NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM
WAKATI akifungua Maonesho ya Nne ya Wiki ya Viwanda ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), Rais Dk. John Magufuli, alihimiza ujenzi wa viwanda kwa nchi wanachama waweze kuchangamkia fursa zilizopo katika jumuiya hiyo.
Takwimu zinaonesha idadi ya watu katika jumuiya hiyo ni milioni 350 lakini urali wa biashara baina ya jumuiya hiyo na mataifa mengine bado si mzuri licha ya kuwa na rasilimali nyingi kulinganisha na mabara mengine.
Takwimu za mwaka 2017 zinaonyesha ufanyaji biashara kati ya Afrika na Umoja wa Ulaya ulikuwa Sh trilioni 708 (Euro bilioni 280) ambapo Afrika ilinunua bidhaa za Sh trilioni 376.7 (Euro bilioni 149) na ikauza bidhaa za Sh trilioni 331 (Euro bilioni 131) huku asilimia 60 bidhaa zilizouzwa zikiwa ni ghafi hivyo kuwa na thamani ni ndogo.
Kwa upande wa Tanzania imekuwa ikifanya vizuri katika biashara ndani ya SADC ambapo mauzo kwa mwaka jana yalikuwa Dola za Marekani milioni 999.34 ikilinganishwa na milioni 877.8 mwaka juzi.
Katika kipindi hicho, uagizaji wa bidhaa kutoka SADC uliongezeka kutoka Dola za Marekani milioni 600.64 hadi milioni 604.32 mwaka jana.
Bidhaa ambazo Tanzania inauza SADC ni madini mbalimbali kama vile Tanzanite na dhahabu, bidhaa za kilimo yaani chai na kahawa, bidhaa za viwandani, plastiki, sigara na saruji, marumaru, madawa na vifaa tiba.
Bidhaa ambazo Tanzania inanunua kutoka nchi za SADC zinahusisha magari, mbegu za mahindi, gesi, mabati, vilainishi, bia na sukari na zaidi zinatoka Afrika Kusini, Zambia, Mauritius na Malawi.
Maonesho ya Nne ya Wiki ya Viwanda ya SADC yamefungua milango ya masoko na bidhaa na wananchi wengi wamepata fursa ya kujionea namna nchi za SADC zilivyodhamiria kukuza uchumi kupitia viwanda na biashara.
Kulikuwa na mwitikio mkubwa wa wadau hapa nchini ambao walichangamkia fursa ya kuonyesha bidhaa zao na wengine walishiriki katika mijadala mbalimbali.
Maonesho hayo yameonyesha namna teknolojia inavyokua kwa wazalishaji wa ndani kwani maeneo ambayo awali ilionekana hawamudu wazalishaji wameonyesha uwezo mkubwa.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa, anasema wataendelea kuweka mazingira mazuri ya shughuli za uzalishaji wa malighafi na bidhaa za viwandani ili kuwa na wepesi wa kufanya biashara.
“Biashara ikifanyika vizuri inakuwa kichocheo cha kukuza sekta nyingine nyingi za kiuchumi na wananchi wanapata fursa ya kushiriki katika shughuli hizo na kupanua wigo wa fursa za ajira,” anasema Bashungwa.
Maonyesho hayo yaliyokuwa na kaulimbiu ‘Mazingira Wezeshi kwa Maendeleo Jumuishi na Endelevu ya Viwanda’ yalishirikisha washiriki 5,352 ambapo waonyeshaji walikuwa 585 vikiwemo viwanda 69, taasisi za umma 61, taasisi za fedha 65 na wajasiriamali 405.
Baadhi ya taasisi za umma na wenye viwanda wameonyesha namna walivyojiandaa kuliteka soko la SADC.
Wenye viwanda
Mkurugenzi wa Mahusiano wa Kampuni za Bakhresa, Hussein Sufian, anasema baada ya kujitosheleza ndani wamejitanua katika mataifa mbalimbali ya Afrika na tayari wanapeleka bidhaa zao katika nchi saba za SADC.
Nchi hizo ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Angola, Comoro, Msumbiji, Malawi, Zimbabwe na Afrika Kuisini.
“Soko letu baada ya kujitosheleza ndani tulijipanua katika mataifa mbalimbali ya Afrika, tunafikisha bidhaa zetu katika nchi mbalimbali za SADC,” anasema Sufian.
Anasema pia katika kukuza ajira na kuongeza tija katika uzalishaji wamekuwa wakichukua malighafi za hapa nchini na kwamba asilimia 15 ya bidhaa zao wanazisafirisha nje ya Tanzania hasa hizi nchi za SADC.
Anasema kampuni hiyo ina viwanda mbalimbali vikiwamo vinne vinavyosindika bidhaa za vyakula na kwamba kiwanda cha kusindika matunda kilichopo Mwandege Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, uwekezaji wake umegharimu Dola milioni 210.
Naibu Meneja wa kiwanda cha kuzalisha maji ya Uhuru Peak cha Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMA JKT), Meja Makala Nzinza, anasema kitendo cha maji yao kutumika katika shughuli mbalimbali za mkutano wa SADC ni fursa ya wao kujitangaza kwa nchi wanachama hivyo wataitumia kuliteka soko hilo.
Mkurugenzi wa Kiwanda cha 21 Century, Aminderjiti Singh Billu, anasema mkutano huo umewaongezea nguvu ya kusambaa zaidi katika nchi za jumuiya hiyo.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji (EPZA), Joseph Simbakalia, anasema moja ya mikakati ya kuendeleza uchumi wa viwanda ni kujenga maeneo maalumu ambayo yameandaliwa kwa uwekezaji na yenye huduma zote muhimu zikiwemo maji na umeme.
Anasema eneo hilo lina ekari 63 lakini yako maeneo mengine yameandaliwa yakiwamo Bagamoyo (Kilomita za mraba 100), Morogoro (zaidi ya ekari 8,600), Tanga, Manyara, Bunda na Kigoma.
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, viwanda vilivyopo eneo hilo ni vile vinavyotengeneza bidhaa ambazo ni sehemu ya mahitaji ya msingi ya binadamu kama vile mavazi na chakula.
Katika eneo hilo kuna kiwanda cha nguo, kusindika na kufungasha kahawa, kubangua na kufunga vyakula aina ya mikunde yaani choroko, dengu, mbaazi na ufuta.
Dk. Somani wa kiwanda cha kuzalisha mazao jamii ya mikunde kilichopo EPZA, anasema wanauza Canada, Pakistani, India, Malaysia, Singapore, Afrika Kusini, Qatar na kwamba wataendelea kujitanua zaidi katika nchi za SADC.
Mkurugenzi Mkuu wa Lodhia Group of Companies, Sailesh Pandit, anasema kampuni hiyo ilianzishwa mwaka 1996 wanafanya biashara ya jumla ya kuuza vyuma na mwaka 2004 walianza kuzalisha katika kiwanda kilichopo mkoani Arusha.
Anasema pia wamegeukia bidhaa nyingine zikiwamo mabomba ya maji, gypsum board, matenki ya ya kuhifadhia maji na bidhaa nyingine za ujenzi ili kuhakikisha Tanzania inajitosheleza katika vifaa vya ujenzi bila kuagiza nje ya nchi.
Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC), Profesa Damian Gabagambi, anasema Kiwanda cha Viuadudu kilichopo Kibaha mkoani Pwani kina mchango mkubwa katika kutokomeza malaria na kuwaomba wajumbe wa SADC watakaporudi katika nchi zao wakawe mabalozi ili waweze kutokomeza ugonjwa huo kwa pamoja.
Anasema uwezo wa mashine zilizosimikwa ni kuzalisha lita milioni sita kwa mwaka lakini wamekuwa wakikwama kuzalisha kiasi hicho kwa sababu ya masoko.
“Uwezekano wa kupata masoko Tanzania na nchi za jirani ni mkubwa mno, kama tungeweza kuwatangazia na kuwahimiza magereza, shule za bweni, makanisa na hospitali zote nchini unaweza kuona ni soko kubwa kiasi gani,” anasema Profesa Gabagambi.
Nalo Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), tayari limepata fursa ya kuuza gesi katika nchi za Zambia, Malawi na DCR.
Mkurugenzi Mkuu wa TPDC, Dk. James Mataragio, anasema hivi sasa matumizi ya gesi yameongezeka na nchi mbalimbali zikiwemo za SADC zimeonyesha nia ya kutaka kuuziwa gesi na shirika hilo.
“Tumeshaanza kufanya upembuzi yakinifu katika baadhi ya maeneo na Tanzania tuna uzoefu wa zaidi ya miaka 50 katika ujenzi wa miundombinu ya nishati hasa kwenye eneo la gesi na mafuta.
“Tulishiriki kujenga mabomba manne yakiwamo yale yanayosafirisha mafuta mazito (Tanzania – Zambia), linalosafirisha gesi (Mtwara – Dar es Salaama) na Songosongo – Dar es Salaam,” anasema Dk. Mataragio.
Baraza la Biashara SADC
Katibu Mtendaji wa Baraza la Biashara la SADC, Peter Varndell, anasema ukanda huo una utajiri mkubwa lakini bado hawajaweza kuuendeleza na kufikia viwango vya ushindani kwani hata biashara baina yao imekuwa chini kwa asilimia 25.
Varndell ambaye aliwasilisha maazimio ya baraza hilo wakati wa kufunga Maonyesho ya Nne ya Wiki ya Viwanda, anasema mazingira mazuri ya biashara yatasaidia kukuza biashara na ajira kikanda.
Miongoni mwa maazimio ya baraza hilo ni nchi wanachama kuhimiza ushirikiano baina ya sekta ya umma na binafsi, kuainisha sera na sheria zinazosababisha ufanyaji biashara kuwa mgumu, kusimamia sera na kuharakisha maendeleo ya vijana katika jumuiya hiyo.
Mengine ni kuwa na mfuko wa kuendeleza teknolojia na ubunifu, kuwawezesha wanawake na vijana kuhakikisha wanashiriki katika ujenzi wa viwanda na kuwa na mpango kabambe wa kuzalisha gesi ya kutosha ili watu waweze kuanzisha viwanda kwa wingi.
Mwenyekiti wa baraza hilo, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Salum Shamte, alimuomba Rais Magufuli kusukuma mbele ajenda ya biashara ili waweze kunufaika na eneo huru la biashara Afrika.
Shamte anasema zaidi ya asilimia 90 ya ajira zinatengenezwa na sekta binafsi katika nchi za SADC lakini bado sekyta hiyo inakabiliwa na changamoto nyingi.
Anasema kutokana na vikwazo hivyo gharama za kufanya biashara Afrika ni zaidi ya mara saba kulinganisha na nchi za Asia.
Anasema pia zaidi ya Dola bilioni 30 zimekuwa zikitumika kuagiza chakula nje wakati kuna asilimia 60 ya ardhi inayoweza kutumika kuzalisha.
“Tuachane na ushindai usio na maana tukumbatie zaidi ushirikiano kuhakikisha miradi midogo na mikubwa inafanikiwa. Tunaunga mkono jitihada za serikali kupata suluhisho la matatizo yetu na hatuna sababu ya kuendelea kulalamika,” anasema Shamte.
Wajumbe walioshiriki Maonyesho ya Nne ya Wiki ya Viwanda pia walipata nafasi ya kutembelea viwanda mbalimbali vilivyopo Tanzania Bara na Visiwani na kuridhishwa na namna Tanzania ilivyopiga hatua katika ujenzi wa uchumi wa viwanda.
Mmoja wa wajumbe kutoka Afrika Kusini, Renatus Joseph, anasema kuna matumizi makubwa ya teknolojia katika viwanda vilivyoko nchini na kama itakuzwa nchi nyingine kutakuwa na bidhaa zinazoleta ushindani ndani na nje ya Afrika.
This is a appealing article by the way. I am going to go ahead and bookmark this post for my sister to read later on tonight. Keep up the good work.