Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
CHAMA cha Gofu cha Wanawake Tanzania (TLGU) kwa kushirikiana na familia ya Nkya wameandaa shindano linaloitwa ‘Lina PG Tour’ kwa ajili ya kumuenzi mchezaji wa gofu wa zamani anayeitwa Lina Nkya.
Lina Nkya ambaye alikuwa mchezaji wa Timu ya Taifa ya Gofu na miongoni mwa wachezaji waliopeperusha vyema bendera ya Tanzania, alifariki dunia miaka mitatu iliyopita.
Akizungumza na waandishi wa habari jijjni Dar es Salaam, Makamu wa Rais wa TLGU, Ayne Magombe amesema shindano hilo litafanyika kwa mwaka mzima katika mikoa mbalimbali ikiwemo Dar es Salaam na Moshi.
“Lina alikuwa mchezaji gofu maarufu nchini, ivyo katika kumuenzi tunataka tuendelee kuibua wengi watakaopeperusha bendera ya taifa.
“Tunachukua fursa hii kuwaalika wachezaji wote wa Gofu waweze kushiriki kwani kutakuwa na zawadi nono kwa washindi na yatakuwa yanafanyika kila mwaka,” amesema Magombe.
Katibu wa mashindano wa TLGU, Rehema Athumani amesema shindano litaanza Februari 29 hadi Machi 3 katika klabu ya TPC iliyopo Moshi na Zanzibar Aprili 11 hadi 14, mwaka huu.
“Baada ya hapo litafanyika Arusha Gymkhana Julai 11 hadi 14, na kumalizika Novemba 14 hadi 17 katika klabu ya Gymkhana, Dar es Salaam,” amesema Rehema.
Naye mume wa marehemu Lina, Said Nkya amesema mke wake alikuwa akiupenda mchezo huo kiasi cha kuibua wachezaji wengi wa kulipwa kupitia klabu ya Moshi jambo ambalo wameona waliendeleze kuibua wengine wa kuwakilisha taifa.
“Tumeandaa zawadi nzuri ili kutoa motisha kwa vijana wadogo kuongeza bidii na kuonesha kiwango cha juu ili kutamani kuwafikia waliofanya vizuri,” amesema Nkya.