Na Sabina Wandiba, Mtanzania Digital
Serikali kupitia Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC), imeazimia kutokomeza magonjwa yasiyoambukiza ifikapo mwaka 2030.
Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Chakula na Lishe nchini, Dk. Ray Masumo, wakati akifungua Mafunzo ya siku moja kwa Waandishi wa Habari kuhusiana na ulaji
unaofaa na mitindo bora ya maisha katika kukabilina na magonjwa sugu yasiyoambukiza.
Dk. Msumo amesema, jamii inapaswa kuzingatia ulaji unaofaa ili kukabiliana na tatizo la magonjwa yasiyoambukiza.
“Pamoja na kuzingatia ulaji wa vyakula lakini pia jamii inapaswa kuepuka kula vyakula vyenye sukari nyingi, mafuta, chumvi nyingi, kufanya mazoezi, unywaji wa pombe, sigara na kuepuka kuwa na uzito mkubwa,”, amesema.
Amesema, mpangilio mbaya wa chakula umeonekana kuwa ni chanzo cha magonjwa sugu kama kisukari, shinikizo la damu na baadhi ya saratani.
Naye, Mkurugenzi wa Idara ya Mafunzo wa Taasisi hiyo, Dk. Esta Mkuba amesema kuwa, magonjwa yasiyoambukiza yamekuwa yakisababishwa na ulaji wa vyakula usiofaa.
Akasema, utafiti unaonyesha kuwa, kati ya vifo milioni 56.9 Duniani, vinavyotokea duniani, asilimia 71 vinatokana na mahonjwa sugu yasiyoambukiza.