23.3 C
Dar es Salaam
Tuesday, May 21, 2024

Contact us: [email protected]

Hong Kong yasitisha safari za ndege maandamano yakipamba moto

HONGKONG

MAMLAKA za HongKong jana zilisitisha safari za ndege baada ya viwanja vya ndege kuonekana kuzidiwa na waandamanaji.

Hatua hiyo inaelezwa kuathiri safari za ndege 100 zinazoingia na kutoka Hong Kong.

Waandamanaji hao wanaounga mkono demokrasia walivamia uwanja wa ndege siku nne zilizopita ukiwa ni muendelezo wa maandamano kama hayo yaliyochukua takribani miezi miwili katika maeneo mbalimbali ya HongKong wakipinga uamuzi wa serikali kutaka kupitisha sheria inayotaka raia wa eneo hilo kushitakiwa nchini China. 

Mamlaka ya viwanja wa ndege ya Hong Kong ilisema kuwa wamesitisha safari zote za kutoka na kuingia nchini humo kupitia katika uwanja wake wa ndege kutokana na maelefu ya waandamanaji kuingia eneo linalotumika kwa ajili ya wageni wanaowasili.

“Pamoja na ndege zinazondoka kukamilisha taratibu zote na zile ambazo tayari zinaelekea Hong Kong,  na ndege nyingine tumesitisha kwa siku ya leo,” ilieleza taarifa ya mamlaka ya viwanja vya ndege.

“Shughuli za uwanja wa Kimataifa wa ndege Hong Kong vimevurugwa kwa sababu ya waandamanaji,” ilieleza taarifa hiyo.

Inaelezwa kuwa kutokana na maandamano hayo kulikuwa na msongamano mkubwa wa magari na katika maegesho kulikuwa hakuna nafasi yeyote.

“Umma unashauriwa kutofika uwanja wa ndege,” iliongeza taarifa hiyo.

Idadi ndogo tu ya ndege ndiyo iliyoruhusiwa kutua katika uwanja wa ndege wa Hong Kong.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, mamlaka za Hong Kong pia zilishauri abiria wote kuondoka katika eneo la uwanja wa ndege haraka iwezekanavyo.

Vyombo vya habari vya Hong Kong pia viliripoti kuwa wafanyakazi wa uwanja wa ndege nao walitakiwa kuondoka katika eneo hilo haraka iwezekanavyo, wakiwamo wale wa mashirika makubwa kama Cathay  na Hong Kong Airlines.

Mwandishi wa Al Jazeera, aliyeko Hong Kong Rob McBride alisema zaidi ya waandamanaji 5,000 wameripotiwa kuvamia uwanja wa ndege.

“Kuna hali ya hasira …polisi walilazimika kutumia mabomu ya machozi, hasira inatokana na kile ambacho waandamanaji wanadai polisi haijawatendea haki,” alisema McBride.

Hali kuendelea kutokuwa shwari huku maandamano  hayo yakichukua miezi zaidi ya miwili sasa hatua hiyo imeiingiza HongKong kwenye mzozo mkubwa wa kisiasa kuwahi kutokea ndani ya muongo mmoja  na hivyo kuleta changamoto kwa China.

Maandamano hayo ambayo yalinza baada ya mamlaka za Hong Kong kupeleka muswada tata bungeni, yamevuka mipaka na sasa raia wa eneo hilo wanataka mabadiliko ya kidemokrasia  na zaidi uchunguzi huru juu ya utendaji wa polisi  waliouonyesha wakati wa kudhibiti maandamano hayo.

Waandamanaji pia wanataaka kiongozi wa Hong Kong Carrie Lam kujiuzulu na kuitisha uchaguzi ili kumtafuta mrithi wake.

Mwishoni mwa juma lililopita,  waandamaji walirusha vizuizi vilivyokuwa vimewekwa barabarani, polisi walijaribu kuwatawanya waandamanaji waliokuwa katika njia ya chini ya treni kwa mabomu mfululizo ya machozi  na kwa mara ya kwanza kuwarushia risasi za mpira.

Waandamanaji wengi wamekamatwa, wakati mwingine baada ya kipigo kutoka kwa polisi.

Inaelezwa kuwa zaidi ya watu 600 wamekamatwa tangu maandamano  hayo yaanze.

Mamlaka za nchini China zimeeleza kuwa kinachofanywa na waandamanaji hao ni kitendo cha ugaidi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles