Na Hadija Omary, Lindi
Timu ya wataalamu kutoka Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) ikiambatana na Taasisi ya Utafiti Wanyama pori Tanzania (TAWIRI) imewasili wilayani Nachingwea tayari kutekeleza agizo la Naibu Waziri wa Wizara wa Maliasili na Utalii, Meru Masanja la kuwataka kuweka Mizinga ya Nyuki katika mapito ya Tembo (Ushoroba) ikiwa ni njia moja wapo ya kuwaondoa Wanyama hao waaribifu na kurudi kwenye hifadhi.
Akizungumza na Waandishi wa Habari juzi kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea Katibu Tawala Wilaya hiyo, Omary Mwanga amesema kuwa mizinga hiyo itatumika kukabiliana na Wanyama waharibifu ambapo itawekwe kwenye vijiji ambavyo ni mapitio ya tembo kutoka kwenye hifadhi kuingia kwenye makazi ya watu itawekwa kwenye njia.
Hata hivyo, Mwanga amesema hiyo ni mara ya pili kwa wilaya yao kupokea wataalamu kwa ajili ya kupambana na Wanyama hao wahalibifu hasa katika kata zilizopata changamoto hizo.
“Kwa zaidi ya wiki mbili sasa kata za Namapwia, Nditi, Namikango, Lionja na nyingine kumekuwa na changamoto hiyo ya tembo, lakini wiki iliyopita tuliwapokea wataalamu kama hawa ambao walikuwa askari wa Tawa lakini hawa wa leo wanakuja kutoe elimu kati ya Wanyama waharibifu na Binadamu,” amesema Mwanga.
Kwa upande wake Afisa Mwelimishaji kutoka (TFS) Kanda ya Kusini Masasi, Underson Besisila amesema baada ya mizinga hiyo kuweka kwenye mapitio hayo tembo watashindwa kuendelea na safari watajikuta wanarudi kwenye hifadhi zao.
Hata hivyo, Besisila ameongeza kuwa licha ya mizinga hiyo kusaidia kukabiliana na tembo, pia itachangia kuingiza kipato katika vijiji vyao.
Kwa upande wake Mtafiti kutoka Taasisi ya utafiti wanyama pori (TAWIRI), Dk. Emanuel Masenga amesema kuwa Taasisi hiyo inatarajia kutoa mafunzo kwa wananchi 60 kutoka katika vijiji saba vilivyoathirika na tembo wilayani humo ambayo yatakuwa katika shemu mbili, kufundisha darasani na mafunzo kwa vitendo.
“Katika mafunzo haya tumekuja na vifaa mbali mbali ambavyo tutawafundisha kwa wananchi namna ya kuvitumia, lakini katika watu hao 60 tutakao wafundisha tutataka wawe mabalozi wa kuwafundisha watu wengine namna ya kukabiliana na wanyama hao wahalibifu bila ya kuleta madhara,” amesema.