoza ikifuatiwa na Magharibi.

Fimbo amesema jumla ya bidhaa zenye thamani ya Sh milioni 172.2 zimekamatwa katika operesheni hiyo.

Pia amesema operesheni hiyo ilibaini uwepo wa dawa zenye madhara ya kulevya aina ya ‘pathidine’ katika maeneo mbalimbali zikiuzwa kwa siri na mtandao wote umebainika na wahusika wameshafahamika.

Aidha amesema watuhumiwa wote waliokutwa na kuhusika moja kwa moja na kusambaza au kuuza dawa, vifaa tiba au vitendanishi  vya serikali na bandia wamefikishwa katika vyombo vya sheria.

Amesema jumla ya majalada 13 yamefunguliwa dhidi ya watuhumiwa na taratibu za kuwafikisha mahakamani zinaendelea katika vituo vya polisi.

“Jumla ya Sh milioni 100 zimetozwa kama faini  kwa wote ambao makosa yao hayakuhitaji kufikishwa mahakamani,” amesema.

Ametaja hatua  yingine iliyofanyika ni kuondoa dawa bandia, dawa na vifaa tiba duni, dawa na vitendanishi vilivyokwisha muda wa matumizi na dawa zisizosajiliwa katika soko kwa ajili ya taratibu za uteketezaji kwa mujibu wa sheria zilizopo.

Pia wametaifisha dawa na vifaa tiba vya serikali na kuelekeza wamiliki wa maduka yasiyo na vibali na wataalamu kufunga maduka yao na kufanya utaratibu wa kuyasajili rasmi.

Fimbo amesema serikali itaendelea kuwatafuta na kuwachukulia hatua  wale wanaofanya biashara  hiyo haramu  kwa mujibu wa sheria ya dawa na vifaa tiba.

“Wale wote wanaotengeneza, kusambaza, kuuza dawa, vifaa tiba na vitendanishi bandia kuacha mara moja kwani ni hatari kwa afya ya jamii kwani bidhaa kama hizo zinakosesha watu haki yao ya kupata huduma ya matibabu  kuweza kupona maradhi yao,”amesema.

Amewataka watoa huduma za afya kwa hospitali kuacha kuiba dawa, vifaa tiba, vitendanishi  vya serikali na kuviuza  katika maduka ya watu binafsi.

Naye Msajili wa Baraza la Famasia, Elizabeth Shekalaghe ameonya maduka ya dawa yanayotoa huduma  kinyume  kama kuchoma watu sindano  kwani  kufanya hivyo kunahatarisha afya za wananchi.

“Nawataka wananchi kutoweka afya zao rehani kwa kwenda katika maduka ya dawa kuchukuliwa vipimo, kuchomwa sindano kwani hayaruhusiwi kutoa huduma hiyo.

“Kazi ya duka la dawa ni kuuza dawa pekee na kazi ya maabara ni kupima tu na sio kutoa dawa nawasihi wananchi kuweni makini kwa hili,” amesema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles