29.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

TDA: TATIZO LA KISUKARI KWA WATOTO NI KUBWA

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM


UTAFITI uliofanywa mwaka 2012 unaonyesha asilimia 9.1 ya Watanzania wanaishi na ugonjwa wa kisukari huku wataalamu wakisema tatizo hilo linazidi kuwakumba watoto wadogo.

Kisukari ni mojawapo ya magonjwa hatari yasiyo ambukiza na hutokana na kiwango kikubwa cha sukari kwenye damu kuliko inavyotakiwa. Sukari ikizidi viwango vya kawaida kwa muda mrefu husababisha madhara mengi mwilini.

Kwa muda mrefu ilizoeleka dhana kwamba tatizo hilo huwakumba watu wazima imani ambayo imechangia wazazi kutokuwa na utaratibu wa kuwapima watoto wao ama kukubali kama wana kisukari.

Kutokana na hali hiyo Shirikisho la Vyama vya Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza (TANCDA) limeanza kutoa elimu kwa wanafunzi kwa lengo la kuwajengea ufahamu kuhusu ugonjwa huo.

Elimu hiyo ilienda sambamba na upimaji wa magonjwa ya kisukari na shinikizo la damu ambapo wanafunzi 1,352 wa Shule za Sekondari za Jangwani na Kisutu walipimwa magonjwa yasiyo ya kuambukiza kwa lengo la kubaini kama wana viashiria vya magonjwa hayo.

HALI ILIVYO KWA WATOTO

Msimamizi wa Huduma za Kisukari kwa Watoto kutoka Chama cha Kisukari nchini (TDA), Herieth Mganga, anasema ugonjwa wa kisukari kwa watoto upo lakini baadhi ya wazazi bado hawajakubali.

“Tatizo la magonjwa yasiyoambukiza ni kubwa na linakua sana, mzazi anapoona mtoto amepata kisukari anatakiwa aendelee kumfuatilia na hata kumsindikiza kliniki. Tuna watoto wanaofariki kwa sababu tu wazazi wameshindwa kuwafuatilia vizuri,” anasema Mganga.

Msimamizi huyo anasema hadi sasa kuna watoto 2,488 ambao wanatibiwa kisukari katika kliniki 34 zilizopo nchini.

Anasema lengo lao ni kufikia watoto wa kike katika shule za sekondari na kuwajengea ufahamu na kuwapima afya zao ili kujua kama wana viashiria vya kisukari na magonjwa mengine yasiyoambukiza.

DALILI

Anazitaja baadhi ya dalili za mtoto mwenye kisukari kuwa ni kukojoa mara kwa mara hasa nyakati za usiku kwa mtoto ambaye alikuwa hakojoi kitandani na kusikia kiu kupita kiasi.

Dalili zingine ni uchovu wa mwili, kiu kupita kiasi, njaa kila wakati, kupungua uzito au kukonda, kuwashwa sehemu za siri, na majipu mwilini.

Anasema vyanzo vyake vinavyoweza kuzuilika ni pamoja na kutojishughulisha mwili, unene, ulaji usiofaa, kuvuta sigara na msongo wa mawazo.

Naye Meneja Mradi wa TANCDA, Happy Nchimbi, anasema kasi ya magonjwa hayo inazidi kukua.

“Wanawake wengi wako kwenye hatari kubwa ya kuugua kisukari lakini bado hawajitambui, na kaulimbiu ya Siku ya Kisukari mwaka huu inasema ‘Wanawake na Kisukari’ ndio maana tumeamua kuja kutoa elimu kwa wanafunzi wa kike,” anasema Nchimbi.

Anasema magonjwa hayo kwa sasa yanakua kwa kasi hivyo inahitajika elimu hasa kwa watoto wanaokua na kuingia katika ngazi za familia.

ATHARI ZA KIAFYA

Kulingana na wataalamu ugonjwa wa kisukari usipodhibitiwa unaweza kusababisha upofu, figo kushindwa kufanya kazi, magonjwa ya moyo na mishipa ya damu na ya fahamu, uhanithi, vidonda miguuni, maambukizo ya figo, njia ya mkojo na sehemu za siri.

Athari nyingine ni Kifua Kikuu na ngozi, mimba kuharibika au mtoto kuwa mkubwa mno na kusababisha uzazi mgumu.

Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Kisutu, Sylivia Lyimo, anashauri zoezi hilo liendelee kufanyika katika shule zingine kwa sababu watoto wengi hawana ufahamu juu ya ulaji wa vyakula pamoja na kukosa mazoezi ya kutosha.

Mmoja wa wanafunzi wa kidato cha pili katika shule hiyo, Kisa Hebron, anasema zoezi hilo limemsaidia kutambua afya yake na kupata ufahamu wa kujilinda zaidi dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza.

Mwanafunzi mwingine wa Shule ya Sekondari Jangwani, Violeth Mlay, anasema elimu aliyoipata itamsaidia kuepuka ulaji wa vyakula vyenye sukari nyingi kama vile soda, juisi bandia, keki, biskuti na vingine visivyoruhusiwa.

Kwa ujumla tatizo la kisukari ni kubwa lakini linaweza kudhibitiwa kwa kutumia dawa na kubadili mtindo wa maisha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles