26.9 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

UPE MOYO WAKO THAMANI HALISI INAVYOTAKIWA – 2

KUENDELEA kuumia moyo wako, wakati una uhakika kuwa uliyenaye hana mapenzi ya dhati kwako, haina maana. Ni ujinga wa hali ya juu. Maisha yako yana thamani kubwa kuliko chochote.

Wewe kwanza mengine baadaye. Leo nahitimisha mada yetu. Bila shaka unajifunza mambo mengi ya msingi yanayokufanya uzidi kuwa bora katika uhusiano wako kila siku.

Inawezekana bado kuna mtu anakusumbua, umejaribu kumbembeleza lakini hataki kukubaliana nawe, huyo hakufai. Mapenzi hayapo ili yatutese, badala yake yapo kwa lengo la kutupa faraja.

Muondoe akilini mwako mtu wa aina hiyo, kwani atakufanya uyaone maisha kwa mtazamo hasi jambo ambalo siyo zuri.

 

NINI CHA KUFANYA?

Hili ni swali ambalo kwa hakika linahitaji majibu yakinifu ili kuondoa vilio vya mapenzi vinavyowakumba wengi. Kama nilivyoeleza huko nyuma kuwa mapenzi yana kanuni zake ambazo zinatakiwa kufuatwa ili kuepusha maumivu.

Hapa chini nitakuonyesha mambo ya msingi kuzingatia ili kupishana na maumivu ya mapenzi maishani mwako.

 

UAMINIFU NI MUHIMU

Ukiwa mwaminifu katika ndoa au uhusiano wako, basi itakuwa ni vigumu kwako kuteswa na mapenzi maana utakuwa umefuata moja ya kanuni zake.

Si busara kuwa na wapenzi zaidi ya mmoja ukidhani ni ujanja au ni kwenda na wakati, la hasha. Mapenzi hayaendi hivyo na usipokuwa makini utaishia kulia kila mara.

Utakapobainika kuwa wewe si mwaminifu, watu wengi watakutumia kimapenzi kwa faida zao na mwisho watakuacha ungali bado unawahitaji na hapo ndipo mwanzo wa chungu ya mapenzi huanza, yaani kuachwa na mtu ambaye bado unampenda.

Kwa waliowahi kutokewa na hali hiyo, wanaelewa ninachomaanisha. Acha kurundika wapenzi. Jiheshimu na  mapenzi yatakuheshimu.

 

UONGO

Kudanganya ni sumu kwenye mapenzi, kama wewe ni mzuri wa kupiga porojo katika uhusiano wako, basi mapenzi ni lazima yakutese.

 

Kwa nini uwe muongo katika mapenzi? Jifunze kuwa mkweli na katika hali ya kawaida, huwezi kukwepa uongo kama huna uaminifu.

Leo uko na huyu, kesho uko na yule, maisha hayo hadi lini rafiki yangu? Utaishia kuwadanganya wanawake/wanaume  hadi lini?

Ikiwa wewe ni mwanamke, utawapanga wanaume hadi lini? Unadhani kuchuna mabwana ndiyo maisha yanaishia hapo?

Unapoteza muda wako mwingi katika kuhangaikia mapenzi, badala ya kuwaza mambo muhimu ya maendeleo.

Kama una mpenzi au bado hujampata, basi vuta subira atakuja. Jambo moja muhimu kuamini ni kuwa kila mmoja ana mwenza wake maishani, tatizo linakuja pale tunapoishiwa na uvumilivu na badala yake tunageuka watu wa kudandia na kubadilisha wapenzi kama nguo kila kukicha.

Hayo siyo  maisha jamani. Vuta subira, msubiri wako yuko njiani anakuja, ikiwa umeshampata basi tulia naye huku mkipanga mikakati ya mafanikio kwenye ulimwengu huu uliojaa ushindani.

Si kwamba hawaruhusiwi kupenda la hasha! Nashauri waache kupaparukia mapenzi kwa kutofuata kanuni zake. Yataishia kutuliza kila kukicha.

Mapenzi yapo tangu enzi za mababu zetu, ya nini kuyaendea pupa? Epuka sana kunga’ng’ania mapenzi kwa mtu asiye na chembe hata moja ya mapenzi juu yako.

Kung’ang’ania usipopendwa ni kujiletea mateso ambayo mimi nasema si ya lazima. Ndugu yangu,  wewe ni mzuri mno, mapenzi yasikuumize kabisa. Usiumie kwa kumkosa wako wa maisha, inawezekana hajajitokeza tu.

Tuliza akili, hakikisha mapenzi hayakuongozi, bali wewe ndiye unakuwa kiongozi wake. Inawezekana kabisa. Tutakutana tena wiki ijayo katika mada nyingine, USIKOSE!

Kama unapenda kupata mafunzo haya zaidi kupitia kundi letu la WhatsApp, tafadhali wasiliana nasi inbox kupitia namba 0712 170745.

Pia jiandae kupata kitabu changu kipya cha SIRI ZA NDOA YENYE FURAHA kitakachotoka hivi karibuni.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles