Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk. Hashil Twalib Abdallah, amesema kitakachokomesha bidhaa bandia ni ushirikishwaji wa wananchi, wenye viwanda na matumizi ya Tekonolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama).
Amebainisha hayo leo Desemba 12, 2023, jijini Dar es Salaam wakati akiwasilisha mada ya kudhibiti bidhaa bandia katika Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI).
Amesema CTI imeamua kujadili mada hiyo kwa kina ili kuona, je nini kinasababisha uwepo wa bidhaa bandia kwa wingi ndani ya masoko?
Amesema Rais Dk.Samia Suluhu Hassan anasisitiza kuweka mazingira wezeshi na rafiki katika ufanyaji wa biashara na uendelezaji wa viwanda katika jamii.
“Katika kufanya hivyo sera yetu ya viwanda inahitaji kuwa na ushindani ndani ya soko kwa hiyo miongoni mwa vitu vinavyopelekea kutokuwa na ushindani halali ndani ya soko ni uwepo wa bidhaa bandia,“amesema Dk.Abdallah.
Ameeleza kuwa CTI imedhihirisha kwamba ni miongoni mwa wadau wanaoweza kuifanya vita dhidi ya bidhaa bandia kuwa rahisi.
Ameongeza kuwa matumizi ya Tehama pamoja na mambo mengine wamejadili na kuona kitu ninkitu kinaweza kusaidia kuondoa bidhaa bandia sokoni.
Aidha amesema mjadala umejikita kwenye sera za viwanda,ubora wa viwanda lakini pia katika fursa zinazowezeshwa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuendeleza sekta ya viwanda, upatikanaji wa bidhaa bora katika soko la Tanzania.
Dk. Abdallah mesema wameelewa dhana nzima ya bidhaa bandia na jinsi ya kuidhibiti katika soko la Tanzania ili mlaji aweze kupata bidhaa bora na Serikali iweze kupata mapato stahiki na huduma katika jamii ziweze kuimarika.
Naye Mkurugenzi wa Kudhibiti Bidhaa Bandia wa Tume yaTaifa Ushindani ( FCC), Khadija Ngasongwa, amesema Mkutano wa AGM ni muunganiko wa CTI na baada ya kuchakata wakaona kuna umuhimu wa kuwa na mada ya kupambana na bidhaa bandia ili kuweza kumlinda mlaji na kufanya viwanda vyao viweze kushindana kutokana na nguvu ya soko.
Amesema katika mada yao kuu waliwasilisha rasmi asubuhi ya leo ikiwa na lengo ni kukumbushana na kuelimisha hasa kwenye dhana hiyo ya viwanda ni wajibu wao wote.
“Kuna umuhimu na ni mtambuka taasisi za Serikali kushirikiana na kampuni na viwanda ili kuweza kusaidia kuumbua wafanyabiashara wenye mbinu potofu na ambao hawaitakii mema serikali yetu na viwanda vyetu,”amesema Ngasongwa.
Ameeleza kuwa ongezeko la bidhaa bandia niasilimia chache na bidhaa ambayo imeongezeka kwa sasa hasa kwenye vipuli vya pikipiki , magari vifaa vya umeme ndio vimejaa kwa sababu soko limekuwa kubwa na tatizo kwenye dawa hivyo wanafanya uchunguzi watatoa taarifa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa CTI, Leodegar Tenga amesema kikao hicho kimelenga kuzungumzia umuhimu wa kupambana na bidhaa bandia ili viwanda vyao viweze kufanikiwa vinahitaji kuuza na kuleta ajira na kama kuna bidhaa bandia viwanda vinapata tabu kwa maana haviwezi kupata faida.
“Mazungumzo yeti no jinsi gani tunaweza kupambana na bidhaa bandia, sisi kama wenye viwanda ndiyo wenye bidhaa, tuna wajibu mkubwa sana kupambana na bidhaa bandia, “amesema Tenga.