Na MWANDISHI WETU-KAGERA
MAMLAKA ya Chakula na Dawa (TFDA), Ofisi ya Kanda ya Ziwa, imekifungia kwa muda kiwanda cha kutengeneza maji ya kunywa cha Kabanga Springs kilichoko Kamachumu, Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera.
Uamuzi wa kukifungia kiwanda hicho, umechukuliwa baada ya wakaguzi wa chakula wa TFDA Kanda ya Ziwa kubaini uapungufu makubwa ya usafi na utaalamu kinyume na kanuni za uandaaji wa chakula salama za mwaka 2006.
Akizungumza jana, Mkaguzi wa Chakula wa TFDA Kanda ya Ziwa, Nuru Mwasulama aliyataja upungufu huo kuwa ni uwapo wa vumbi katika mashine za kusindika, sakafuni na kwenye kuta za kiwanda hicho, wafanyakazi kutopimwa afya na kukosa sare, kukosekana kwa mfumo wa maji safi katika vyoo hali ambayo ilikuwa inasababisha uchafu katika eneo hilo.
Mwingine, ni uchakavu wa machujio ya maji katika sehemu ya kuchujia maji na kutofanya kazi kwa mfumo wa UV-Light hali ambayo inahatarisha usalama wa maji yanayozalishwa, uchafu uliokithiri katika maabara ya uchunguzi wa maji na kukosekana kwa taarifa zinazoonesha ufuatiliaji na upimaji wa ubora na usalama wa maji.“Kutokana na mapungufu makubwa yaliyoonekana wakati wa ukaguzi na yanayokinzana kwa kiasi kikubwa na kanuni za usindikaji salama wa chakula tumesitisha shughuli zozote za usindikaji wa maji katika kiwanda mpaka watakapo fanya marekebisho muhimu,” alisema Mwasulama.
Alisema mamlaka hiyo,itakuwa tayari kukifungua kiwanda hicho pale ambapo itajiridhisha kuwa maelekezo yote yalitolewa yamefanyiwa kazi.
Aliyataja baadhi ya maelekezo yaliyotolewa kwa wamiliki wa kiwanda kuwa pamoja na kuwapima afya wafanyakazi, kubadirisha machujio ya maji, kutengeneza mfumo wa UV- Light unaotumika kuangamiza vijidudu hatarishi ili kuhakikisha usalama wa maji yanayozalishwa, kufanya usafi katika chumba cha maabara na kutunza kumbukumbu za maabara, kutafuta mtaalamu wa chakula mara moja kwa ajili ya kusimamia uzalishaji salama wa maji na kuwapatia wafanyakazi sare za kazi.
“Tumemuagiza atutaarifu kwa maandishi pale atakapo maliza utekelezaji wa maagizo yote tuliyompatia. Tutakapo jiridhisha kuwa ametekeleza maagizo ya mamlaka tutamfungulia ili aendelee na uzalishaji,” alisema Mwasulama.
Mwisho
Mbaroni kwa kumpaka mtoto kinyesi cha mbuzi
Na JUDITH NYANGE-MWANZA
JESHI la Polisi Mkoa wa Mwanza, linamshikilia mkazi wa Mtaa wa Chakechake, Sospeter Rajabu (42), kwa kosa la kumpaka kinyesi cha mbuzi kwenye majeraha yaliyotokana kuungua moto mtoto wake, Neema Sospeter (10) mwanafunzi wa darasa la kwanza na kusababisha hali yake kuwa mbaya.
Taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi jana, ilisema mtuhumiwa alikamatwa juzi saa 10:30 jioni Mtaa wa Chakechake wilayani Nyamagana.
Alisema Sospeter anatuhumiwa kumpaka mavi ya mbuzi mtoto wake kwenye majeraha ya moto aliyoungua maeneo ya mapaja ya miguu yote miwili kwa muda wa wiki mbili na kusababisha majeruhi kuwa na hali mbaya kiafya ambapo wananchi walitoa taarifa polisi kuhusiana na tukio hilo, askari walifanya ufuatiliaji wa haraka hadi maeneo hayo na kufanikiwa kumkuta mtoto akiwa kwenye hali mbaya na kushirikiana na wananchi kumkimbiza hospitali na kumkamata baba wa mtoto.
“Huyu mtoto aliungua moto Agosti 4, mwaka huu saa 1:45 usiku Mtaa wa Kitangiri wilayani Iilemela ambapo alikuwa akiishi na mama yake kwani wazazi wake walitengana kwa muda mrefu, inadaiwa alimwagikiwa na mafuta ya taa alipokuwa akiweka kwenye kibatari na kuwasha na njiti ya kibiriti na moto kulilipuka kisha kumuunguza.
“Baada ya mama yake kukosa fedha za matibabu, aliamua kumpeleka kwa baba yake Mtaa wa Chakechake alipokua akiishi na mke mwingine ili amsaidie mtoto apate matibabu, lakini baada ya mtoto kufikishwa kwa baba yake hakupelekwa hospitali na badala yake alikuwa akipakwa mavi ya mbuzi na kusababisha hali yake kuzidi kuwa mbaya,” alisema Kamanda Msangi.
Alisema polisi wapo kwenye upelelezi na mahojiano na mtuhumiwa dhidi ya ukatili aliyokuwa akimtendea mwanae pindi uchunguzi utakapokamilika atafikishwa mahakamani, majeruhi amelazwa Hospitali ya Mkoa wa Mwanza Sekou Toure akiendelea kupatiwa matibabu na hali yake inaendelea vizuri.