Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital
Serikali ya Tanzania na Malawi zimesaini mkataba wa ushirikiano kuhusu ushoroba wa usafirishaji baina ya nchi hizo mbili kutokana na Malawi kutumia Bandari ya Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa wakati wa hafla ya kusaini makubaliano hayo amesema kwenye bandari ya hiyo kuna faida kubwa.
Amesema kwa kutumia bandari hiyo imezifanya bidhaa na mambo mengine kuwa na bei nzuri nchini Malawi.
“Mkataba huu ulikuwa wa mda mrefu tumeweza kusaini upya na kuhakikisha kwamba sasa unafanya vizuri zaidi, serikali imejenga miundombinu mingi kwa ajili ya kuboresha ushoroba huo wa usafirishaji kati ya nchi hizi mbili,” amesema Profesa Mbarawa.
Amesema wamefanya maboresho makumbwa kwenye bandari ya Dar es Salaam kuanzia gate namba moja hadi saba pia wamejenga gate maalum kwa ajili ya gate namba sifuri.
Amesema wameanza kuleta sekta binafsi na wawekezaji kwenye bandari ya hiyo na wanafanya hayo yote kuhakikisha wanaongeza ufanisi.
Profesa Mbarawa amesema kuhusu bandari ya Mtwara wamefanya mabadiliko makubwa, wamejenga gate ya kisasa mbali na urefu takribani mita 300 inafanya kazi kwa vifaa vya kisasa.
Ameongeza kuwa wiki inayokuja wanatarajia kusaini mkataba wa ujenzi wa bandari ya Mbamba Bay kwa kuwa ni muhumi kwa ziwa Nyasa.
“Bandari muhimu kwa ajili ya watu wa Malawi, jitihada zote zinafanywa kuhakikisha wanafungua ushoroba huu kati ya Tanzania na Malawi,”‘amesema.
Ameeleza kuwa mkataba huo una faida kwa Tanzania na Malawi, mwaka 2022 mzigo ulihudumiwa na bandari ya Dar es Salaam kwa nchi ya Malawi ulikuwa takribani ya zaidi tani laki 5.
“Lakini ukilinganisha na mwaka 2018 kumekuwa na ongezeko kubwa hivyo wanataka ongezeko lifikie hadi tani million moja au mbili hiyo itawasaidia kuongeza ufanisi wa bandari ya Dar es Salaam,” ameongeza.
Aidha amesema wamekuwa wakisaini mikataba ya kuifungua bandari hiyo japo kuna ushindani ila wakijipanga vizuri na miundombinu wanayojenga sasa hakuna mtu ataweza kushindana nayo
Naye Waziri wa Uchukuzi wa Malawi, Jacob Hara amesema wamefurahi kusaini mkataba huo kati ya nchi hizo mbili na kushirikiana kwa pamoja ni muhimu.
“Anaamini mkataba huu tuliosaini utasaidia kufanya kazi kwa pamoja kati ya Tanzania na Malawi na kurahisisha usafirishaji na ni fursa kwa nchi zote mbili,”amesema Hara