Na Mwandishi Wetu-Dar es Salaam
WAZIRI wa Kilimo, Dk. Charles Tizeba ameanza kutekeleza agizo la Rais Dk. John Magufuli kuhakikisha mbolea inafika maeneo yote nchini hasa mkoani Rukwa ambako kumetajwa kuwa na upungufu mkubwa.
Juz,i wakati akimwapisha Naibu Waziri mpya wa Wizara ya Madini, Doto Biteko, Rais Magufuli aliwanyooshea kidole Waziri wa Kilimo, Dk. Charles Tizeba na Waziri wa Madini, Angellah Kairuki, kuhusu utendaji kazi wao.
Kuhusu Tizeba, Rais Magufuli alisema haiwezekani hadi sasa baadhi ya mikoa, ikiwamo inayotegemewa kwa uzalishaji wa chakula kwa wingi, kushindwa kupata mbolea, huku yeye yupo bila kuchukua hatua.
Alitoa maelekezo kwa Waziri kushughulikia malalamiko ya uhaba wa mbolea katika Mkoa wa Rukwa na maeneo mengine ya jirani na kutaka hadi Ijumaa Januari 12, 2018 mbolea iwe imefika katika mikoa hiyo.
“Ninapozungumza hapa ndugu zangu, ipo mikoa haijapelekewa mbolea, ikiwamo mikoa ya Rukwa sijui na mkoa gani. Wakati tunaizungumzia kama ‘the big four’ kwa ‘production’ ya chakula, mbolea bado haijapelekwa, lakini Waziri wa Kilimo yupo.
“Nimempa maagizo Waziri Mkuu mbolea isipofika huko ndani ya wiki hii, huyo anayehusika na kupeleka mbolea aachie kazi, labda tukianza kukimbizana tutajifunza.
“Nilishasema wale wote ninaowateua mimi wasifikiri mchezo, wanakuja kufanya kazi,” alisema Rais Magufuli.
Alisema mtu yeyote anayemteua akiona hawezi kufanya kazi, asikubali kuteuliwa kwa sababu uteuzi wake unalenga kutatua matatizo ya wananchi.
Rais Magufuli alionekana wazi kutoridhishwa pia na utendaji kazi wa Waziri wa Madini, Kairuki na kutaka afikishiwe salamu zake kwa sababu yuko likizo.
Alisema tangu Sheria ya Madini mwaka 2017, Wizara ya Madini haijamshawishi na aliwaagiza watendaji wa wizara hiyo kumfikishia waziri salamu kuwa bado hajamshawishi.
Kwa sababu hiyo tangu juzi usiku na jana, Dk. Tizeba amelazimika kutembelea maghala mbalimbali Dar es Salaam yanayohifadhi mbolea.
Akiwa katika ghala la mbolea Mbagala Dar es Salaam jana, Dk. Tizeba alisema hadi kufika jana jioni zaidi ya tani 2000 tayari zilikuwa zimekwisha kusafirishwa kupelekwa mikoa Rukwa, Mbeya, Katavi na Ruvuma.
“Tutahakikisha kabla ya muda tuliopewa na mheshimiwa Rais haujaisha mbolea itakuwa imefika katika maeneo husika kwa kiwango kinachohitajika.
“Tangu jana usiku (juzi) tumekesha hapa kwenye ghala la mbolea la Mohammed Enterprises kuhakikisha magari yanapakia na kuanza safari.
“Jana (juzi) usiku tulipakia magari 21 yenye mbolea zaidi ya tani 600 na leo (jana) tutapakia magari mengine 21 yatakayokwenda Rukwa na Makambako hadi Mbeya.
“Kuna tani nyingine 600 zitapakiwa, yote ni kuhakikisha inakuwapo mbolea ya kutosha katika mikoa ya nyanda za juu,” alisema.
Alisema Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limeungana na harakati hizo na jana walipakia tani 500 za mbolea kupeleka mikoan.
Waziri alisema TAZARA na Shirikali la Reli Tanzania (TRL) nao wametoa mabehewa 21 kwa ajili ya kupakia tani 900 za mbolea ambazo watazisogeza hadi Mbozi au mjini Mbeya kwa ajili ya kupelekwa maeneo mengine ya nchi.
Kampuni nyingine ya Premium Agrochem LTD ya Dar es Salaam hadi jana ilikuwa imesafirisha tani 1000 za mbolea kati ya tani 4000 zilizomo katika ghala lao.
Ilielezwa kuwa juhudi hizo zinazofanyika zitapunguza au kuondoa uhaba wa mbolea….
Kwa habari zaidi, jipatie nakala yako ya MTANZANIA.