27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

JKCI kuanza kupandikiza moyo kwa wagonjwa

Tunu Nassor – Dar es Salaam

TAASISI ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), inatarajia kuanza matibabu ya kupandikiza moyo kwa wagonjwa wenye mahitaji hayo.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuhusu miaka minne ya Rais Dk. John Magufuli madarakani, Mkurugenzi wa JKCI, Profesa Mohamed Janabi, alisema mpango huo utatekelezwa ndani ya miaka mitano kuanzia sasa.

Alisema maandalizi yaliyopo ni kutoa elimu kwa jamii namna ya kulipokea suala hilo kwa kuchangia moyo na kuandaa miundombinu mbalimbali kwa upandikizaji huo.

“Tumejiwekea lengo la kuanza kupandikiza moyo hapo baadaye, kuna baadhi ya wagonjwa ambao wanapotibiwa huonekana hawawezi kupona, lakini moyo wake ni mzima, hivyo ndugu na yeye kama watakubali wanaweza kuutoa moyo kwa mtu mwingine,” alisema Profesa Janabi.

Alisema kulingana na kukua kwa teknolojia, si lazima kupata mchangia moyo, kwa kuwa pia kuna uwezekano wa kupandikiza moyo wa bandia na mgonjwa akaishi.

Profesa Janabi alisema katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Tano, wamefanikiwa kuokoa zaidi ya Sh bilioni 86 kwa kufanya upasuaji wa moyo kwa wagonjwa 5,744 hapa nchini.

Alisema wagonjwa hao wangetibiwa nje ya nchi, Serikali ingetumia zaidi ya Sh bilioni 172 kulipia gharama hizo.

“Fedha hizi zimelipwa na bima, misaada ya wafadhili wa ndani na nje ya nchi, wagonjwa wenyewe na Serikali kugharamia asilimia kubwa ya matibabu kwa wale wasiokuwa na uwezo wa kumudu gharama za matibabu,” alisema Profesa Janabi.

Alisema katika kipindi hicho wagonjwa 300,836 wamepatiwa matibabu na kurudi nyumbani, huku 14,960 walilazwa.

Profesa Janabi alisema taasisi imeweza kufanya upasuaji mkubwa kwa kusimamisha moyo kwa wagonjwa 1,537 kwa mafanikio, ikiwa 92 walipoteza maisha sawa na asilimia sita tofauti na wastani wa kimataifa wa asilimia 13.

“Kwa upande wa upasuaji wa moyo kwa njia ya tundu dogo linalotolewa kwenye paja kwa kutumia mtambo maalumu wa cathlab, wagonjwa 4,207 walipatiwa huduma hiyo huku vifo vikiwa ni wagonjwa 42 sawa na asilimia 1.3,” alisema Profesa Janabi.

Alisema jumla ya wagonjwa 226 wamewekewa betri za aina mbalimbali za moyo kulingana na mahitaji waliyonayo.

Profesa Janabi alisema hata hivyo bado kuna wagonjwa ambao wanakwenda kupatiwa matibabu nje ya nchi kutokana na baadhi ya huduma kutokuwapo hospitalini hapo.

Alisema kutokana na hali hiyo, tayari Serikali imetoa Sh bilioni 4.6 kununua mitambo mbalimbali ya matibabu itakayosaidia huduma hizo kutolewa nchini.

Profesa Janabi alisema kutokana na taasisi hiyo kuelemewa na idadi kubwa ya wagonjwa, Serikali ya Tanzania na ile ya China zimeanza ujenzi wa hospitali kubwa ya moyo katika eneo la Mloganzila, Manispaa ya Ubungo, Dar es Salaam.

“Kwa siku taasisi inahudumia wagonjwa kati ya 300 hadi 500, hivyo ujenzi wa Hospitali ya Mloganzila umeanza rasmi kwa upembuzi yakinifu ili kupunguza msongamano katika taasisi yetu,” alisema Profesa Janabi.

Alisema wakati wanasubiri kukamilika kwa ujenzi huo, Rais Dk. John Magufuli alitoa jengo kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ili kuwapo kwa wodi na kliniki za watoto wanaotibiwa moyo.   

“Taasisi imenunua mashine mbalimbali mpya za matibabu ya moyo, zikiwamo za kuchunguza jinsi moyo unavyofanya kazi, kuchunguza mfumo wa umeme wa moyo unavyofanya kazi, ventilators, test gears, mashine ya X-Ray pamoja na vifaa vya chumba cha upasuaji,” alisema Profesa Janabi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles