29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

BALOZI MWAMBULUKUTU AFARIKI DUNIA

Na  AGATHA CHARLES

ALIYEKUWA Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Emmanuel Mwambulukutu (73) amefariki dunia usiku wa kuamkia juzi, kutokana na maradhi ya sukari.

Akizungumza nyumbani kwa marehemu, Mikocheni, Dar es Salaam jana, kaka wa marehemu Ulli Mwambulukutu, alisema marehemu hakuwa sawa kiafya tangu alipopatwa na shambulio la majambazi mwishoni mwa mwaka 2007.

“Hajaumwa ile ya kusema kuumwa, kama utakumbuka kuelekea mwaka 2008, aliumia akiwa Afrika Kusini. Alivamiwa na majambazi. Alipona baada ya kutibiwa, lakini hakuwa sawa.

“Alikuwa na sukari ambayo aliendelea kuidhibiti ingawa hali ilikuwa inabadilikabadilika, nguvu kupungua na kupumua ilikuwa inampa shida,” alisema Ulli.

Alisema baada ya kuendelea kwa miaka kadhaa katika hali hiyo, juzi hali yake ilibadilika na kulazimika kumpeleka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambako alifariki dunia akipatiwa matibabu.

“Jana (juzi) saa tatu usiku alikuwa hapa nje, baadaye akaenda chumbani kupumzika lakini hali ikabadilika ikawa si nzuri, tukatafuta ambulance saa nne tukawa tumemfikisha emergence Muhimbili, alifariki wakiwa wana mhudumia,” alisema Ulli.

Alisema mwili wa Balozi Mwambulukutu ambaye ameacha mke na watoto wanne, unatarajiwa kusafirishwa kwenda Tukuyu mkoani Mbeya, baada ya vikao vya familia vinavyoendelea kukamilisha taratibu.

Enzi za uhai wake akiwa Balozi nchini Afrika Kusini, Mwambulukutu aliwahi kushambuliwa na majambazi eneo la Garsfontein na kuumizwa vibaya, ambako aliwekwa chumba maalumu cha uangalizi (ICU) katika hospitali moja mjini Pretoria.

Katika uvamizi huo ambao majambazi walilenga kuiba gari, mke wake naye alijeruhiwa.

Itakumbukwa marehemu Mwambulukutu enzi za uhai wake kabla ya kustaafu 2010 kazi ya balozi huko Afrika Kusini, aliwahi kushika nyazifa mbalimbali serikalini pamoja na kuwa mbunge.

Moja ya nyazifa hizo, alikuwa mbunge katika moja ya majimbo mkoani Mbeya kuanzia mwaka 1985 hadi 1995. Aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Serikali za Mitaa, Maendeleo ya Jamii, Ushirika na Masoko mwaka, 1988 hadi 1990.

Aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa mwaka 1990 hadi 1991 na baadaye kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimatifa, mwaka 1991 hadi 1993.

Mwaka, 1993 hadi 1995, aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo Mijini na mwaka 1995 aligombea ubunge Jimbo la Rungwe Mashariki na kushinda ambapo alihudumu hadi mwaka 2000.

Baada ya nafasi hiyo, mwaka 1995 aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani hadi 1999 chini ya aliyekuwa waziri wa wakati huo, Jakaya Kikwete.

Desemba 1999 hadi Juni, 2008, alikuwa Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini.

Marehemu  Mwambulukutu, alipata Shahada ya Juu ya Sanaa katika fani ya Ualimu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na baadaye aliendelea na Shahada ya Juu ya Filosofia ya Maendeleo ya Uchumi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam  na alihitimu  Shahada ya Umahiri kutoka Chuo Kikuu cha Princeton New Jersey nchini Marekani katika fani ya Elimu ya Masuala ya Kimataifa na Maendeleo ya Umma Kitivo cha Woodrow Wilson.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles