24.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

TEKNOLOJIA YA KUPANDIKIZA FIGO INDIA SASA YAHAMIA MUHIMBILI

Na TUNU NASSORO-DAR ES SALAAM

UGONJWA wa Figo unaendelea kuitesa dunia siku hadi siku kutokana na kuongezeka kwa idadi ya wagonjwa.

Hadi sasa, zaidi ya asilimia 10 ya watu duniani tayari wanasumbuliwa na figo. Inakadiriwa kuwa ifikapo mwaka 2025 asilimia ya 70 ya wagonjwa watatokea Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Mkuu wa Kitengo cha Magonjwa ya Figo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Dk. Jaqueline Shoo anasema ukubwa wa tatizo hilo nchini umekuwa ukiongezeka.

Anasema jumla ya wagonjwa 200 wanapatiwa matibabu katika kitengo hicho ikiwa ni pamoja na kutakatisha damu.

Anasema wagonjwa wanaofikishwa MNH kwa matibabu wamekuwa wakipelekwa wakiwa katika daraja la tano, hatua  ambayo ni hatari kwa maisha yao.

“Utafiti uliofanyika mkoani Kilimanjaro umebaini kuwa asilimia 7.5 ya watu waliofanyiwa uchunguzi wanaugua ugonjwa wa figo,” anasema Dk. Jaqueline.

Anasema asilimia 60 ya wagonjwa wanaotibiwa hospitalini hapo wanahitaji upandikizaji wa figo.

Novemba 21, mwaka huu, MNH kwa kushirikiana na Hospitali ya BLK ya nchini India, kwa mara ya kwanza imefanikiwa kupandikiza figo kwa mgonjwa.

Upandikizaji huo umefanyika chini ya jopo la wataalamu kutoka hospitali zote mbili, ambapo mwanamke mwenye umri wa miaka 30 alipewa figo na ndugu yake mwenye umri wa miaka 27.

Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Profesa Lawrance Museru anasema hospitali hiyo ilianzisha mikakati ya kufanikisha tukio hilo hapa nchini.

Anasema kwanza walifanya uchaguzi wa wapi wataalamu wa hapa nchini watapata mafunzo ya upandikizaji.

“Tuliichagua hospitali ya BKL watupatie mafunzo ya upandikizaji wa figo. Tunawashukuru kutukubalia na kuwapokea wataalamu wetu bila gharama yoyote,” anasema Profesa Museru.

Anasema kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, waliandaa sheria itakayoruhusu kufanyika kwa upandikizaji huo nchini.

“Tuliandaa kanuni za kuruhusu upandikizaji huo ambapo zilichapishwa katika gazeti la serikali.

“Iliandaliwa kamati ya watu tisa kusimamia kanuni hizo na kuhakikisha kuwa hakuna biashara ya viungo vya binadamu itakayoingia katika upandikizaji huo,” anasema.

Anaongeza MNH inashirikiana na taasisi nyingine zikiwamo Chuo Kikuu Kishiriki cha Sayansi ya Tiba Muhimbili (Muhas), Ocean Road, Taasisi ya afya ya Ifakara, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) na Ofisi ya Mkemia Mkuu kuhakikisha upatikanaji wa vifaa vinavyotumika katika upandikizaji figo vinapatikana nchini.

Naye Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu anasema kuanzishwa kwa huduma hii nchini kutaleta nafuu kwa wagonjwa wengi zaidi kupata matibabu na hivyo kuokoa maisha ya wengi.

Anasema upasuaji huo mkubwa ni juhudi zilizoanzishwa na serikali ya awamu ya nne chini ya Rais Jakaya Kikwete, kuwekeza katika matibabu ya kibingwa nchini.

Anasema upasuaji huu umeokoa fedha ambazo zingelipwa nje ya nchi kugharimia matibabu na badala yake fedha hizo zitatumika kuleta maendeleo katika maeneo mengine yenye uhitaji,” anasema Ummy.

Anasema matibabu hayo yaliyofanywa na MNH hugharimu kati ya Sh milioni 80 hadi 100 kwa mgonjwa mmoja.

“Tulikuwa tukipeleka wagonjwa 35 kwa mwaka, hivyo mnaweza kuona kiasi cha fedha tutakachookoa kwa kufanya upasuaji nchini,” anasema Ummy.

Anasema takribani wagonjwa 400 wa figo wanafanyiwa utakatishaji wa damu (Renal Dialysis) katika vituo mbalimbali vya tiba hapa nchini, ambapo asilimia 60 wanaweza kuhitaji huduma ya kupandikiza figo.

Kutokana na hali hiyo, Waziri Ummy anawataka wananchi kujiunga katika mifuko ya bima ya afya ili kuweza kupata matibabu kwa urahisi.

Profesa Museru anasema wamemshauri waziri kuweka kipengele kitakachomruhusu mtu anayetarajiwa kufa kutoa viungo vyake kwa ajili ya matibabu ya wengine.

“Katika nchi nyingine zilizoendelea, sheria zao zinatoa ruhusa kwa mtu anayetarajiwa kufa kutoa viungo vyake kwa ajili ya matibabu ya watu wengine,” anasema Profesa Museru.

Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Upasuaji kutoka Hospitali ya BLK, Dk. Hardev Bhatyal anasema wataendelea kushirikiana na MNH na taasisi nyingine za afya nchini kuwajengea uwezo wataalamu wa afya.

“Tupo Mkituhitaji muda wowote tunawakaribisha kwani safari hii ya ushirikiano ndio kwanza imeanza,” anasema Dk. Bhatyal.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles