SERIKALI za Tanzania na Misri zimekubaliana kuendelea na mazungumzo ya kuhakikisha matumizi ya Mto Nile yanazifaidisha nchi zote zinazotakiwa kupata maji ya mto huo.
Makubaliano hayo yamefikiwa leo Agosti 14, jijini Dar es Salaam wakati wa mazungumzo baina ya Rais Dk. John Magufuli na Rais wa Misri, Abdel Fattah Al Sisi, ambaye amewasili nchini kwa ziara ya kikazi.
“Ziara yake imezaa matunda mazuri na utekelezaji wake ukifanyika vizuri mafanikio makubwa ya kiuchumi yatapatikana, tutaendelea na mazungumzo na kuzihusisha nchi mbalimbali zinazotumia Mto Nile ili ziweze kunufaika na mto huo,” amesema Rais Magufuli.
Aidha, amesema pia wamesaini makubaliano mengine ya kuisaidia Tanzania katika sekta za viwanda, kilimo, afya, utalii, ulinzi na elimu ambapo Misri wataanzisha kiwanda cha nyama ili mifugo ichinjwe nchini na nyama isafirishwe Misri na nchi nyingine.
Pamoja na mambo mengine, amesema Serikali ya Misri imeahidi kuongeza fedha kuhakikisha Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) inafanya upasuaji wa figo kabla ya mwaka 2020 lakini pia kuhusu sekta ya utalii, alisema wamekubaliana kubadilishana uzoefu ili kusaidia kuendeleza sekta hiyo.
Awali Rais wa Misri, Al Sisi alisema wataendelea kujenga uwezo na kubadilishana wataalamu katika miradi mbalimbali.
“Mahusiano kati ya Tanzania na Misri ni mfano wa kuigwa na kumekuwa na ushirika kati ya mataifa haya ambayo yameunganishwa na Mto Nile, tuna matumaini makubwa ya kuwa na maendeleo endelevu, kukuza biashara na kuongeza uwekezaji,” amesema Al Sisi.