Na RAMADHANI MASENGA
KUKATAA ukweli hakujawahi kuwa tiba ya tatizo. Ukihisi unaumwa kisha ukakataa kupima hakuondoi ukweli wa tatizo ila kutazidi kudhoofisha afya yako zaidi. Hali hii ilikuwa kwenye tasnia ya filamu Tanzania.
Kwa muda mrefu wadau walipaza sauti na kusema tasnia ya filamu ilikuwa imefubaa na inaelekea kufa ila cha kusikitisha wasanii na watayarishaji wa filamu hizi wakawa wanakataa katakata.
Kana kwamba kukanusha kutakuwa tiba ya matatizo, wasanii hao kwa vipindi tofauti wakawa wanatoa maneno ya kejeli kwa wote waliodiriki kudai tasnia ya filamu imepoteza mvuto.
Ila sasa baada ya hali kuwa mbaya zaidi wameamua kuukubali ukweli. Sasa hata ukienda katika makundi yao kwenye mitandao ya jamii wanakiri tasnia imepoteza mvuto.
Japo kwa sasa wanaonekana kukubali ila wanashangaza kwa kutojiona wao ndiyo wahusika wa ufubao huu wa soko la filamu.
Wengi ukiwauliza ni nini kimekwamisha maendeleo ya soko la filamu, watakuambia ‘series’ za Kikorea na filamu za Ulaya zilizotafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili.
Wanakataa kukubali ukweli kuwa ulipuaji wa kazi zao ikiwa pamoja na kujaza watu wenye mionekano mizuri ila uwezo hafifu ndiyo umeua tasnia hii.
Katika hili huwezi kuacha kuwataja watu kama Vicent Kigosi ‘Ray’ na Wema Sepetu. Ray kama mtayarishaji wa filamu na msanii mkubwa kuna kipindi kwa makusudi kabisa alikuwa bingwa wa kuchukua mamisi na watu maarufu na kuwajaza katika filamu huku akiwatosa wasanii wa kweli kwa sababu za kushangaza.
Watu aliokuwa akiwachukua siyo tu walikuwa na uwezo hafifu wa kuigiza ila pia filamu kwao waliichukulia kama sehemu ya kunadi uzuri na kuonesha mikogo.
Kwa namna hii, wasanii wa kweli wakawa hawapati nafasi. Hapo ndipo tukawapoteza wakina Nyamayao, Kibakuli na wengineo.
Hapa ndipo watu kama akina Kipemba kwa unyonge kabisa wakaamua kugeukia fani nyingine baada ya kuona wakipigwa kibuti na watayarishaji kisa hawavai hereni kama akina Hemed Suleiman.
Hili anguko la filamu halisababishwi hata kidogo na uwepo wa filamu za Kikorea. Mbona toka zamani Watanzania walikuwa na utamaduni wa kuangalia filamu za nje ila ulipokuja ujio wa filamu za Kibongo ukapokelewa kwa mikono miwili?
Nani amesahau mtu kama marehemu Lufufu Mkandala ambaye alikuwa fundi wa kupachika maneno ya Kiswahili katika filamu za nje?
Katika zama zile mbona baadaye zilivyokuja movie za Kibongo watu walizilaki kwa nguvu na mahaba? Filamu za nje kutajwa katika ufubao wa soko la filamu za Kibongo ni sababu za kibabaishaji mno.
Akina Wema Sepetu na wengineo waliopewa nafasi ya kuigiza na kushindwa kuendelea kushawishi watu kupenda filamu za Kibongo ndiyo wanafaa kuwekwa msalabani kwa hili.
Wao wanaona fahari kutoka katika magazeti kwa skendo na visa vya ovyo kila siku huku filamu ambazo ndiyo zinatajwa kuwatambulisha wakiwa wamezipa mgongo.
Tuulizane; Wema Sepetu kama msanii maarufu wa filamu, ana filamu gani nzuri ya kumshawishi mtu akaitazame kwa sasa? Hamna kitu!
Filamu zimeuliwa na akina Ray kwa kuwapachika katika filamu watu aina ya Wema Sepetu. Katika hili janga la kifo cha filamu, amini Wema hata haimuumi sana kama inavyomuuma Thea au Riyama.
Thea na Riyama wanaigiza kwa sababu wanapenda filamu, wanahusudu filamu na wana ndoto katika filamu. Wema anaigiza kwa sababu tu aliweke jina lake juu ili akifanya kituko kiwe habari ya mjini.
Ndani ya Wema hakuna msanii makini wa filamu. Kuna msichana mrembo asiyejua nini anakitaka katika mambo anayofanya.
Ni kichekesho baadhi ya wadau wa filamu kutaka serikali ipige marufuku filamu za Kikorea. Watu wanataka kitu kizuri. Kama wasanii wakiacha ulimbukeni wa kubabaikia vitu na kuamua kupambana katika tasnia yao kwa kuwekeza ubunifu na maarifa, sioni kwanini filamu za Kitanzania zikakataliwa na wadau.
Filamu za Kikorea hazifai kuchukiwa na wasanii wa filamu za Kibongo, badala yake ziwaamshe na kuona wanaweza kufanya kitu bora kupitia ushindani wa filamu hizo.