Na Esther Mnyika Mtanzania Digital
Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TNGP), Lilian Liundi ametoa wito kwa jamii kutoa elimu ya masuala ya jinsia kwa watoto tangu wakiwa shuleni ili kuondoa mfumo dume.Liundi amebainisha hayo Septemba mosi, jijini Dar es Salaam wakati wa semina ya Wahariri wa Vyombo vya Habari kuhusu Tamasha la Jinsia ya miaka 30 ya TNGP na Tapo la Kifeminia ambalo linatarajia kufanyika Novemba 7 hadi 10, mwaka huu.
Amesema lengo ni kuongeza uelewa na uwezo wa wanahabari juu ya tamasha hilo na kwamba ni moja ya jukwaa kubwa la ujenzi wa nguvu na harakati za pamoja.
“Kuna haja ya kutoa elimu ya usawa jinsia wote ifike wakati tukaelewe vizuri mifumo hii ili tukishirikiana kwa pamoja katika mambo mbalimbali ikiwemo kusaidia watu kushiriki katika ngazi ya jamii,” amesema Liundi.
Aidha, amesema lengo la tamasha hilo ni kubadilishana ujuzi, uzoefu na kusherehekea maendeleo mbalimbali yaliofanywa na TNGP.
Amesema TNGP imeanzishwa mwaka 1993 hivyo mwaka huu itatimiza miaka 30 nakwamba wamekuwa wakiendesha matamasha tangu mwaka 1996 hadi sasa wamefanya matamasha 14.
Amesema miaka 30 ya TNGP wanatarajia kuwa na mada mbalimbali kujadili na watu maaarufu ikiwemo mada ya tapo la ukombozi wa wanawake.
“TNGP imefanya maendeleo mbalimbali kuendeleza usawa wa jinsia katika nchini yetu tunaendelea kupambana zaidi mifumo dume tumeona madhara mengi,” amesema Liundi.
Ameeleza kuwa katika tamasha hilo la miaka 30 ya TNGP watakuwa na maonyesho mbalimbali na watu kuonyesha ubunifu wao, watakuwa na semina mbalimbali, siku ya mwanamke na mengine.
Liundi amesema katika tamasha hilo wanatarajia, kushiriki watu zaidi ya 1,500 na kuendelea, kujenga ushirikiano kati, kikanda na duniani.