Na ELIZABETH KILINDI -NJOMBE
ZAIDI ya asilimia 70 ya Watanzania waishio vijijini wamenufaika na mpango wa kunusuru kaya masikini zinazotolewa na Mfuko wa Maendeo ya Jamii (Tasaf).
Mkurugenzi wa Ukaguzi wa ndani wa Tasaf, Christopher Sanga, aliwaambia waandishi wa habari juzi kuwa mkakati wa sasa ni kufikia Watanzania kwa asilimia 100.
Alisema miradi inayotolewa na Tasaf imelenga watu maalumu ambao ni masikini ili kuwasaidia kuwa na maisha bora kwenda sambamba na kuwaongezea kipato kuanzia ngazi za kaya.
Alisema mpango huo wa kaya masikini hauchagui watu wa kuingia bali wanategemea kupata taarifa sahihi kutoka kwenye uongozi wa kijiji au kata kwa utambuzi wa kaya masikini.
“Taarifa za wanufaika na miradi yetu inatokana jamii yenyewe kuleta taarifa kupitia uongozi wa kijiji au kata na ndio maana awali tulifanya ukaguzi na baadhi ya changamoto zilifanyiwa marekebisho,” alisema Sanga.
Sikujua Utumu alisema changamoto kubwa katika kijiji chao ni ukosefu wa zahanati kwa sababu wanatembea kilomita zaidi ya 12 kufuata huduma za afya.
“Tunaomba mradi ujao wa kunusuru kaya masikini uzingatie suala zima la afya kwani hapa kijijini kwetu hakuna zahanati, hivyo tunalazimika kutembea umbali wa kilomita 12 kufuata matibabu,” alisema Sikujua mkazi wa Kijiji cha Ilengititu, Kata ya Kichiwa, Njombe.
Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe, Ally Kasinge ambaye alimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Ruth Msafili, aliwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa maofisa wa Tasaf kutekeleza miradi katika jamii yao.