Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Damas Ndumbaro, ameitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Nchini (TIRA) kulinda haki za watumiaji wahuduma za bima ili kuifanya sekta hiyo iaminike na kuwa kimbilio la wananchi vijijini na mjini.
Dk. Ndumbaro amebainisha hayo leo Desemba 6, 2023 jijini Dar es Salaam alipokuwa anazindua taarifa ya utendaji wa soko la bima kwa mwaka 2022.
Amesema leo wamekutana na wadau wa bima katika tukio hilo muhimu na kuupongeza uongozi wa TIRA.
“Muwafikiwe watu wengi waliopo vijijini na mjini ambako watanzania wengi wanawahitaji hasa huduma ya bima na bima ya afya kwa wote ni haki za binadamu kila mtu apate huduma sawa awe tajiri au masikini,”amesema Dk. Ndumbaro.
Amesema TIRA katika kuandaa taarifa hiyo imeongozwa na mambo mbalimbali ikiwemo sehemu tatu ambazo zinahitaji kutoa elimu kwa wananchi
Ametaja sehemu hizo tatu kuwa ni kujenga ufahamu kwenye bidhaa zake na umuhimu wake ambapo bado uelewa ni mdogo, hivyo
wadau wote wachukue hiyo kama changamoto wafanye kuelimisha watu.
“Wadau kubuni bidhaa mpya za bima ambazo zitauzika sokoni,kazi ya bima kulinda mali na maisha ya watu,wadau wa bima mshirikiane na TIRA muweka pakegi za chini kila mwananchi aweze kumudu huduma za bima,” amesema.
Pia amewataka kuanzisha mifumo wa madai ya wateja, kwa kuwa uliopo bado hauna nguvu na kwa maslahi ya kila mmoja vizuri malalamiko yashugulikiwe mapema.
Ameongeza kuwa TIRA kwa kushirikiana na wadau kuweka mikakati ya kutoa huduma ya bima kidigital na kuhakikisha wananchi wanapata huduma stahiki na kudhibiti ubadhilifu
Dk. Ndumbaro amesema bima katika michezo ni eneo pana zaidi kuna wadau wengi, hivyo kuuanzia January Mosi, 2024 timu zote zinazo shirika Ligi Kuu wachezaji wote wawe na bima.
Naye Kamishina wa TIRA, Dk. Baghayo Saqware amesema Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ametia saini mswaada wa sheria ya bima ya afya kwa wote na sasa imekuwa sheria kamili wapo tayari kusimamia biashara ya bima na kufanya kazi nchini.
Amesema hadi kufikia Desemba 31, 2022 kulikuwa na jumla ya kampuni 36 za bima lakini zinaendelea kuongezeka hadi leo na wakala wa bima mwaka 2021 walikuwa 789 na mwaka 2022 ni 922.
“Mwaka 2022 tulipokea malalamiko 332 ambapo kampuni ya Insurance Group Tanzania limited ikiongoza kwa malalamiko 82 sawa na asilimia 59.0 na kampuni zingine, “amesema Kamishina Dk.Saqware.
Ametaja nchi ambazo zinafanya kazi na soko la bima nchini ni pamoja na Kenya, Afrika Kusini, India na Uingereza soko hilo linachangia uchumi kwa asilimia kubwa.
Aidha Dk. Saqware amesema wameanza bima ya kilimo nchini na wapo kwenye mazungumzo na wizara ya kilimo kwa sababu kuna asilimia 65 ya nguvu kazi ya nchi.
Ameongeza kuwa asilimia moja ni ufunguo wa uchumi kupitia sekta ya kilimo, hivyo wanatarajia Julai , 2024 itafanya kazi ambapo hadi sasa kampuni zinazotoa huduma ya bima ya kilimo ni tano.