28.2 C
Dar es Salaam
Sunday, December 1, 2024

Contact us: [email protected]

Tanzania yahimiza Mataifa makubwa kuendelea kuzifutia madeni nchi za OACPS

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Tanzania imeendelea kuhimiza umuhimu wa mataifa makubwa kuzifutia madeni nchi za Jumuiya ya nchi za Afrika, Caribbean na Pasifiki (OACPS) zilizoathiri na janga la COVID-19 pamoja na kuyataka mataifa hayo kuhakikisha kwamba chanjo ya COVID-19 itakayopatikana inazifikia nchi zote za Jumuiya hiyo.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi ambaye pia ni Rais wa Baraza la Mawaziri la OACPS wakati alipokuwa anawasilisha hotuba yake katika Mkutano wa 39 wa Bunge la pamoja baina ya nchi za ACP na EU na Mkutano wa 111 wa Baraza la Mawaziri kutoka nchi za Jumuiya ya OACPS uliofanyika jana kwa njia ya Mtandao (Video Conference) jijini Dar es Salaam.

“Kutokana na jukumu langu kama Rais wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya OACPS nimehutubia kwa njia ya video Bunge la pamoja la Ulaya na ACP (ACP-EU Joint Parliamentary Assembly). Katika hotuba yangu nimehimiza umuhimu wa mataifa makubwa kuendelea kuzifutia madeni nchi za OACPS zilizoathiri na janga la COVID-19, pamoja na kuyataka mataifa hayo kuhakikisha kwamba chanjo ya COVID-19 itakayopatikana inazifikia nchi zote za Jumuiya yetu ya OACPS,” amesema Prof. Kabudi

Halikadhalika, Prof. Kabudi ameelezea hatua iliyofikiwa na nchi za OACPS ikiwemo Tanzania katika kujenga democrasia, uchumi, biashara na maendeleo ya watu ikiwemo suala la kulinda na kuheshimu haki za binadamu. Aidha, aliwajulisha juu ya  changamoto zinazozikabili nchi za OACPS katika kutimiza adhma yao ya maendeleo, ikiwemo janga la ugonjwa wa COVID -19, mabadiliko ya tabia nchi, ugumu wa kuyafikia masoko ya ulaya, masuala ya amani na usalama ikiwemo suala la wakimbizi.  

Kwa upande wake Waziri wa Uchumi na Maendeleo wa Ujerumani, Dk. Gerd Muller, ambaye pia ni Raisi wa Baraza la  Mawaziri la Umoja wa Ulaya alimhakikishia Prof. Kabudi kuwa Umoja wa Ulaya (EU) utaendeleza ushirikiano wake na nchi za OACPS katika kuhakikisha kuwa uchumi wa Jumuiya hiyo unazidi kuimarika.

“Naomba kutumia fursa hii kukuhakikishia kuwa sisi ka EU tupo tayari kushikamana na Jumuiya ya OACPS kuimarisha uhusiano wetu kiuchumi, kisiasa, kidiplomasia lakini pia kulinda na kuapa kipaumbele masuala yote yanayohusu haki za binadamu,” amesema Dk. Muller.

Mbali na Dkt. Muller wengine waliohutubia katika mkutano huo ni pamoja na Jutta Urpilanen, Kamishna wa Ubia wa Kimataifa kutoka EU ambaye nae pia alisisitiza kuendeleza mshikamano baina ya nchi za EU na OACPS.

Katika hatua nyigine, Prof. Kabudi ameeleza kuwa kumalizika kwa mkutano wa 39 wa Bunge la pamoja baina ya nchi za ACP na EU kumetoa fursa ya kufanyika kwa mkutano wa wa Baraza la Mawaziri wa nchi za OACPS unaotegemewa kuanza kufanyika kwa njia ya mtandao (Video Conference) kuanzia tarehe 13 hadi 17.

Prof. Kabudi ameongeza kuwa katika mkutano huo, masuala muhimu yatakayo jadiliwa ni pamoja na Mapambano dhidi ya ugonjwa Corona, majadiliano ya mkataba mpya wa ubia mpya baina ya nchi za OACPS na Umoja wa Ulaya, Mageuzi (reforms) ndani ya Sekretariati ya OACPS, kusimamia kusainiwa kwa Mkataba ulioboreshwa wa Georgetown (the Revised Georgetown Agreement) na nchi za OACPS pamoja na Mikakati ya kufanya shughuli za Jumuiya ziguse zaidi Maisha ya wananchi.

Itakumbukwa kuwa Agosti 1, 2020 Tanzania ilikabidhiwa jukumu la kuongoza Jumuiya ya nchi za Afrika, Caribbean na Pasifiki (OACPS) kwa ngazi ya Mawaziri na kwa ngazi ya balozi Brussels.

Jukumu hilo ni heshima kubwa kwa Tanzania na ni ishara ya wazi ya jumuiya ya kimataifa kutambua kazi kubwa anayofanya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Joseph Magufuli ndani ya nchi na hivyo kutamani pia ushawishi wake huo uwe katika ngazi ya kimataifa hususan katika jumuiyan hii ya OACPS.

Hii ni mara ya tatu Tanzania kuchaguliwa kuwa  Mwenyekiti wa Jumuiya hii tangu ilipoanzishwa mwaka 1975. Tanzania ilikuwa Mwenyekiti mwaka 1992 na mwaka 2014.

Chini ya Uongozi wa Tanzania vipaumbele vikuu ni pamoja na kupambana na ugonjwa wa corona na athari zake, kusimamia kukamilishaji wa majadiliano ya mkataba mpya wa ubia kati yan chi za OACPS na Umoja wa Ulaya,  kusimamia mageuzi makubwa ndani ya Jumuiya ya OACPS ili iendane na wakati na kuelekeza rasilimali zake kwenye maeneo  muhimu yenye tija  kwa wanachama.

 Aidha, Tanzania pia imelenga kuimarishaji ushiriano miaongoni mwa nchi za OACPS (Connectivity) na kufanya mashauriano na wabia wetu wengine wa maendeleo ukiwemo Umoja wa Ulaya katika kuweka mifumo mizuri zaidi ya kuimarisha biashara, ongezeko la thamani ya mazao ya kilimo, matumizi ya digitali na fursa zaidi za masoko.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles