Na Mwandishi Wetu, Arusha
CHAMA Cha Wanawake Wanasheria Tanzania (TAWLA), tawi la Arusha, kimekutanisha madiwani kutoka majimbo matano ya mkoani Arusha na kuwapa mafunzo ya masuala ya uongozi.
Tawla ilikutanisha madiwani hao kupitia mradi wa kuongeza ushiriki wa wanawake na vijana katika nafasi za uongozi wa kisiasa(IDIEP) ambao wanautekeleza katika mikoa mbalimbali nchini unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya(EU).
Akizungumza katika mafunzo hayo, mmoja wa watekelezaji wa mradi huo kutoka Tawla na Mwanasheria wa chama hicho, Ekael Michael, alisema washiriki hao wametoka majimbo ya Longido, Arumeru Mashariki, Arumeru Magharibi, Karatu na Monduli.
Amesema lengo ni kukuza ushiriki wa makundi hayo katika kuwania nafasi za uongozi na kutoa mafunzo ili kuhakikisha wanawajengea viongozi hao uwezo zaidi na uelewa ili wanapotekeleza majukumu yao waweze kushirikisha wananchi.
“Leo tulikuwa tukitoa mafunzo ya uongozi kwa madiwani hao na lengo ilikuwa ni kuhakikisha pamoja na kwamba wao ni viongozi,tunaweza kuwajengea uwezo ili waweze kushirikisha wananchi na kutekeleza majukumu yao katika jamii zao kwa usahihi,” amesema.
Mmoja wa madiwani hao, Dastan Panga kutoka Kata ya Qurus wilayani Karatu, amesema yeye ni mnufaika wa mradi huo kuanzia awamu ya kwanza ambapo mradi mradi ulianza kwa kuhamasisha vijana na akina mama kuwania nafasi katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2019.
“Mradi huu umewezesha wanawake na vijana kushiriki kuwania nafasi za uongozi,na Uchaguzi Mkuu 2020 nikiwemo mimi kwani awali sikuwa kiongozi ila baada ya mradi niliwania nafasi ya udiwani na sasa ni diwani.
“Tunawashukuru Tawla kwani walitutuma vijijini kuelimisha jamii faida za ushiriki wa wanawake na vijana katika makundi haya na sasa mwamko ni mkubwa na mradi umetujengea uwezo wa kusimamia haki za wananchi kuanzia ngazi za chini,” amesema.
Naye Diwani wa VitiMaalum kutoka Tarafa ya Longido na Mwenyekiti wa Kamati ya elimu, afya na maji, Upendo Ndoros, alisema mafunzo hayo yamwajangea uwezo na kuwa viongozi bora hasa katika kuwashirikisha wananchi.
“Nimefurahi kupata mafunzo haya yametusaidia tunashukuru Tawla,yatatusaidia kuendelea kuwa viongozi bora katika maeneo tunayotoka.
“Tuna changamoto za jumla kwa wanawake tunaowaongoza lakini pia kwenye jamii,kwamba kuna changamoto za mfumo dume na mashirika haya yanatusaidia na mafunzo haya ni muhimu bila elimu hatutaweza,” amesema Ndoros.
Kwa upande wake Diwani kutoka Kata ya Monduli Juu,Thomas Meyan, alisema miongoni mwa mambo yanayokwamisha shughuli mbalimbali za uongozi na maendeleo kwa ujumla ni pamoja na viongozi wanaotokana na rushwa.
Amesema uongozi unaotokana na rushwa uanweza ukakwamisha maendeleo katika jamii kwani mtu aliyeingia madarakani kwa kutumia rushwa hataweza kutekeleza matakwa ya wananchi.
“Hatakuwa anawajali wale wnaanchi kama jinsi kiongozi ambaye hajaingia kwa rushwa atakavyokuwa anatekelza majukumu yake kwa usahihi kwa sababu atakuwa anawashirikisha wananchi.
“Tumejifunza katika mafunzo haya kuwa katika uongozi tunahitaji pia ushirikishwaji,uongozi unahitaji uwashirikishe wananchi unaowaongoza na uwape nafasi watoe maoni yao ili yaweze kujenga,” amesema.