32.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

Timu 12 kuanza kuvuna zilivyopanda VPL ikianza mikiki yake leo

WINFRIDA MTOI-DAR ES SALAAM

PAZIA la Ligi Kuu Tanzania Bara, msimu wa 2020/2021, linatarajiwa kufunguliwa leo kwa michezo sita kupigwa kwenye viwanja tofauti.

Mabingwa watetezi wa ligi hiyo, Simba itajitupa Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya kuumana na wenyeji wao Ihefu, mchezo utakaoanza saa 10:00 jioni.

Yanga itakuwa itakuwa nyumbani jijini Dar es Salaam kuumana na wageni wao Tanzania Prisons, mchezo utakaochezwa kuanzia  saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa Mkapa.

Michezo hii miwili inatarajiwa kuvuta hisia za mashabiki wengi wa soka hapa nchini.

Usajili ulifanywa na vikosi hivi kwa ajili ya msimu mpya, ndio unaochochea kiu ya mashabiki wa timu hizo kutamani kile kitakachofanyika dimbani.

Yanga imesajili sura mpya 12 miongoni   nyota sita wa kigeni, ikisaka makali zaidi katika msimu huo.

Wachezaji wakigeni wapya  waliotua Yanga ni Mukoko Tonombe na Tuisila Kisinda kutoka Klabu ya AS Vital ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo(DRC), Carlos Carlinhos(Inter Clube, Angola), Yacouba Songne(Asante Kotoko, Ghana) na Michael Sarpong, APR, Rwanda.

Wazawa ni Kibwana Shomari(Mtibwa Sugar), Yassin Mustafa(Polisi Tanzania) Bakari Mwamnyeto(Coastal Union), Abdallah Shaibu ‘Ninja'(huru), Zawadi Mauya(Kagera Sugar), Wazir  Junior(Mbao FC) na Farid Mussa, aliyemaliza mkataba na Klabu ya FC Tenerife ya Hispania. 

Lakini gumzo kuu kwa sasa kwa mashabiki wa Yanga ni Kisila ambaye alionyesha kiwango cha juu wakati akiichezea timu hiyo dhidi ya Aigle Noir ya Burundi, ukiwa ni mchezo wa kimataifa wa kirafiki, uliochezwa Uwanja wa Mkapa siku ya kilele cha tamasha la Wanajangwani hao maarufu Wiki ya Mwananchi.

Mbali ya kushuhudiwa sura mpya,  Yanga pia itaaongozwa na benchi jipya la ufundi.

Kocha Mkuu atakuwa, Zatko Krmpotic ambaye ni raia wa Serbia, msaidizi wake atakuwa Juma Mwambusi .

Sura nyingine mpya katika benchi hilo ni katika nafasi  ya kocha wa makipa ambayo klabu hiyo imemwajiri Vladimir Niyonkuru raia wa Burundi. 

Kwa upande wa Simba,  imesajili  nyota wanne wa kigeni na watatu wazawa.

Wakigeni ni Joash Onyango(Gor Mahia, Kenya ),Larry Bwalya(Power Dynamol), Chrispine Mugalu(Lusaka Dynamol, Zambia) na Bernard Morrison aliyemaliza mkataba na Yanga akiwa raia wa Ghana.

Wazawa ni David Kameta(Lipuli), Ibrahim Ame(Coastal Union) na Charles Ilafya, KMC.

Lakini matamanio zaidi ya mashabiki wa Wekundu hao ni kuendelea kushuhudia viwango bora vya Bwalya na Morrison.

Wachezaji hao wameng’ara katika michezo miwili rasmi ya kirafiki ambayo Simba ilicheza na kuibuka na ushindi dhidi ya Vital’O ya Burundi Uwanja wa Mkapa (6-0), AFC(6-0), Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha.

Pia walitakata katika mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Namungo, ambapo Simba ilishinda mabao 2-0, Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.  

Hata hivyo, timu hizo zinatarajia kukutana na upinzani mkali kutoka kwa timu wanazokutana nazo.

Prisons inafahamika kwa rekodi zake za kuonyesha upinzani  wa hali ya juu inapocheza dhidi ya miamba hiyo.

Kwa upande wa Ihefu ni timu ngeni katika ligi hiyo, baada ya kupanda daraja msimu uliopita hivyo itataka kuonyesha kwamba haikufuzu Ligi Kuu kwa kubahatisha.

Michezo mingine ya ligi hiyo itakayopigwa leo, Namungo itaumana na Coastal Union Uwanja wa Majaliwa, Lindi, Gwambina itakuwa na kibarua dhidi ya Biashara United, Uwanja wa Karume, Mara.

Mtibwa Sugar  itakuwa mwenyeji wa Ruvu Shooting,  Uwanja wa  Gairo, Morogoro, Dodoma Jiji itapimana ubavu na Mwadui, Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.

Ligi hiyo itaendelea kesho , ambapo Azam FC itaikaribisha  Polisi Tanzania Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles