25.9 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

TATIZO MIMBA KWA WANAFUNZI MFUPA MGUMU

Na Hamisa Maganga,

ELIMU ndiyo msingi wa maisha ya watoto wetu. Urithi mzuri kwa mtoto ni elimu na si fedha, majumba au magari ya kifahari. Hivyo, katika vitu ambavyo tunapaswa kuvipa kipaumbele na kuvikazania kwa watoto ni kuhusu elimu kwani ndiyo itakayoonesha mwelekeo wa maisha yake ya hapo baadaye.

Tumeshuhudia watoto wa kike wakikatisha masomo yao kwa sababu kadhaa ikiwamo kupata ujauzito wakiwa shuleni.

Wanafunzi katika sehemu mbalimbali nchini hukatisha masomo yao kwa sababu ya mimba.

Kwa mujibu wa takwimu za tatizo la mimba Mkoa wa Ruvuma zinaonesha kuwa takribani watoto wa kike 155 walishindwa kumaliza elimu yao ya msingi na sekondari katika kipindi cha mwaka 2013 kwa sababu ya kupata mimba.

Takwimu hizo zinaonesha kuwa mwaka 2013, watoto 16 wa shule za msingi na 78 wa sekondari walikatisha masomo kwa sababu ya kupata mimba.

Mwaka 2014 wasichana watano wa shule za msingi na 56 wa sekondari waliacha shule kwa sababu ya ujauzito.

Mwaka 2009 wasichana 300 mkoani Tanga waliacha shule, Kagera 880 na Pwani wasichana 500 walikatisha masomo kwa sababu ya mimba.

Kama hiyo haitoshi, ripoti ya utafiti uliofanywa mwaka jana na Shirika la Kimataifa la Human Right Watch, iliyopewa jina la ‘Nilikuwa na ndoto za kumaliza shule’ inaonesha kuwa asilimia 40 ya wanafunzi nchini hukatisha masomo yao sekondari kutokana na ujauzito.

Utafiti huo ulibaini kuwa wasichana zaidi ya 8,000 waliacha masomo baada ya kupata mimba au kuolewa kwa nguvu.

Pia uligundua kuwa maofisa wa shule hufanya vipimo vya lazima vya ujauzito mara kwa mara, jambo wanaloamini kuwa ni udhalilishaji.

SHERIA YA ELIMU

Sheria ya Elimu ya mwaka 1978 inamnyima haki msichana anayepata mimba shuleni. Kifungu cha 35 na kanuni zake na marekebisho yaliyofanyika mwaka 1995 na 2002 kinasema mtoto wa kike akipata mimba akiwa shuleni ni ushahidi tosha kuwa amefanya ngono kinyume na sheria hivyo adhabu yake ni kufukuzwa shule.

BUNGE LAJADILI

Katika mkutano wa saba wa Bunge la 11, wabunge pamoja na kujadili na kupitisha bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka wa fedha 2017/18 iliyowasilishwa na Waziri wa wizara hiyo, Profesa Joyce Ndalichako,

baadhi ya wabunge walitaka Serikali iruhusu wanafunzi wanaopata ujauzito wakiwa shuleni waendelee na masomo baada ya kujifungua.

Wabunge hao wanasema kitendo cha kuwanyima fursa ya kusoma wanafunzi waliopata mimba shuleni, kinawanyima haki ya kupata elimu.

Lakini pia wapo waliopinga vikali wanafunzi hao kuendelea shule wakidai kuwa suala hilo linakwenda kinyume na maadili ya Mtanzania.

WANAOPINGA

Mbunge wa Makete, Profesa Norman Sigalla (CCM), anasema haungi mkono wanafunzi kuendelea na masomo kwa sababu kuna njia nyingine za kuwasaidia baada ya kuachishwa.

Anasema mtoto wake akipata mimba si kwamba haruhusiwi kuendelea na masomo bali anachotakiwa kufanya ni kumpeleka katika shule nyingine baada ya kujifungua.

“Yaani, ukimwambia mtoto kwamba mwanangu ukipata mimba utaendelea na shule, basi tujue mimba zitakuwa nyingi mno shuleni,” anaonya Profesa Sigalla.

Naye Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Keissy (CCM), anasema akina mama wengi waliopo bungeni huwa wanaongoza mapambano ya kupinga wasichana wasiolewe chini ya miaka 18 lakini anawashangaa kuwaona wakiunga mkono suala hilo.

Anasema wasichana wengi huvunja ungo (kukua) wakiwa na miaka 10 – 12 kwa hiyo wanaweza kupata mimba.

Anasema watoto hawa bado ni wanafunzi hivyo wakianza kuchanganya mapenzi na shule ni lazima elimu yao itashuka.

“Sasa, nataka akina mama humu ndani (bungeni) ambao walikuwa wanafunzi na wako hapa, wanithibitishie kwamba walianza mapenzi mapema wakiwa shuleni na elimu yao ilikuwaje, kama ilikuwa pale pale nitawaunga mkono, watueleze.

“Na mimi kwa kuwa ni Muislamu, dini yangu inaniambia nisikaribie zinaa, sasa kama Muislamu anasimama hapa anaunga mkono mtoto wa shule aanze zinaa huyo si Muislamu, amekiuka maadili yake ya dini moja kwa moja,” anasema Keissy.

Anasisitiza kuwa wabunge wasichangie kuongeza watoto wa mitaani ambao watakuwa hawana malezi wala wazazi. “Tusicheze na kuongeza watoto mitaani, kwanza kuna Ukimwi. Hatuwezi kukubali, tukiruhusu hapa basi mjue watafungulia… wataanza kuishi na watoto wetu.

Kwa upande wake Mbunge wa Kuteuliwa (CCM), Salma Kikwete anapinga vikali wanafunzi wanaopata mimba wakiwa shuleni kuruhusiwa kuendelea na masomo.

Anasema suala la mimba na utoro ni tatizo shuleni hivyo hakubaliani na hoja ya kwamba watoto wakipata mimba warudi kuendelea na masomo.

“Kwanza mkumbuke kuwa hapa tunazungumzia suala la mila, desturi, utamaduni, mazingira na dini. Hakuna dini yoyote inayomruhusu mtoto wa kike kupata mimba kabla ya wakati.

“Biblia inasema na Quran pia inasema, hivyo tunapofanya mambo yetu ya msingi tuangalie na masuala yanayohusu imani yetu ya dini, tutafute njia mbadala ya kumsaidia mtoto anayepata mimba shuleni lakini si kurudi kuendelea na masomo,” anasema Salma na kuongeza:

“Sisi wabunge tuna kanuni zetu tunazozifuata hali kadhalika kwenye suala la mimba lazima sheria inayofuata hapa iwe mtoto akipata mimba asirudi shuleni.”

Anasema ni lazima sheria imbane mtoto ili akipata mimba asirudi shuleni bali atengenezewe mazingira wezeshi kwa kuwa akirudi kuendelea na masomo wengi watapata mimba katika umri mdogo.

Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba (CCM), anasema tatizo lililopo ni kwamba watu wakipata njaa hawahangaiki kujiuliza kwanini wanapata njaa badala yake wanataka wapewe chakula.

Anasema hali kadhalika watoto wakifeli kwa kiwango kikubwa watu hawahangaiki kujiuliza kwanini wanafeli bali wanabadilisha daraja ili wafaulu.

“Vivyo hivyo katika suala hili la watoto kupata mimba badala ya kuhangaika kujua kwanini wanapata mimba na kutafuta mbinu za kuzuia suala hili lisitokee, wanahangaika kutaka kuhalalisha wapate mimba,” anasema Mwigulu.

Anasema: “Hatuwezi tukaipa dhambi jina zuri na baadaye tukaitukuza, dhambi ni dhambi na itabakia kuwa dhambi, atakayeruhusu masuala ya kupata mimba ajue anakiuka maadili ya mila, imani na sheria za nchi.”

Naye Mbunge wa Jimbo la Rufiji (CCM), Mohamed Mchengerwa anasema suala hili si la udini lakini ni muhimu Watanzania wakalea watoto wao kwa misingi ya elimu ya dunia na akhera.  “Nasisitiza kwamba kuliweka jambo hili hapa ni kutaka watoto wetu washiriki katika mambo hayo mapema,” anasema.

WANAOUNGA MKONO

Mbunge wa Jimbo la Temeke (CUF), Abdallah Mtolea anasema ni jambo la aibu kwa wabunge kupinga kumpa fursa mtoto wa kike ambaye pengine alifanya makosa kupata mimba, au alipata kwa bahati mbaya.

Mbunge wa Jimbo la Buyungu (Chadema), Mwalimu Kasuku Bilago anasema wanaopinga watoto wanaobeba mimba wasirudi shuleni, ndio hao hao wanaosema wanataka usawa wa asilimia 50 kwa 50.

“Unapata wapi 50 kwa 50 wakati kuna watu walibeba mimba na hawakuruhusiwa kuendelea kusoma?” anahoji.

Mbunge wa Viti Maalumu, Susan Lyimo (Chadema), anamshangaa Salma Kikwete kwa mtazamo wake licha ya kwamba naye ni mwanamke.

“Nimesikitishwa na mheshimiwa Salma Kikwete ambaye ni mwanamke mwezetu. Lakini, simshangai kwa sababu hata mumewe alipokuwa rais, aliwahi kusema kuwa watoto wanaopata mimba ni kutokana na viherehere vyao,” anasema Lyimo.

Huku Mbunge wa Viti Maalum, Tauhida Nyimbo (CCM), anasema watoto walio katika familia zenye uwezo hupata fursa ya kuendelea na masomo baada ya kujifungua wakati wanaotoka familia masikini hulazimika kubaki nyumbani.

“Atakayempa mimba mwanafunzi awekwe ndani na mwanafunzi wa kike apewe elimu ya kuepuka mimba, pia ziwepo taratibu kali za kuwalinda watoto wa kike.

“Mtoto wa mwenye fedha akipata mimba, ujue itatolewa ili aendelee na masomo, kwa hiyo watoto waruhusiwe kusoma baada ya kujifungua,” anasema Tauhida.

Mbunge wa Viti Maalum, Lucia Mlowe (Chadema), anasema kutowaruhusu watoto wa kike wasiendelee na masomo kwa sababu ya mimba ni kutowatendea haki kwa sababu baadhi yao hubeba mimba baada ya kudanganywa.

SHERIA INABANA

Mbunge wa Mbinga Mjini, Sixtus Mapunda (CCM), anasema ili watoto waruhusiwe kuendelea na masomo baada ya kujifungua, kuna haja ya kubadili sheria ya ndoa ya mwaka 1971 kwa sababu inawazuia wasifanye mapenzi wakiwa na umri mdogo.

Hivyo, anataka tahadhari zaidi zichukuliwe kabla ya kufikia uamuzi wowote, huku mila, desturi na imani za kidini zikizingatiwa kwa kuwa dini zinazuia mapenzi katika umri mdogo.

WANAFUNZI WATENGWE

Kesi nyingi zinazohusu wanafunzi kupewa ujauzito zinahusisha wanafunzi wenyewe kwa wenyewe. Watoto wengi wa kike wanapewa mimba na wanafunzi wenzao wa miaka 14 hadi 16.

Sasa basi, baadhi ya wazazi wanashauri Serikali kutenga shule za wanafunzi wa kike na kiume.

“Wanafunzi wa kike wengi huanzisha uhusiano wa kimapenzi na wanafunzi wenzao wa kiume, kwa hiyo njia moja wapo ya kuepuka jambo hili ni kuwatenganisha,” anasema Doris Peter, mama anayesomesha watoto wake shule ya Msingi Yombo.

UMASIKINI UNACHANGIA

Licha ya tamaa za kimwili zinazowakabili watoto, asilimia kubwa hujikuta wakijihusisha na uhusiano wa kimapenzi hatimaye kupata mimba kutokana na umasikini unaowakabili.

Watoto wengi ambao hawana wazazi, hasa wale wa vijijini huwa hawafanikiwi kuhitimu masomo yao.

Sheila Yusuph (18) si jina halisi) anasimulia jinsi alivyobeba ujauzito bila kutarajia.

“Nilipata mimba nikiwa na miaka 15. Wazazi wangu walifariki nikiwa na miaka saba, hivyo nimelelewa na bibi upande wa mama ambaye naye maisha yake si mazuri.

“Baada ya kuona hali ya kifedha inazidi kuwa mbaya nyumbani, nikajikuta naanzisha uhusiano na kijana wa bodaboda nikidhani atatusaidia.

“Lakini wakati mimba ikiwa na miezi miwili mwanamume alifariki nikakosa pa kuegemea kwani shule nilishaacha na sasa natangatanga tu mtaani na mwanangu,” anasema Sheila.

Naye Nora Andrew (19), anasema alishika mimba akiwa na miaka 13 baada ya kuona maisha ya nyumbani ni magumu.

“Naishi na mama yangu ambaye anauza pombe za kienyeji. Hakuwahi kunikataza kujihusisha na uhusiano wa kimapenzi kwa kuwa nilikuwa napeleka hela nyumbani.

“Niliacha shule nikiwa darasa la tatu mara baada ya kuvunja ungo, nikawa na uhusiano na kijana mmoja mkulima, alikuwa akinihudumia kila ninachohitaji ambacho nyumbani nilikuwa sipati.

“Wakati mwingine ananipa fedha nimpelekee mama, mwishowe nikapata ujauzito naye akanitelekeza,” anasema Nora.

ELIMU KWA VIJANA

Kuna umuhimu mkubwa wa vijana kupewa mafunzo kuhusu ngono. Kuzungumza nao bila usiri ili kuepuka mimba zisizotarajiwa.

Ofisa Ustawi wa Jamii Manispaa ya Temeke, Doris Maagi anasema kuna umuhimu mkubwa wa kuzungumza na watoto kuhusu masuala ya ukuaji.

“Usiri ndiyo chanzo cha watoto kuangamia, wengi hawajui matokeo ya kushiriki ngono wakiwa na umri mdogo. Tukisema mtoto akipata mimba arudi shule tutachangia wanafunzi wengi kujiingiza katika masuala ya kimapenzi kabla ya umri,” anasema na kuongeza kuwa jambo la muhimu ni kuwaelimisha wasitumbukie katika mapenzi kabla ya umri.

Anasema mashirika ya kiraia, sekta binafsi, vyombo vya habari, familia na watoto wenyewe, wote wanapaswa kusaidia kupunguza mimba za utotoni.

MSIMAMO WA SERIKALI

Serikali imejipanga kutengeneza mwongozo wa kuwarudisha shuleni wanafunzi waliopata mimba wakiwa masomoni ili kuhakikisha wanapata elimu hadi kufikia ngazi za juu.

Nia hiyo ilitolewa na Mkurugenzi Msaidizi Masuala Mtambuka kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Venance Manori alipokuwa akifungua warsha ya kuwawezesha maafisa waandamizi wa Serikali kutoka nchi sita za Afrika katika kutengeneza mipango inayozingatia jinsia katika elimu.

Anasema Serikali inajitahidi kuzingatia jinsia katika utoaji wa elimu ambapo takwimu zinaonyesha kuwa elimu ya msingi na sekondari uwiano wake ni moja kwa moja japo kuwa idadi ya wasichana hupungua kutokana na changamoto zinazowakumba ikiwamo kupata ujauzito na ndoa za utotoni.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Plan International- Tanzania, Jorgen Haldorsen ameahidi kushirikiana na Serikali kuhakikisha mipango ya elimu nchini inaangalia usawa wa kijinsia kwa kuwa ni njia moja wapo itakayochochea maendeleo ya elimu kwa watoto wa kike.

WALICHOAMUA AFRIKA KUSINI

Nchini Afrika Kusini, kuna shule maalumu ambayo wanafunzi wote ni wasichana wenye ujauzito.

Lengo la kuanzishwa kwa shule hiyo maalumu ni kuwasaidia wasichana hao wasisimamishwe masomo yao na kutengwa na jamii.

Ingawa Serikali ya Afrika Kusini imetoa amri kwamba shule yoyote isiwafukuze wanafunzi waliopata mimba shuleni, bado kuna wanaofukuzwa na wengine  kuacha masomo kutokana na shinikizo kutoka kwenye jamii.

Shule ya wanafunzi wajawazito nchini humo ipo Mjini Pretoria, wanafunzi wengi waliopo hapo ni wale wenye miaka kuanzia 13 hadi 20.

Nchi hiyo kupitia Idara ya Elimu ya msingi imeweka mikakati ya kuhakikisha inashughulikia sera ya kupunguza ujauzito kwa wanafunzi, licha ya kwamba bado haijazaa matunda.

Miongoni mwa mambo muhimu yanayotakiwa kutekelezwa kwenye mikakati hiyo ni kutoa huduma za uzazi wa mpango, kuwapa motisha ya kumaliza shule kabla ya kupata ujauzito na programu za elimu ya umma ambayo inakataza ngono isiyo salama.

HALI ILIVYO NAMIBIA

Nchini Namibia pia wanakabiliwa na tatizo hili. Kuna shule moja ya mchanganyiko iitwayo Ontoko ambayo ipo katika Mkoa wa Omusuti, ina rikodi ya kesi tisa za wanafunzi wanaoacha shule kutokana na ujauzito. Shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 800, kesi nyingi zilizoripotiwa za wanafunzi waliopata ujauzito ni wale wa madarasa ya chini.

Shule hiyo ilifikia hatua ya kuwaamuru wanafunzi wote wa kike kunyoa nywele wakidhani huenda mitindo ya nywele ndiyo inayowafanya wajali zaidi mambo ya urembo ili kuwavutia wanafunzi wa kiume.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

  1. Uchambuzi wa suala hili umeandikwa uzuri bila kupendelea upande wowote na huu ndio weledi. Mwandishi hajatoa hitimisho lake lakini ameweza kusaidia kwa kuonyesha mifano ya nchi ya Afrika Kusini na Namibia jinsi wanavyojaribu kupambana na suala hili na pia ameweza kupata maoni ya wananchi wa kawaida kuonyesha mawazo yanayojiri mtaani na hatimaye maamuzi ya serikali.

    Kwa faida tu ya Watanzania ni kuwa Serikali kupitia Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) inatoa elimu ya sekondari kwa hawa watoto waliopoteza fursa ya elimu katika mfumo rasmi. Elimu hii hutolewa kwa njia ya ujifunzaji huria na masafa yaani Open and Distance Learning na walengwa hujisajili katika vituo vya TEWW vilivyoko kila mkoa Tanzania bara. Kupitia mfumo huu mtanzania yeyote, awe ameolewa ama la, na awe kijana au mzee anaweza kujisomea kwa wakati wake mwenyewe na kwa gharama nafuu bila kuathiri shughuli zake za kila siku za maendeleo kwani halazimiki kuingia darasani kila siku kutwa nzima kama ilivyo kwa wanafunzi wa shule za serikali katika mfumo rasmi.

    Hii ni fursa ya pekee kwa wasichana walioathirika na mimba au ndoa za utotoni. Taarifa zaidi zipo katika tovuti ya TEWW http://www.iae.ac.tz

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles