ISTANBUL, UTURUKI
KIONGOZI wa ngazi ya juu nchini Uturuki, Yasin Aktay, amesema anaamini kuwa mwili wa mwandishi, Jamal Khashoggi, uliyeyushwa kwenye tindikali baada ya kuuawa na kukatwa katwa.
Akizungumza na gazeti la kila siku la Hurriyet, Atkay, ambaye ni mshauri wa Rais wa Uturuki, Racip Erdogan, amesema hitimisho pekee linaloingia akilini ni kuwa waliomuua mwandishi huyo wameteketeza mwili wake ili kufuta kabisa ushahidi.
Khashoggi, ambaye alikuwa mkosoaji mkuu wa utawala wa Saudia hususan sera za mrithi wa kiti cha ufalme mwanamfalme, Mohammed bin Salman, aliuawa ndani ya ubalozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul mnamo Oktoba 2 mwaka huu.
Mwandishi huyo alikimbilia Marekani mwaka 2017, akihofia usalama wake na huko alikuwa akiandika makala na maoni kwenye gazeti la Washington Post.
“Sababu ya kumkata vipande vipande ilikuwa ni kurahisisha kuyeyusha mwili huo kwa wepesi. Sasa tunafahamu kuwa si tu walikata kata mwili wake vipande bali waliuyeyusha kabisa,” amesema Aktay.
Licha ya kauli hiyo kutoka kwa kiongozi mkubwa, bado hakuna ushahidi wowote wa kiuchunguzi uliotolewa unaothibitisha kuwa mwili huo ulitoswa kwenye tindikali. Lakini mpaka hii leo, mwezi mmoja toka auawe, mwili wake bado haujapatikana.
Kauli hiyo imekuja wakati ambao mchumba wa Khashoggi, Hatice Cengiz, akiwataka viongozi wa dunia kuwachukulia hatua walioshiriki mauaji.
Aidha, vyombo vya habari nchini humo vimesema kuwa taarifa mpya zimeibuka kuwa mwanamfalme, Mohammed bin Salman, aliwaambia maofisa wa Marekani kwamba anamchukulia mwanahabari Khashoggi kama mshirika hatari wa kundi la Kiislamu lenye itikadi kali.
Mwanamfalme Mohammed ameripotiwa kusema hayo katika mazungumzo yake ya simu na maofisa wa Ikulu ya Marekani baada ya kupotea kwa Khashoggi.
Saudia hata hivyo imekanusha ripoti hiyo iliyochapishwa katika magazeti ya Washington Post na New York Times.
Waendesha mashtaka wa Istanbul wamethibitisha siku ya Jumatano kuwa mwandishi huyo alinyongwa, huku wenzao wa Saudia wakikiri kuwa mauaji hayo yalipangwa.
Huku hayo yakijiri mtoto wa kiume wa Jamal Khashoggi, Salah pamoja na familia yake wamewasili Marekani siku chache baada ya kukutana na Mwanamfalme, Mohammed Bin Salman.
Katika taarifa iliyochapishwa magazetini, familia ya Khashoggi imekanusha madai kwamba Khashoggi alikuwa mwanachama wa kundi la Muslim Brotherhood.
Familia hiyo pia imeongeza kwamba yeye mwenyewe aliyapinga madai hayo mara kadhaa katika miaka ya hivi karibuni.
“Jamal Khashoggi hakuwa mtu hatari kwa vyovyote. Madai hayo ni ya kushangaza sana,” ilisema taarifa hiyo.
Mpaka sasa hakuna makubaliano yaliyofikiwa kuhusu jinsi Khashoggi alivyofariki. Aliingia katika ubalozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul kushughulikia stakabadhi za kumwezesha kumuoa mchumba wake wa Uturuki, Hatice Cengiz.
Katikati ya wiki hii Serikali ya Uturuki ilisema kuwa aliuawa alipoingia ndani ya ofisi za ubalozi huo na mwili wake kukatwa katika vipande kulingana na utaratibu uliopangwa awali.
Vyombo vya habari vya Uturuki viliwahi kuripoti kuwa Khashoggi aliteswa kabla ya kuuawa.
Saudi Arabia imebadilisha kauli yake ya awali kuhusu mkasa wa kutoweka na kuuawa kwa Khashoggi.
Habari za kutoweka kwake zilipoangaziwa kwa mara ya kwanza Saudi Arabia ilisema kuwa Khashoggi alitoka ndani ya ubalozi wake mjini Istanbul akiwa hai.
Lakini baadaye ikakiri kuwa aliuawa na watu hatari waliokuwa wanatekeleza operesheni ya kikatili.
Kufikia sasa Saudia imewakamata washukiwa 18 ambao inasema watashtakiwa nchini humo.
Uturuki inataka washukiwa hao wafunguliwe mashtaka katika taifa hilo kwa sababu uhalifu ulifanywa katika ardhi yake.
Saudi Arabia imekosolewa vikali kufuatia mauaji hayo huku washirika wake wa karibu wakitaka kupewa majibu kuhusu mkasa huo.
Rais Donald Trump, amesema hajaridhika na kauli ya Saudia lakini hata hivyo hayuko tayari kuvuruga mkataba wa kuliuzia silaha taifa hilo.
Wanaharakati nchini Marekani wamezindua ombi la kutaka jina la sehemu ya barabara iliyopo karibu na ubalozi wa Saudi Arabia mjini Washington igeuzwe kuwa barabara ya Jamal Khashoggi.