Renatha Kipaka, Kagera
Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii wakunusuru kaya maskini (TASAF) imelipa zaidi ya Sh Bilioni 5 kwa kaya masikini mkoani Kagera kwa lengo la kusaidia elimu na afya hususan kwa watoto.
Hayo yamebainishwa Juzi na Mratibu wa TASAF awamu ya tatu mkoani Kagera, Efurazi Mkama, wakati akizungumza na Waandishi wa Habari
Amesema mpango huo unawasaidia watoto chini ya miaka mitano wapatao 16,886 kupata huduma ya afya (Kliniki) huku wengine 47,860 wakiandikishwa kuanza darasa la kwanza.
“Lengo la TASAF nikushirikiana na serikali kupunguza vifo vya watoto chini ya umri wa miaka mitano na kuboresha Afya zao,” amesema Mkama.
Amesema kuwa mpango huo unazihudumia kaya na watoto ambao wakimaliza huduma za kliniki wanawezeshwa kujiunga na darasa la kwanza .
Pia mkoa wa Kagera unawatoto wanaotimiza masharti ya kujiunga na darasa la kwanza ambapo TASAF imewazesha kupata daftari, sare za shule, viatu, kalamu na kuwafanya watoto hao kuwa na morali wa kusoma kwa bidii na kupunguza watoto wa mitaani.
“TASAF inasaidia watoto kuwa msaada wa baadae kwa familia zao kiuchumi nakupunguza tatizo la ajira,” amesema.
Mratibu huyo amefanunua kuwa kwa kipindi cha Julai hadi Agosti 2021 zililipwa Sh bilioni 2.1 kwa kaya 55,776 katika vijiji 494.
Kwa kipindi cha Septemba hadi Oktoba 2021 zililipwa Sh 3.1 kwa kaya 81,306 katika vijiji 727.