BEKI wa Chelsea, Mwingereza John Terry, amedai kuwa timu yake ilinyimwa penalti katika mchezo wa juzi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya (UEFA) dhidi ya Dynamo Kiev ambapo timu hizo hazikufungana.
Katika mchezo huo wa kundi G uliopigwa Olympic Stadium nchini Urusi, kiungo wa Chelsea, Cesc Fabregas, aliangushwa ndani ya eneo la hatari na mlinzi wa Dynamo Kiev, Sergiy Rybalka, lakini mwamuzi Damir Skomina, aliamuru mchezo uendelee, jambo ambalo Terry anahisi si sahihi.
“Bado tupo vizuri, lakini nahisi tulistahili kushinda. Hatukua na bahati ya kushinda na tumesikitishwa kwa hilo. Tulikuja kushinda na tulicheza vizuri.
Ingawa Chelsea inashika nafasi ya tatu katika kundi hilo ikiwa na alama nne ilizoambulia katika michezo mitatu ya michuano hiyo, Terry anaamini kuwa kikosi hicho kitatinga hatua ya mtoano ikiwa kitafanya vizuri katika michezo yake ya nyumbani.
Katika mchezo ujao wa michuano hiyo mikubwa barani Ulaya, klabu hiyo ya jijini London itamenyana na Dynamo Kiev, mchezo uliopangwa kuchezwa mapema mwezi ujao.