Nora Damian – Dar es Salaam
WAKATI vifo kutokana na maambukizi ya virusi vya corona nchini China vikiongezeka na kufikia 106, inasadikika kuwa mtu mmoja mwenye dalili za virusi hivyo amepatikana Kenya.
Hadi kufikia juzi, vifo vilivyoripotiwa vilikuwa 106, huku idadi ya watu waliokumbwa na ugonjwa huo ikiongezeka na kufikia 4,515 wakiwamo 976 ambao hali zao ni mbaya.
Taarifa za jana zinaonyesha mwanafunzi mwenye dalili za virusi hivyo aliyekuwa akitokea mjini Guangzhou nchini China, alipofika Uwanja wa Ndege wa Jomo Kenyatta alipelekwa hospitali baada ya uchunguzi wa awali katika kituo cha afya kilichopo uwanjani hapo.
Juzi Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, ilisema inafuatilia mlipuko huo tangu ulipoanza China na kusambaa katika mataifa mengine.
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Afya ilisema hakuna mwathirika wa virusi vya corona nchini, lakini ikatahadharisha kutokana na mahusiano ya kijamii na kibiashara yaliyopo kati ya Tanzania na Bara la Asia, kuna hatari ya kuingia.
Serikali pia ilitoa tahadhari kwa Watanzania wanaosafiri kuelekea China, Thailand, Japan, Marekani na Korea Kusini nchi ambazo zimeripotiwa kuwapo maambukizi hayo.
Tahadhari pia imetolewa kwa wanaopokea wageni kutoka nchi hizo.
Virusi hivyo vilianza kusambaa mwishoni mwa mwezi uliopita katika Jiji la Wuhan lililopo Jimbo la Hubei nchini China na kwa sasa vimesambaa takribani majimbo yote nchini humo ingawa kwa viwango tofauti.
UBALOZI WA TANZANIA – CHINA
Taarifa ya Ubalozi wa Tanzania – China, inaonyesha hadi sasa hakuna Mtanzania aliyepata maambukizi ya virusi hivyo China na nchi nyingine zilizopo katika eneo la uwakilishi la ubalozi wa Tanzania kituo cha Beijing.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Serikali ya China imechukua hatua mbalimbali kudhibiti maambukizi ya virusi hivyo sambamba na kutoa kipaumbele katika suala la uwazi, kuujulisha umma kuchukua tahadhari, kudhibiti, kuzuia maambukizi na kutoa tiba ya ugonjwa huo.
Ubalozi umewashauri Watanzania waendelee kuwa na utulivu na kuondoa hofu, wazingatie maelekezo ya Serikali katika kuchukua tahadhari muhimu za kujikinga na maambukizi ya virusi hivyo.
“Ubalozi umekuwa ukifanya mawasiliano ya karibu na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kuhusu maendeleo ya ugonjwa wa corona.
“Ubalozi ungependa kuwajulisha kwamba Serikali ya China imetuhakikishia ina uwezo wa kudhibiti na kutibu virusi hivyo, hasa kutokana na uzoefu wake na utaalamu wa kutibu magonjwa ya milipuko, hususan Sars na ebola,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Aidha ubalozi uliwasihi Watanzania kuwasiliana haraka na ubalozi au mamlaka za vyuo, jimbo au jiji pale itakapojitokeza changamoto ya aina yoyote.
WANAFUNZI WA TANZANIA WAJIFUNGIA
Akizungumza na MTANZANIA, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watanzania wanaosoma katika mji wa Wuhan, Jacob Julius, alisema hadi sasa hakuna Mtanzania yeyote aliyedhurika.
“Kimsingi hakuna Mtanzania ambaye amepata tatizo la kuugua na tunamshukuru Mungu kwa hilo.
“Tahadhari tunayopewa ni kutojichanganya na watu, tunashauriwa kukaa ndani muda wote na kama mtu anataka kwenda nje basi awe na sababu ya msingi na anashauriwa kuvaa ‘mask’ pia.
“Tumeambiwa tuepuke sehemu za mikusanyiko, lakini kipindi hiki hakuna mwingiliano kwa sababu kuna baridi… tuko ndani tumejifungia,” alisema Julius.
Alisema kwa takwimu za juzi, Watanzania wanaosoma katika mji huo ni 436.
“Wanafunzi wengi ni ‘private’, kupata takwimu zao ni ngumu kwa sababu wengine wakija huwa hawaendi ubalozini,” alisema Julius.
Mmoja wa wanafunzi wanaosoma katika Jiji la Jiangxi ambaye kwa sasa yuko likizo, aliliambia MTANZANIA kuwa wameongezewa muda kwa wiki mbili.
“Likizo ilikuwa iishe tarehe 31, lakini tumetumiwa ujumbe wamesogeza mbele tarehe ya kufungua shule, na wamesema kama hali itaendelea kuwa mbaya, ikibidi tutasoma na kufanya mitihani kupitia ‘online’,” alisema mwanafunzi huyo.
WUHAN CHINI YA UANGALIZI
Jiji la Wuhan ambako ndiko chimbuko la virusi hivyo, limewekwa chini ya uangalizi maalumu hadi Serikali ya China itakapojiridhisha kwa lengo la kudhibiti kusambaa zaidi kwa maambukizi ya virusi hivyo.
Aidha China imetoa mwongozo wenye vipengele sita kwa raia wa kigeni kuepuka kuathiriwa na virusi hivyo.
Kwa mujibu wa mwongozo huo, raia wote wa kigeni wametakiwa wawe na subira na waendelee kukaa mahali walipo.
Kwamba kama itatokea haja ya kuwaondoa, watu wote watakaohusika katika mpango huo, lazima wawekwe kwenye karantini maalumu kwa siku 14.
“Muda huo unatosha kujiridhisha kuwa hawajapata maambukizi ya virusi. Baada ya muda huo, kama bado kutakuwa na hitajio la kuondolewa, itawasilishwa taarifa kupitia mamlaka za Serikali ya China kwa ajili ya kuridhia,” inasomeka sehemu ya mwongozo huo.
Pia Serikali hairuhusu ndege za kukodi kutua Wuhan wala usafiri wowote wa umma.
Aidha Serikali ya China hairuhusu kuwahamishia raia wa kigeni katika miji mingine kwa lengo la kuendelea kudhibiti maambukizi ya virusi hivyo.
Kuhusu wanafunzi ambao Visa zao zinamalizika wakiwa hawajaondoka China, mwongozo unaelekeza yafanyike mawasiliano na vyuo vikuu husika, Wizara ya Elimu au mamlaka za uhamiaji ili kupata suluhu.
Pia tarehe za kufungua vyuo vikuu vya Wuhan zimesogezwa mbele, hivyo wanafunzi waliosafiri nje ya mji huo wataendelea kubakia maeneo waliko hadi Serikali itakaporuhusu.
Changamoto zozote zitakazojitokeza kwa wanafunzi, wanaweza kuwasiliana na mamlaka za Serikali ya Jimbo la Hubei kwa uratibu wa misaada au mahitaji yoyote.
KENYA YATOA TAHADHARI
Jana Kenya ilitahadharisha raia wake kutokwenda mji wa Wuhan nchini China hadi mlipuko wa virusi hivyo utakapodhibitiwa.
Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo ilisema ilikuwa na mawasiliano na raia wake waliokwama katika mji wa Wuhan, ambao ni kitovu cha mlipuko wa virusi hivyo.
”Ubalozi unafahamu kuwa kuna raia wa Kenya 85 mjini Wuhan ambao wamesajiliwa ubalozini, hivyo unafuatilia kwa karibu hali hiyo,” wizara ilieleza kwenye taarifa yake.
Wakitoa maoni kwenye mtandao wa Twitter, Wakenya waliokwama mjini Wuhan walitoa wito kwa Serikali iwaondoe katika mji huo.
”Ni masikitiko tu kwa nchi yetu. Wiki ya pili sasa kwenye mji huu na hakuna lolote linalofanyika,” aliandika Cornelius Mulili kwenye ukurasa wa Twitter.
”Hali hapa ni mbaya. Ilichofanya Serikali yetu ni kutoa taarifa kwa vyombo vya habari pekee. Sitaki kueleza tunachokipitia hapa kimwili na kiakili,” alieleza Rono Kipkorir.
Tahadhari ya kusafiri imekuja siku chache baada ya maofisa nchini Ivory Coast kubaini mgonjwa aliyekuwa na dalili zinazofanana na mtu mwenye virusi vya corona. Hata hivyo haijathibitishwa kama mgonjwa huyo ana virusi hivyo.
Kenya ina moja kati ya viwanja vilivyo na pilikapilika nyingi barani Afrika na imeongeza umakini katika uangalizi wake. Inawapima abiria wote kutoka China.
VIRUSI VYA CORONA
Virusi hivyo vipya vinatajwa kuathiri zaidi wanyama.
Virusi hivyo vinasababisha matatizo ya kupumua.
Dalili zake zinasemekana kuwa ni homa, kikohozi kikavu, kisha baada ya wiki moja mwathirika anakuwa na matatizo ya kupumua na kuhitaji matibabu kwa haraka.
Virusi hivyo vipya vinafananishwa na vile vya Sars, ambavyo vilisababisha vifo vya mamia ya watu mwaka 2003.
Hadi kufikia sasa, hakuna tiba maalumu au chanjo dhidi ya virusi hivyo.
Hata hivyo Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Tedros Ghebreyesus, alisema ana imani China ina uwezo wa kudhibiti kusambaa kwa virusi hivyo.