Na THERESIA GASPER,DAR ES SALAAM
MKURUGENZI wa Mashindano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Salum Madadi, amezitaka timu za soka zinazoalika timu za nje kwa michezo ya kirafiki kufuata taratibu.
TFF imetoa agizo hilo kutokana na hivi karibuni Simba kuialika AFC Leopards ya Kenya na Biashara United kuwaalika Sony Sugar na kucheza nao mechi za kirafiki nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Madadi alisema kutokana na uwepo wa mialiko isiyofuata utaratibu, wameamua kuziandikia timu hizo na vyama vyote vya soka nchini kuwataka kufuata kanuni.
“Tumeandika barua kwa wanachama wetu na mashirikisho ya soka kutokana na mialiko ya hivi karibuni ya timu mbili za Kenya, Leopads na Sony Sugar, kuna baadhi ya mechi tumezuia zisichezwe kutokana na kutokukamilika kwa taratibu za mwaliko wa timu hizo,” alisema Madadi.
Alisema hairuhusiwi timu ya soka kutoka nje ya nchi kucheza mechi ya kirafiki au kushiriki mashindano mbalimbali bila kupata kibali kutoka katika chama au shirikisho la soka la nchi inayotoka.
“Tunafanya hivyo kwa sababu tuliwahi kupata adhabu ya kulipa faini FIFA kutokana na timu ya Twiga Stars kuongeza mchezo wa pili Cameroon bila kufuata taratibu baada ya kualikwa,” alisema Madadi.