Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
MTANDAO wa Madeni na Maendeleo Tanzania (TCDD) , umeliomba Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania liwe linakopa kwa niaba ya nchi kwani kwakufanya hivyo kutaongeza uwajibikaji kwenye mikopo inayokopwa na serikali .
Hayo yamesemwa Jijini Dar es Salaam leo na Mkurungezi wa TCDD, Hebron Mwakagenda katika mkutano uliokutanisha viongozi mbalimbali wa dini pamoja na wadau wa Maendeleo ulioenda sambamba na uzinduzi wa ripoti ya Hali ya deni iliyolenga kujadili taarifa kuhusu deni la taifa na Maendeleo .
Amesema Bunge linapaswa kuizinisha kwa kutoa ruhusa au kukataa huku Waziri wa fedha akipeleka mapendekezo kwa kamati kwa kueleza kuwa anataka kukopa sehemu fulani kwa ajili ya kitu fulani.
Mwakagenda amesema Bunge ndilo linapawa kukopa kwa niaba ya nchi mikopo mbalimbali ya ndani na nje Ili kusimamia uwajibikaji wa mikopo hiyo badala ya utaratibu wa sasa wa Waziri wa fedha kukopa kwa niaba ya nchi.
“Baada ya Waziri wa fedha kueleza kuwa fedha hizo zitakopwa wapi kwa ajili ya kitu gani ndipo bunge nzima linakaa na kujadili kwa kutoa hoja za kukubali au kukataa,”.
Na kuongeza
“Kinachofanyika kwa sasa katika hotuba ya Waziri wa fedha anasoma hotuba yake akieleza kuwa atakusanya kiasi hiki ndani na kukopa kiasi hiki kwa ujumla sisi tunachotaka ni kutoa maelezo kuwa fedha hizi zinakwenda sehemu fulani na zimetoka sehemu fulani,”aliongeza Mwakagenda.
Akizungumzia kuhusu Hali ya deni ya kwa nchi za Afrika Mashariki alisema hali ni mbaya zaidi katika nchi ya Kenya, Uganda, na Rwanda huku Tanzania ikionekana kuwa na unafuu.
Alisema nchi hizo zimekuwa zikiendelea na kupelekea kupata maendeleo hivyo zimekuwa zikikopa ili kujenga miundombinu, Madarasa,Madaraja,Reli, pamoja na Barabara ambapo fedha nyingi hutumika huko.
“Uchumi wa Tanzania umebadilika kwa sasa awali kulikuwa na mfumo wa kijamaa ambapo serikali ilikuwa ikiendeshwa kwa kitu, kwa Kenya mfumo wao umekuwa ukiendeshwa na sekta binafsi jambo ambalo limepelekea Uchumi wao kukua kwa haraka,”alisema
Mwakagenda amesema Nchi ya Tanzania imekuwa na rasilimali nyingi huku kwa Sasa ikija kwa kasi zaidi na kusisitiza kuwa kinachotakiwa kwa sasa serikali ni kuwa na nidhamu ya ukopaji.
Awali Mwenyekiti wa TCDD, Piter Maduki akizungumza mara baada ya kuzindua taarifa hiyo alisema kwa sasa deni la Taifa ni imilivu ambapo aliwaomba watanzania kutambua kuwa fedha hizo ni kwa ajili ya manufaa ya wote hivyo ni vyema kutumika vizuri katika utekelezaji na hatimaye kuleta mafanikio makubwa zaidi.
Akiwasilisha taarifa ya ripoti hiyo Mwalimu wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu huria Dkt Felician Mutasa alisema kukopa sio dhambi kwani hata nchi tajiri zimekuwa zikikopa huku akieleza ni jambo la kawaida katika mifumo ya kiuchumi.
Amesema kinachotakiwa kuzingatia fedha zinapokopwa ni vema zikaelekezwa katika miradi iliyokusudiwa zaidi.
Amesema ripoti hiyo pia imependekeza kuwepo kwa wigo mpana wa Kodi kwani ndo kitu pekee kitakachoifanya Serikali kujiendesha kuliko msaada na mikopo hivyo ni vema serikali ikaweka nguvu zaidi.