*Ukuta wa Mererani waongeza mapato maradufu
*Makinikia yadhibitiwa, biashara ikiimarika
Na Ramadhan Hassan,Dodoma
WAZIRI wa Madini, Doto Biteko amesema ndani ya miaka 60 ya Uhuru sekta ya madini imepata mafanikio makubwa ikiwemo kuimarisha biashara ya madini pamoja na kuzuia utoroshaji wa madini nje ya nchi ambapo amedai ni muhimu kuwa na wasiwasi kwamba kumekuwa na wizi katika sekta hiyo.
Amesema kutorosha madini ni ‘zilipendwa’ nakwamba hakuna faida wala tija na anaetorosha anatafuta jela ama umaskini nakuongeza kuwa wachimbaji hawahangaiki na kwenda jela.
Akizungumza leo Ijumaa Novemba 5, 2021 na Waandishi wa Habari jijini Dodoma, wakati akieleza mafanikio na maendeleo ya sekta ya madini kabla na baada ya uhuru, Waziri Biteko amesema sekta ya madini ina historia ndefu kuanzia kipindi cha kabla ya uhuru hadi kufikia kipindi cha maadhimisho ya miaka 60.
Waziri Biteko amesema mafanikio ambayo yamepatikana ni pamoja na kuzuia utoroshwaji wa madini nje ambapo amedai kwa sasa wamejitahidi kuweka masoko kila eneo nchini.
Amesema kuwa na wasiwasi na mashaka katika utoroshaji wa madini ni jambo muhimu hasa kwa mtu mwenye akili timamu huku akitolea mfano wa ndoa ambapo amesema wasiwasi nimuhimu.
“Ni muhimu tuwe na wasiwasi siku tukiridhika kwamba mambo yapo swari ujue siku hiyo ndio tumeanza kuibiwa kuwa na wasiwasi na mashaka kwa mtu mwenye akili timamu ni bora lakini twende kwenye namba.
“Turudi nyuma tulipotoka ni kesi za watu wangapi walikuwa wakikamatwa wakitorosha madini? wachimbaji na wafanyabiashara ukikuatana nao watakwambia kutorosha kuna hasara, zamani walikuwa wanatorosha kwa sababu hapa ndani hapakuwa na utaratibu mzuri.
“Tuendelee kuwa na wasiwasi kwa sababu wasiwasi ni sehemu ya maisha muhimu, mtu akisema atatorosha tujue uchochoro.
“Wito wangu kwa Watanzania, kutorosha madini ni zilipendwa hakuna faida hakuna tija mtu yeyote kwa anaefanya hivyo, kwani atakuwa anatafuta vitu viwili tu kati ya jela au umaskini kwenye maisha yake,” amesema Biteko.
Changamoto zilizopo
Aidha, Waziri Biteko amezitaja baadhi ya changamoto ambazo Wizara imekutana nazo katika kipindi cha miaka 60 ni pamoja na matokeo ya maendeleo ambapo kwa sasa rasilimali fedha, vitu na watu zinahitajika.
“Changamoto kubwa kwetu ni matokeo ya maendeleo kama ambavyo kwenye maisha ya kawaida tu ukifanikiwa jambo moja utazalisha jambo lingine, kwa mfano sekta inapokuwa inavutia watu wengi kuingia ndio mwanzo wa kuiongezeka kwa fursa kama raslimali fedha, watu na vitu kwa ujumla,” amesema Biteko.
Hata hivyo, Waziri huyo amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kibali cha kuajiri watumishi wapya ambapo amedai itapunguza changamoto ya uhaba wa watumishi.
Ameitaja changamoto nyingine kuwa ni utengenezaji wa sheria zinazofanana ambapo amesema ni lazima Waafrika wawe na sheria zinazofanana ili kuendelea kulinda rasilimali madini katika maeneo yao.
“Mfumo wa usimamizi wa madini sisi Tanzania hatupo peke yetu tuna majirani zetu ambao wana madini kama sisi, hivyo ni lazima sasa changamoto ninayoiona ni ya kiafrika zaidi, ni lazima waafrika tusimame tuwe tunasheria zinazofanana,”amesema.
Vilevile, amesema changamoto nyingine ni mtazamo wa wachimbaji wadogo kuvamia waeneo ya wawekezaji ambapo amedai serikali itaendelea kuwalinda wawekezaji wenye leseni.
“Mwekezaji lazima alindwe ni muhimu Watanzania tuwalinde wawekezaji wetu haina maana tunampa mtu leseni halafu anaingiliwa katika biashara zake.
WATANZANIA WAPO TAYARI KUCHIMBA MADINI
Katika hatua nyingine, Biteko amesema kwa sasa Watanzania wapo tayari kuchimba madini kwani kuna watalamu wengi wa kutosha tofauti na miaka ya nyuma ambayo Hayati Mwalimu Julius Nyerere alidai mpaka watanzania wawe tayari ndio madini yachimbwe.
“Tumejaribu kuonesha hata tofauti ya wakati wa wakoloni na sisi, tumepiga hatua kubwa sana na utayari wetu ni kuwa na wataalamu wa kusimamia madini. Nchi hii inazalisha Wajiolojia, Wahandisi wengi sana migodi yetu unayoiona hata wachimbaji wadogo asilimia zaidi ya 80 wana Wajiolojia wao.
“Kwa hiyo kile ambacho baba wa Taifa alisema tukiwa tayari tuchimbe madini yetu mimi naamini wakati ndio huu, tupo tayari kwa sababu tuna watalaamu,”amesema Biteko.
UWAZI WA MIKATABA
Aidha, amesema mikataba yote inayoingia Wizara yake haijifungii bali inaifanya kwa uwazi na inasaini hadharani mbele ya Waandishi wa Habari.
“Mikataba yote tunaingia Waziri hajifungii ndani akaingia mikataba na mwekezaji tunasaini hadharani na ninyi mnakuwepo(waandishi) na mikataba inawekwa hadharani.
“Isipokuwa lazima kwenye mikataba wawekezaji wanamikataba yao ambayo hawataki ijulikane kama nchi zipo taratibu za kufuatwa,”amesema. Biteko.
MASOKO YA MADINI YALETA FAIDA
Kwa upande wa masoko ya madini, Biteko amesema ndani ya miaka 60 kumekuwa na masoko mengi ya madini ambapo amedai yamesaidia kuongeza mapato na kwa sasa kuna masoko 102 ambapo makubwa ni 50 na madogo 52.
“Dar es Salaam tulikuwa na watu wana viwanda bandia ‘fek’i lakini vitafute kwa sasa kama vipo kwa sababu tumebadilika na hela unaipata hapo hapo na siku hiyo hiyo na mabenki yapo na tunawauliza mnataka mpewe fedha mkononi au kwa njia ya benki.
“Wachimbaji wadogo wananufaika sana nenda katika Mahakama ilikuwa ni kudhulumiana lakini kwa sasa hakuna kwenye masoko watu wenye hela ndio wananunua,” amesema Biteko.
AFUNGUKA MAKINIKIA
Kuhusu makinikia amewahakikishia Watanzania kwamba wana toza kila aina ya madini tofauti na zamani ambapo walikuwa wakitoza katika madini ya dhahabu na almasi.
“Niwahakikishie sasa hivi kwenye makinikia haya mnayoona yanayozalishwa tunatoza kila aina ya madini yaliyopo, huku tulikotoka tulikuwa tunatoza dhahabu na almasi lakini sasa hivi tunachaji mpaka Iron iliyopo ni kiasi gani na inauzito kiasi gani,”amesema.
Amesema mara baada ya kukubaliana kutosafirisha makinikia nje ya nchi kwa sasa wanayachukua na kuyapeleka katika maabara zao tatu ambapo zinapimwa na kuonesha kuna madini kiasi gani.
“Kwa hiyo tulikubalina tubadilishe utaratibu mwaka 2020 tulisaini mkataba na ule utaratibu wa kusafirisha makinikia tunaachana nao na yauzwe kama madini,” amesema.
Amesema kutoka mwaka 2020 walivyosaini mkataba mpaka kufika Machi, mwaka huu kulikuwa kuna makontena 1,600 ambayo tayari yalikuwa yameuzwa.
“Na mchango wa makinikia yenyewe katika mapato yake yote kwenye zile fedha bilioni 584 asilimia 2.5 inatokana na mauzo ya makinikia,”amesema.
MIGODI
Amesema ikilinganishwa na nchi ilipotoka ba hivi sasa Taifa lina migodi 9 ambapo 6 ni ya dhahabu, mmoja almasi, Tanzanite mmoja na mmoja wa Makaa ya mawe nakuongeza kuwa ipo migodi takribani ya 28 ya uchimbaji wa kati na mingine mingi ya uchimbaji mdogo.
UKUTA WAONGEZA MAPATO YA TANZANITE
Waziri huyo amesema kwa upande wa madini ya Tanzanite yameongeza mapato ya serikali kutoka Sh milioni 166 kwa mwaka kabla ya kuwepo kwa ukuta hadi kufikia Sh bilioni 3.9 baada ya ujenzi wa ukuta.
“Yapo mambo mengi ambayo tumefanikiwa ikiwemo kupandisha uchumi wetu kuongeza ufanisi wa sekta kuongeza uwazi na ushiriki wa Watanzania,”amesema.