Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema Tanzania imeorodheshwa nafasi ya sita duniani na ya kwanza Afrika kwa ongezeko la idadi ya watalii, kulingana na takwimu za Shirika la Utalii Duniani.
Akizungumza Oktoba 11, 2024 jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa Onesho la 8 la Utalii la Kimataifa la Swahili (Swahili International Tourism Expo – S!TE 2024), Dk. Mwinyi alieleza kuwa onesho hilo, linalofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City, limewaleta pamoja wanunuzi wa bidhaa za utalii, waoneshaji, wawekezaji na wadau wengine wa sekta hiyo kutoka ndani na nje ya Tanzania.
Dk. Mwinyi aliipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa juhudi zake ambazo zimeongeza mapato ya sekta ya utalii, akieleza kuwa serikali inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan imewezesha idadi ya watalii wa kimataifa kufikia 2,026,378 hadi Agosti 2024 – kiwango cha juu zaidi katika historia ya Tanzania. Mapato yatokanayo na sekta hiyo pia yamefikia Dola za Marekani bilioni 3.5.
“Juhudi za Rais Dk. Samia zimewezesha idadi ya watalii wa kimataifa wanaotembelea nchi yetu kukua kwa kasi, sambamba na ongezeko la mapato. Sekta ya utalii imekuwa nguzo muhimu katika kukuza uchumi wa Tanzania, ikichangia asilimia 17.2 ya Pato Ghafi la Taifa na kuzalisha ajira zaidi ya milioni 1.5,” alisema Dk. Mwinyi.
Aidha, Dk. Mwinyi alibainisha kuwa Tanzania imepokea tuzo mbalimbali za kimataifa kutokana na umaarufu wake katika sekta ya utalii. Kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Utalii Duniani iliyotolewa Septemba 2024, Tanzania inashika nafasi ya kwanza barani Afrika kwa ongezeko kubwa la watalii. Miongoni mwa tuzo hizo ni za World Travel Awards ambapo Bodi ya Utalii Tanzania ilitambuliwa kama Africa’s Leading Tourist Board, na Ngorongoro kama Africa’s Leading Tourist Attraction.
Kwa upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dk. Pindi Chana, alisema sekta ya utalii imekuwa na mchango mkubwa katika pato la taifa kwa kuchangia asilimia 17.2 na kwamba inatarajiwa kuendelea kuimarika.
Maonesho ya S!TE 2024 yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika sekta ya utalii, huku Tanzania ikithibitisha hadhi yake kama kivutio bora barani Afrika.