26.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

Tawla yawapiga msasa wajasiriamali wanawake matumizi ya ardhi

Janeth Mushi, Arusha

Wanawake kutoka Vikundi vya wajasiriamali (Vicoba), katika kata mbalimbali zilizopo Halmashauri ya Wilaya ya Meru wamepatiwa mafunzo juu ya matumizi ya ardhi iliyosajiliwa ili kujiinua kiuchumi.

Mafunzo hayo yalitolewa mwishoni mwa wiki na Chama cha Wanawake Wanasheria Tanzania (Tawla), tawi la Arusha, chini ya mradi wa kukuza upatikanaji wa haki za ardhi na mali kwa wanawake unaotekelezwa na chama hicho na kufadhiliwa na Taasisi ya Foundation For Civil Society.

Kwa mujibu wa Mratibu wa Tawla Mkoa wa Arusha, Happy Mfinanga, lengo la mafunzo hayo ni kuwafundisha wanawake hao wajasiriamali namna wanavyoweza kutumia ardhi iliyosajiliwa kisheria kujiinua kiuchumi pamoja na kuwaelimisha umuhimu wa kuwa na hati miliki za maeneo yao ili kupunguza migogoro ya ardhi pamoja na kuepuka kunyang’anywa.

Awali Meneja wa Benki ya NBC tawi la Meru, Florence Ng’wavi, akiwasilisha mada juu ya umuhimu wa kuwa na ardhi iliyosajiljwa na namna ambavyo benki inaweza kusaidia vikundi vya ujasiriamali kuendeleza ardhi iliyosajiliwa,alisema kupitia taasisi mbalimbali za kifedha ni rahisi kupata mikopo itakayowasaidia kujiinua kiuchumi na kukuza mitaji yao ya biashara.

Aidha, Meneja huyo aliwatahadharisha juu ya matumizi  mabaya ya mikopo ikiwa ni pamoja na kupeleka katika vitu visivyozalisha na kuwasihi wahakikishe wanatumia kwa malengo waliyokusudia mikopo wanayochukua katika taasisi za kifedha.

“Nawasihi kopeni kwenye taasisi zilizopo kisheria na zenye vibali na leseni ili kuepuka matapeli ambao wakati mwingine wanawakopesha ila unajikuta umeshindwa kurejesha wanachukua mali zenu, matajiri tunaowaona wameinuka kupitia mikopo hivyo tusichukue mikopo kupeleka kwenye vitu ambavyo havizalishi,” amesema.

Naye Meneja Uhusiano na Mikopo kutoka tawi hilo, Hamida Joshua, amesema vikundi vyenye akaunti benki ni muhimu kwani watakuwa na uhakika wa usalama wa fedha zao na kuwataka kutoa elimu juu ya umuhimu wa kuhakikisha wanakuwa na hati miliki za maeneo yao ili kupunguza migogoro ya ardhi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles