Na BENJAMIN MASESE-MWANZA
MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imetangaza bei mpya za mwingiliano wa mitandao ya simu hapa nchini kwa dakika moja kuanzia Januari mosi, mwakani huku ikizitaka kampuni za mitandao kuongeza dakika za maongezi kwa wateja wao.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa jana, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, James Kiliba, alisema uamuzi wa Serikali kutoa viwango vipya vitakavyodumu kwa miaka mitano (2018/2022), ni baada ya kufanya utafiti wa gharama za kampuni –fanisi (efficient operator) za uendeshaji wa mitandao ya simu namba tano wa mwaka huu.
Alisema mbali na kufanya utafiti, pia walikusanya maoni ya wadau husika kama ilivyoelekezwa katika kifungu namba 18(2) cha sheria ya namba 12 ya TCRA ya mwaka 2003 na kuunda jopo la wataalamu la kupitia maoni ya wadau juu ya gharama za mwigiliano zilizopendekezwa na TCRA.
Kiliba alisema kuanzia Januari mosi, gharama ya mwigiliano kwa dakika moja itakuwa Sh 15.60, mwaka 2019 itakuwa Sh 10.40, mwaka 2020 itakuwa Sh 5.20, mwaka 2012 itakuwa Sh 2.60 na mwaka 2022 itakuwa Sh 2.00.
Alisema Serikali imeamua kushusha viwango hivyo zaidi tofauti na miaka mitano iliyopita ambapo kwa mwaka 2013 ilikuwa ni Sh 34.92, mwaka 2014 ilikuwa ni Sh 32.40, mwaka 2015 ilikuwa ni Sh 30.54, mwaka 2016 ilikuwa ni Sh 28.57 na mwaka 2017 ilikuwa ni Sh 26.96.
Kiliba alisema kabla ya viwango hivyo, Serikali ilitoa ruhusa kwa wenye kampuni za mitandao ili kukaa na kupendekeza bei lakini walishindwa kuelewana kutokana na mvutano wa biashara yao ndipo ilipoamua kufuata sheria na kufikia kutangaza bei hizo.
“Kushuka kwa gharama za mwingiliano kutasababisha ongezeko la dakika za maongezi na hivyo kuongezeka kwa mapato ya watoa huduma na ya Serikali kutokana na ongezeko la matumizi ya huduma mbalimbali za mawasiliano.
“Kama TCRA inatarajia kwamba, kupungua kwa gharama za mwingiliano kutasababisha kushuka kwa gharama za kupiga simu kwenda mitandao mingine na hivyo kupunguza ulazima wa wateja kuwa na laini zaidi ya moja kwa kuhofia gharama kubwa kwenda mitandao mingine.
“Awali nimewaeleza laini zinazotumika hadi sasa zimefikia zaidi ya milioni 40, hivyo kuongezeka kwa matumizi ya huduma za mawasiliano kutawezesha na kuongeza ufanisi katika shughuli za sekta nyingine kiuchumi na kijamii, wito wetu kama mamlaka ni kuwataka watoa huduma kuzingatia viwango vipya, vinginevyo sheria zitachukua mkondo wake,” alisema.
Pia alisema gharama zilizotolewa ni bei za jumla ambazo kampuni za simu hulipana ili kufidia gharama ya kupokea simu inayotoka mtandao mwingine na kuifikisha kwa mteja aliye ndani ya mtandao unaopigwa na viwango hivyo si bei ya rejereja anayotozwa mteja anapopiga simu.
IDADI YA SIMU ZA MIKONONI, MEZANI
Pia alisema Tanzania imeendelea kupata mafanikio katika sekta ya mawasiliano ambapo idadi ya watoa huduma na watumiaji imeendelea kuongezeka na kukuwa kwa biashara na ujasiriamali.
“Kwa upande wa mawasiliano ya simu, idadi ya simu za mezani imeongezeka kutoka 16,238 mwaka 1961 hadi 127,976 Septemba, mwaka huu, kila mwaka kulikuwa na ongezeko fulani lakini kasi ipo juu kwa upande wa watumiaji wa simu za mkononi kwa sababu zimeongezeka kutoka laini 2,963,737 kwa mwaka 2005 hadi laini 40,002,364 kufikia Septemba, mwaka huu.
“Katika upande wa simu za kufanya miamala za kifedha, huduma hii nayo imekuwa tangu mwaka 2008 kwa sababu ilikuwa ni kampuni moja tu lakini hadi leo zimefikia kampuni sita ambazo ni Airtel, Tigo, Halotel, TTCL, Vodacom na Zantel, watumiaji wa miamala walikuwa 17,639,349 kwa mwaka 2015, lakini hadi Septemba, mwaka huu wamefikia 21,611,855.
“Watumiaji wa intaneti wameongezeka kwa kasi kutoka 1,681,012 kwa mwaka 2005 lakini hadi Septemba, mwaka huu wamefikia 22,841,903, hili ni ongezeko kubwa la muda mfupi. Serikali tunaendelea kuboresha miundombinu ili kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia,” alisema.
Kuhusu mitandao ya kijamii, alisema kuna watu wanaitumia isivyo kwa kuweka vitu ambavyo si vyake kweli na vingine vinakwenda kinyume na maadili ya Watanzania ikiwamo picha za utupu na aliliomba Jeshi la Polisi kuwa makini kwa kuwakamata wahusika.
“Sisi TCRA tunatoa miongozo na kudhibiti watumiaji lakini hatuwezi kukamata ila tunasaidiana na polisi kuwakamata wahusika, hivyo kila mnachokiona kinakwenda kinyume huwa tunahusika na wengine wamekamatwa, si kwamba kila kitu tutakisema hatua zilizofikiwa, tunaomba ushirikiano hasa waandishi wa habari,” alisema.
FAINI STAR TIMES
Akizungumzia faini za chaneli za bure za televisheni, alisema baadhi ya kampuni zenye ving’amuzi zimekuwa zikikiuka kanuni ya 14 (2)(a) ya mwaka 2011 kwa kushindwa kuonyesha chaneli tano za bure huku zikiwatoza wateja wao.
Alisema baada ya ufuatiliaji wa kampuni hizo, TCRA ilibaini Kampuni ya Star Media Tanzania Ltd inayomiliki king’amuzi cha Star Times haionyeshi chaneli hizo huku ikiwatoza watazamaji wake ndipo Desemba 22, mwaka huu Serikali iliamua kuitoza faini ya Sh milioni 100 kwa kitendo hicho.
Alisema zipo kampuni nyingine za ving’amuzi zinaendelea kufuatiliwa kwa ukaribu na kuwataka Watanzania kutoa taarifa pale chaneli tano ambazo ni TBC 1, ITV, EATV, Channel Ten, Star TV na Clouds TV zitakaposhindwa kuonekana ili sheria ziweze kuchukuliwa haraka.