Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM
KAMPUNI ya Bia Tanzania (TBL Group) chini ya Kampuni ya kimataifa ya ABInBev, kwa kiasi kikubwa imetekeleza malengo ya mkakati wa utunzaji wa mazingira katika kupunguza matumizi ya maji, kwa kutumia nishati mbadala na kupunguza uchafuzi wa hewa kupitia mchakato wa uzalishaji wa viwandani
Akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Maji Duniani ambayo inaadhimishwa leo, Mratibu wa Mazingira wa ABInBev Afrika, Anitha Gerald, alisema mafanikio hayo yametokana na matumizi ya teknolojia za kisasa kuanzia kwenye uzalishaji na ufuatiliaji wa mifumo bora ya uzalishaji inayotumika katika viwanda vya ABINBEV duniani kote.
Alisema kampuni inahakikisha mpango shirikishi wa wafanyakazi wake kuelewa umuhimu wa utunzaji wa mazingira unatekelezwa kwa vitendo wakati wote, jambo ambalo TBL Group imefanikisha kwa kiasi kikubwa katika viwanda vyake vilivyopo mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya, Mwanza, Arusha na Kilimanjaro.
“Kampuni inaliangalia suala la utunzaji wa mazingira si kwa kiwango cha masilahi ya viwanda vyake tu, bali kwa jamii nzima kwa kuwa sera yake ya kujenga dunia maridhawa ambayo inashahabiana na Malengo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs) na suala la utunzaji wa mazingira na vyanzo vya maji ni moja ya suala ambalo limepewa umuhimu mkubwa,” alisema Gerald.
Aidha, kuhusu matumizi ya maji, Gerald alisema mafanikio makubwa yamepatikana katika eneo hili kwa kuwa mpaka sasa matumizi ya maji katika viwanda vya kutengeneza vinywaji vya TBL Group yamepungua, wakati huo mifumo ya utakatishaji wa maji taka ikitumika lengo likiwa ni kutumia maji kidogo zaidi katika shughuli za uzalishaji na zisizo za uzalishaji.
Hivi sasa kampuni inalipa kipaumbele zaidi suala la kushirikiana na Serikali, wadau na wananchi kuhakikisha inakabiliana na changamoto ya upungufu wa maji ambayo inatishia kujitokeza kutokana na mabadiliko ya tabia nchi na sehemu nyinginezo duniani. Kutokana na hilo, Mratibu huyo wa Mazingira wa ABInBev Afrika, alitoa wito kwa Watanzania wote kuzingatia suala la utunzaji wa mazingira hususani kupanda miti, kulinda vyanzo vya maji na kutumia maji kwa umakini hususani katika kipindi hiki ambacho tunaelekea kwenye Tanzania ya viwanda, lengo kuu likiwa ni kupata viwanda bora vinavyozingatia utunzaji wa mazingira kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo.