*Yawapandisha vyeo Maafisa 60 huku Askari 146 nao wakipanda
*Haijawahi kutokea tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo
Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imewapandisha vyeo Maafisa 90 na Askari waliokuwa na vyeo vya chini 146 ikiwa ni kutekeleza agizo la Rais Samia Suluhu Hassan ambaye aliagiza kupandishwa vyeo kwa maafisa na askari waliodumu muda mrefu kazini bila vyeo.
Utekelezaji wa agizo hilo umeanza Oktoba 18, mwaka huu ambapo Kaimu Kamishna wa Uhifadhi TAWA, Mabula Misungwi Nyanda amewatunuku na kuwapandisha vyeo maofisa Maafisa 90 na Askari 146 (wa vyeo vya chini) wa TAWA idadi ambayo haijawahi kutokea tangu taasisi hiyo ianze kupandisha vyeo watumishi wake.
Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika katika ofisi za Makao Makuu ya TAWA mkoani Morogoro, Kamishna Mabula amewapongeza watumishi hao na kuwataka kufanya kazi kwa bidii na kuwa mfano wa kuigwa kwa wengine ili kufikia malengo ya Mamlaka.
Kamishna Mabula amesema Muundo mpya wa Utumishi wa Mamlaka hiyo umetoa fursa Kwa Askari kupanda cheo Kwa kuzingatia vigezo mbalimbali kama vile, nidhamu, mwenendo mwema, utendaji uliotukuka, uzoefu kazini tofauti na muundo wa zamani ambao ulizingatia kigezo cha elimu pekee na hivyo kushusha morali ya watumishi walioshindwa kujiendeleza.
“Nimefarijika sana kuona miongoni wa Askari waliotunukiwa vyeo leo hii, wapo askari 126, ambao wamehudumu kwa muda mrefu bila kupanda cheo, ambao leo wamepanda cheo kutoka Askari wa Uhifadhi daraja la tatu hadi Askari wa Uhifadhi daraja la kwanza,” amesema Kamishna Mabula.
Aidha, Kamishna Mabula ametoa rai kwa watumishi wote wa TAWA kufanya kazi kwa bidii na kuzingatia fursa za kimuundo na vigezo vilivyoanishwa kwenye Amri za Jumla za Jeshi la Uhifadhi vinavyoruhusu kupanda cheo.
Sambamba na hilo, Kamishna Mabula amesema sekta ya Uhifadhi wa Wanyamapori inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ujangili, uvamizi wa maeneo ya hifadhi kwa shughuli za kibinadamu na migogoro baina ya binadamu na wanyamapori, hivyo ametoa maelekezo kwa maafisa na askari wa TAWA kushirikiana na wadau wa uhifadhi ili kuhakikisha changamoto hizo zinaisha katika maeneo yaliyohifadhiwa.
Vilevile amewaagiza watumishi Wote wa TAWA kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha matarajio ya Bodi ya Wakurugenzi ya TAWA iliyozinduliwa hivikKaribuni na Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dk. Pindi Chana yanafafikiwa.