Mwandishi Wetu – Dar es Salaam
TANZANIA imewaahidi wajumbe wa kikao cha 43 cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa (UN), kuwa itafanya uchaguzi huru na haki kwa mujibu wa sheria.
Pamoja na hali hiyo, imesema kuwa hatua zote ambazo zimechukuliwa na Bunge kwa kufanya mabadiliko katika sheria za vyama vya siasa, sheria ya mashirika yasiyo ya kiserikali na ile ya vyombo vya habari zina lengo la kuimarisha uwajibikaji na uwazi pamoja na kuhakikisha misingi na tunu za taifa zinaheshimiwa na kuendelezwa.
Ahadi ya kufanyika kwa uchaguzi huru na wa haki sasa imevuka nje ya mipaka ya Tanzania ambapo kwa mara ya kwanza, ilitolewa na Rais Dk. John Magufuli, Januari 21, mwaka huu alipokutana na mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao Tanzania katika sherehe za mwaka mpya 2020 na chakula cha jioni zilizofanyika Ikulu, Dar es Salaam.
Rais Magufuli alisema kuwa utakapofika uchaguzi, nchi na taasisi mbalimbali zitakaribishwa Tanzania kushuhudia.
Akihutubia jana katika kikao cha 43 cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa (UN), linaloendelea Geneva nchini Uswisi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi, aliihakikishia Jumuiya ya Kimataifa kuwa Tanzania inaheshimu na itaendelea kuheshimu haki zote za binadamu zikiwemo za kisiasa.
Alisema sheria zilizotungwa na Bunge zina lengo jema la kuhakikisha Tanzania inabaki kuwa taifa lenye amani, umoja na utulivu.
Profesa Kabudi alisema kuwa mwaka huu Tanzania itafanya Uchaguzi Mkuu wa sita tangu kuanzishwa kwa vyama vingi vya siasa na kuihakikishia jumuiya hiyo kuwa uchaguzi huo utakuwa wa uwazi, huru na wa haki.
Alisema kuwa waangalizi mbalimbali wa uchaguzi wa ndani na nje ya nchi watakaotaka kushuhudia namna Watanzania wanavyotekeleza moja ya haki zao za msingi katika suala la kidemokrasia kwa kuchagua viongozi wao.
“Tanzania inaheshimu na itaendelea kutekeleza kwa vitendo haki zote za binadamu bila ubaguzi, na kwamba madai yanayoishutumu Tanzania kukiuka haki za binadamu ni propaganda na hasa zinatokana na hatua kali zinazochukuliwa dhidi ya rushwa, ubadhirifu wa mali za umma, madawa ya kulevya, uzembe katika ofisi za umma pamoja na hatua zinazochukuliwa kulinda rasilimali na maliasili ya Tanzania kwa manufaa ya Watanzania,” alisema Profesa Kabudi.
Akizungumza kuhusu masuala ya sheria mpya za huduma vyombo vya habari na haki ya kupata taarifa, Profesa Kabudi aliiambia jumuiya ya kimataifa kwamba sheria hizo zilizotungwa na Bunge zina lengo la kuimarisha, kulinda na kuweka mazingira bora zaidi kwa waandishi wa habari kutekeleza majukumu yao kwa usalama na kwa kuzingatia taaluma sambamba na kuwawezesha kupata haki zao ikiwa ni pamoja na mishahara bora na mikataba ya kazi.
MAREKANI YAPONGEZA
Siku chache baada ya kauli ya Rais Magufuli, kuahidi uchaguzi huru na wa haki, Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania ulimpongeza Rais Magufuli baada ya kiongozi mkuu huyo wa nchi kueleza kuwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2020 utakuwa huru na haki.
Mbali na pongezi hizo, ubalozi huo ulitaka kuharakishwa kwa uanzishwaji wa tume huru ya uchaguzi.
Januari 21, mwaka huu Rais Magufuli aliwahakikishia mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao Tanzania kuwa uchaguzi huo utakuwa huru na wa haki, ambapo kauli hiyo iliibua mjadala miongoni mwa vyama vya siasa na wanaharakati wa demokrasia wakihoji uwezekano huo bila kuwepo kwa tume huru ya uchaguzi.
Katika taarifa ya ubalozi huo iliyotolewa Januari 31, mwaka huu ubalozi huo umeonyesha kutiwa moyo na kauli ya kiongozi mkuu huyo wa nchi.
“Tunatoa wito wa kuharakishwa kwa zoezi la uandikishaji wapigakura lenye uwazi, kuanzishwa kwa tume huru ya uchaguzi na kuteuliwa mapema kwa waangalizi wa uchaguzi wa kitaifa na wa kimataifa wa kuaminika watakaofuatilia uchaguzi kwa kipindi kirefu na kipindi kifupi,” ilieleza taarifa hiyo.
KABUDI NA JUMUIYA YA MADOLA
Katika tukio jingine, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Kabudi, alikutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Patricia Scotland mazungumzo yaliyolenga masuala kadhaa, ikiwa ni pamoja na mradi ambao Jumuiya ya Madola umeufanya kuhusu Tanzania.
Mradi huo umelenga kuangalia takwimu mbalimbali zinazohusu biashara kwa kuangalia nchi ambazo Tanzania inaagiza ama kuuza bidhaa zake kwa wingi katika nchi za Jumuiya ya Madola mradi ambao umeelezwa kuwa na manufaa makubwa kwa nchi ambapo kwa sasa nchi za India na Afrika Kusini ndizo kinara.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Patricia, alisema Tanzania ni mdau muhimu katika jumuiya hiyo na kwamba amefurahi kumkabidhi Profesa Kabudi nakala ya utafiti huo kwa niaba ya Tanzania, jambo litakaloifanya kuendelea kuangalia maeneo ya kujiimarisha katika ufanyaji wa biashara na nchi za Jumuiya ya Madola.
Mbali na masuala hayo ya mradi huo wa takwimu wa biashara kuhusu Tanzania uliofanywa bure na Jumuiya ya Madola, pia viongozi hao walizungumzia masuala mengine ikiwa ni pamoja na namna jumuiya hiyo na Tanzania zitakavyofanya kuongeza usawa wa jinsia, masuala ya haki za binadamu pamoja na uimarishaji wa mfumo wa mahakama nchini.