Na JUDITH NYANGE,
JESHI la Polisi Mkoa wa Mwanza linawashikilia watu tisa kwa tuhuma za kujihusisha na uvunjaji wa nyumba na kuiba mali wilayani Ilemela.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi, alisema watu hao walikamatwa kutokana na doria na msako wa watu wanaojihusisha na uvunjaji wa nyumba usiku na kuiba mali iliyoanza Aprili 9, mwaka huu.
Alisema askari walifanya operesheni hiyo katika Kata ya Kirumba likiwamo soko la Kirumba, Kitangiri, Nyamanoro, Pasiansi, Ibungilo na Kawekamo wilayani Ilemela baada ya kupata taarifa kutoka kwa raia wema.
“Watuhumiwa waliokamatwa katika oparesheni hiyo ni Sandru Seleman(24) mkazi wa Ghana, Joseph Kichonge(28) mkazi wa Uhuru, Victor Sylvester (28) mkazi wa Igombe na Damali Samwel (29) mkazi wa Isenyi.
“Wengine ni Proches Samwel (20) mkazi wa Kigoto, Timoth Paul(53) na Ahmed Bajber (27)m wakazi wa Kilimahewa, Elias Samwel (35) pamoja na Daud James(20) wakazi wa Mecco,” alisema Kamanda Msangi.
Alisema katika operesheni hiyo pia ilikamatwa mali na vitu mbalimbali zikiwamo runinga.
Msangi alisema watuhumiwa wote wanahojiwa na jeshi la polisi na uchunguzi utakapokamilika watafikishwa mahakamani huku msako waa kuwakamata wahalifu wengine wa aina hiyo unaendelea.
Kamanda aliwataka wakazi wa Mkoa wa Mwanza kuendelea kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi kwa kutoa taarifa za wahalifu na uhalifu mapema waweze kukamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.