*Atoa neno kwa TTCL
Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye ameiagiza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kujenga jengo la kudumu ndani ya viwanja vya maonyesho ya Kimataifa ya Biashara (DITF) ili wananchi waweze kupata huduma iliyo bora.
Akizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya kufanya ziara ya kutembelea mabanda mbalimbali amesema ameshaongea na Mamlaka ya Biashara Tanzania (TANTRADE) juu ya TCRA kuwa na ofisi ya kudumu ndani ya uwanja kwa kuwa wanamajukumu makubwa kwa jamii.
Nnauye amesema uwepo wa banda la kudumu la TCRA ndani ya maonyesho hayo litarahisha wananchi kupata huduma kwa wakati, kupunguza gharama ambazo zinatumiwa na mamlaka hiyo kila mwaka wakati wa maonyesho..
“TCRA ni wadau muhimu kwa Watanzania kama mtakuwa na jengo lakudumu mtaweza kuwasaidia walio wengi kuweza kupata huduma sahihi,” amesema Nnauye.
Ameongeza kuwa Tanzania ni sehemu sahihi ya uwekezaji hivyo mawasiliano yakipatikana katika ubora itaongeza ubora zaidi.
Aidha, amesema licha ya makampuni ya nje kuwekeze Tanzania, TCRA isisite kutoa huduma kwa Watanzania .
“Pamoja na huduma zote mnazotoa Mtanzania anatakiwa apewe kipaumbele katika suala zima la utoaji huduma,” amesema Waziri Nnauye.
Ameongeza kuwa ni jukumu la vyombo vya habari kutangaza vitu vizuri vilivyopo Tanzania ili kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan.
Katika hatua nyingine Waziri Nnauye aametembelea banda la Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) na kuzitaka taasisi za Serikali kutumia teknolojia ya TEHAMA ya video Conference katika mikutano yao.
Amesema TEHAMA itasaidia kupunguza gharama kwa serikali na itawawezesha kuwasiliana kwa urahisi zaidi kwa watumishi wao.
“Serikali ipo tayari kuwawezesha kutekeleza mpango huo wa TEHAMA,” amesema Nnauye.
Nae Mkurugenzi wa TTCL, Mhandisi Peter Ulanga amesema wao ndio wa kwanza kutekeleza agizo la serikali la kutumia video conference katika mikutano, huku wateja wengi wakiwa jijini Dodoma.