33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Tumedhibiti uingizaji holela mayai kutoka nje – Prof Gabriel

Na Mwandishi wetu, Kilimanjaro

KATIBU Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia mifugo, Profesa Elisante Gabriel, amesema suluhu ya kudhibiti mayai yanayoingia nchini kiholela imepatikana na kuwataka Watanzania kupenda bidhaa zinazozalishwa nchini.

Profesa Gabriel alisema hayo akiwa katika Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, mara baada ya kutembelea shamba la ufugaji kuku wa mayai la Afro Farm Limited lenye kuku 20,000 wenye uwezo wa kuzalisha mayai zaidi ya makasha (trays) 500 kwa siku.

“Tumedhibiti uingizaji holela wa mayai kutoka nje ya nchi, soko sasa limepatikana na niseme udhibiti huo si nguvu ya soda, ni suala endelevu na tutaendelea nalo na tunazidi kujipanga, lakini sasa lazima tuhamasishe Watanzania wapende vya kwetu, ni suala ambalo kama wizara tumejipanga, mayai yanaleta afya bora na tunapoelekea uchumi wa viwanda tunahitaji watu wenye afya bora,” alisema Prof Gabriel.

Kuhusu wafanyabiashara wanaotozwa tozo Sh 1,000 kwa kila kasha moja la mayai wanapoyatoa Tanzania Bara kwenda Zanzibar, Prof. Gabriel aliesema tayari kanuni zimeshabadilishwa na tozo imepungua hadi Sh 100 kwa kasha moja.

“Nitoe angalizo kwamba siyo vizuri sana mnapokuwa mnafikiria kuwa ifike mahali kwamba msilipe gharama yoyote kwa Serikali, hilo hapana ni lazima mlipe kwa sababu mchango mnaotoa ndiyo unaojenga hospitali, barabara na shule,” alisema Prof. Gabriel.

Alitoa wito kwa vijana kujiajiri katika sekta ya kuku kwa kuwa ni sekta ambayo ni rahisi na yenye mahitaji makubwa kwa watu kwa ajili ya nyama, mayai na mbolea huku akiwataka pia wafugaji wote watambue kwamba lazima waangalie mnyororo wa mapato, gharama na faida ili kupata kupata mafanikio makubwa na kuongeza ajira.

Pia alisema ni vyema wafugaji wa kuku wa mayai kufuata kanuni bora za lishe ili waweze kuzalisha mayai bora badala ya kuwa na mayai mengi yasiyo na ubora na kubainisha kuwa kwa sasa Tanzania ina kuku milioni 83 na mayai bilioni nne huku mahitaji ya mayai yakizidi kuongezeka ndani na nje ya nchi.

Pia aliwataka wafugaji kutumia dawati la sekta binafsi lililo chini ya wizara hiyo kutatua changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo ikiwemo ya mitaji na miongozo kwa kuwa dawati hilo ni kiungo kati ya serikali na wadau wa sekta binafsi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Afro Farm Limited, Remen Kweka, aliwataka vijana kubadilisha fikra zao kwa kuhakikisha wanajifunza pindi miradi mbalimbali inavyoanzishwa maeneo mbalimbali nchini ili kujiwekea mazingira ya kupata ajira na kubuni mitambo mbalimbali ya uzalishaji.

 Kweka pia aliwaasa wadau wa ufugaji wa kuku katika miradi mikubwa kutumia Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) iliyo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupeleka sampuli za vyakula vya kuku ili kuhakikisha kuku wanakula vyakula bora ambavyo vitatoa matokeo chanya ya upatikanaji mayai yaliyo bora ambayo yanaweza kushindanishwa katika soko la kimataifa.

Amillen Kweka ambaye ni mke wa mkurugenzi wa shamba la Afro Farm alisema mradi huo umewawezesha kusomesha watoto shule pamoja na kuwasaidia akinamama kutokata tamaa na kuwafundisha juu ya ufugaji wa kuku wa mayai huku.

Shamba la hilo kwa sasa lina kuku 20,000 na kuzalisha mayai makasha zaidi ya 500 kwa siku, huku likiwa na uwezo wa kuhifadhi kuku 40,000 na linatumia mitambo ya kisasa katika kulishia kuku, kukusanya mayai pamoja na mbolea.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles