33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Imani kubwa wanahisa Benki ya NMB wakiidhinisha gawio la Sh bilioni 96.7

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Wanahisa wa Benki ya NMB Plc wameidhinisha gawio la Sh bilioni 96.7 kwa mwaka 2021, huku wakiwa na Imani kubwa benki yao kuendelea kufanya vizuri zaidi mwaka huu.

Gawio la mwaka 2021 linatokana na kuongezeka kwa faida baada ya kodi kutoka Sh bilioni 206 mwaka 2020 na kufikia Sh bilioni 290 mwaka jana 2021.


Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi wa Benki ya NMB, Dk Edwin Mhede akionyesha Ripoti ya Mwaka 2021 ya Benkiya NMB baada ya kukabidhiwa na  Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna baada ya Mkutano Mkuu wa 22  wa wanahisa wa Benki ya NMB 2022 uliofanyika jijinini Dar es Salaam.

Katika Mkutano wake Mkuu wa 22 wa Mwaka uliofanyika mwishoni mwa wiki, wanahisa walipitisha kiasi hicho cha fedha ambacho ni sawa na malipo ya Sh 193 kwa kila hisa kwa kipindi kilichoishia Desemba 31, 2021 (wanahisa walipata gawio la Sh 137 kwa kila hisa kwa mwaka 2020).

Akizungumza na wandishi wa habari mara baada ya Mkutano Mkuu wa Mwaka mwishoni mwa wiki, Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna alisema Benki hiyo itaendeleza mwenendo wake wa kufanya vizuri kwa kuvuka malengo iliyojiwekea kwa mwaka huu pia.

Matarajio hayo yanatokana na matokeo mazuri ya robo ya kwanza ya mwaka huu ambapo Benki tayari imepata faida baada ya kodi ya Sh bilioni 101 ikiwa ni ongezeko la asilimia 55 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana.

“Ni kweli tumeuanza mwaka 2022 vizuri. Mafanikio makubwa ya kiutendaji kwa mwaka 2021 na matokeo mazuri ya robo ya kwanza ya mwaka 2022 ni kielelezo cha ufanisi mzuri unaotokana na utekelezaji makini wa mikakati yetu. Tutaendelea kutekeleza kwa umakini sana mikakati tuliyojiwekea na tunaamini kwamba malengo tuliyojiwekea kama benki tutayafikia na kuyapita mwaka huu wa 2022,” alisema Zaipuna.

Alisema kwa mahesabu ya kawaida, matokeo ya robo ya kwanza ya mwaka huu yanaleta picha kuwa utakuwa mwaka mzuri pamoja na changamoto zinazoendelea kujitokeza duniani.

“Kadri tunavyoendelea kukabiliana na mazingira ya biashara yanayobadilika kwa kiasi kikubwa, tumejipanga kwa umakini kupata matokeo mengine mazuri yatakayoendeleza rekodi yetu sokoni,” alisema.

Mwaka jana, Benki ya NMB ilifanikiwa kuvuka malengo yake katika vigezo karibu vyote vya kiutendaji, huku amana za wateja zikipanda hadi Sh trilioni 6.6 na  mikopo ikifikia Sh trilioni 4.8.

Benki hiyo pia imeweka rekodi katika sekta ya benki kwa kuwa na uwiano bora wa gharama za mapato wa asilimia 46 hadi kufika Desemba 31, 2021 ikiwa imepungua kwa asilimia 5 ikilinganishwa na mwaka 2020 (asilimia 51), huku uwiano wa mikopo chechefu (NPL) ukifikia asilimia 4 ya mikopo ghafi, kiwango ambacho ni chini ya kile kinachotakiwa na Mdhibiti (Benki Kuu).

Kwa ujumla katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita benki ya NMB ilishuhudia Mizania bora, ukwasi wa kutosha na viwango thabiti vya mtaji ambavyo viko juu ya viwango vya udhibiti. Benki pia ilitambulika kimataifa kama benki bora na salama.

Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya NMB, Dk. Edwin Mhede alisema; “Tumeendelea kudhihirisha ufanisi na ustahimilivu mkubwa kwenye biashara. Tutaendelea kujumuisha mafanikio makubwa yaliyopatikana, tuendelee kuzingatia kuwainua wafanyakazi wenye ujuzi unaofaa ili kuwasaidia kufanya kazi kwa ufanisi. Ninawahakikishia wanahisa wote wa Benki ya NMB, dhamira ya Bodi ni kufanya maamuzi sahihi ya kifedha na kuongeza faida kwa wanahisa wetu kwa miaka mingi ijayo” amesema.

Naye Zaipuna, aliongeza: “Matokeo mazuri tuliyoyapata mwaka 2021 yanatufanya tujiamini zaidi kuhusu uelekeo tuliouchagua baada ya kuhuisha mpango mkakati wetu wa muda wa kati mwaka 2020. Najisikia furaha kwa kila kitu tulichokifanya na kufanikiwa mwaka 2021 kwani tuliongeza thamani kwa wadau wetu. Mafanikio tuliyopata yasingewezekana pasipo kujituma na kujitoa kwa wafanyakazi wetu wenye uzalendo mkubwa wa kujituma kuwahudumia wadau wote.

Zaipuna aliwashukuru wafanyakazi, Bodi ya wakurugenzi kwa maelekezo, ushauri na uongozi, wateja wote, wanahisa, Benki Kuu ya Tanzania kwa miongozo na sera rafiki, Watanzania na jamii kwa ujumla kwa kuendelea kuiamini Benki ya NMB.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles