25.5 C
Dar es Salaam
Wednesday, January 8, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

TANZANIA ILIVYOJENGA MSINGI MATIBABU YA KIBINGWA

NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM


HERI ya mwaka mpya msomaji wa gazeti la MTANZANIA na hasa jarida la Jamii na Afya. Kwa pamoja tunapaswa kumshukuru Mwenyezi Mungu kutujalia kufika mwaka mpya wa 2018.

Mengi yalitokea mwaka 2017 na katika makala haya tunaangazia huduma za matibabu ya kibingwa nchini dhidi ya magonjwa mbalimbali.

UPASUAJI WA KIBYONGO

Mwaka jana jumla ya wagonjwa 13 walifanyiwa upasuaji wa kutibu tatizo la kibyongo ‘scoliosis’ katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa, Mgongo, Ubongo na Mishipa ya Fahamu Muhimbili (MOI).

Akizungumza na MTANZANIA Meneja Uhusiano na Ustawi wa MOI, Almasi Jumaa, alisema upasuaji huo wa aina yake ulianza kutolewa katika taasisi hiyo Januari, 2017.

Upasuaji huo ulifanywa na madaktari bingwa wa upasuaji wa mifupa na mgongo (Spine Surgeons) wakishirikiana na wale wa upasuaji wa ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu (Neurosurgeons) wa taasisi hiyo.

Upasuaji huo huhitaji wataalam bobezi na kwamba ni mgumu na mkubwa kufanyika kwani huwa wanafanya ili  kunyoosha mgongo uliopinda na kuonekana kama herufi ‘S’ unyoke na kuwa wa kawaida.

“Wakati mwingine mgonjwa inabidi afanyiwe upasuaji kwa hatua. Anaweza kufanyiwa upasuaji hata mara tatu ili kuhakikisha mgongo unanyooka kabisa,” alisema.

Jumaa alisema kabla ya kuanza kufanyika upasuaji huo MOI wagonjwa walikuwa wakipewa rufaa kwenda nje ya nchi ambako gharama za matibabu ni ghali.

“Gharama ya matibabu ya upasuaji huu kwa mgonjwa mmoja nje ya nchi ni Dola za Marekani 20,000 hivyo kwa wagonjwa 13 serikali ingegharamia Dola 260,000 ambazo ni sawa na zaidi ya Sh milioni 500 ambazo tumeziokoa kwa kufanya upasuaji huo nchini,” alibainisha.

UPASUAJI WA UBONGO

Novemba mwaka jana, MOI ilifanikiwa kufanya upasuaji mkubwa wa ubongo kwa mgonjwa aliyepooza mwili kutokana na ajali ya barabarani.

Wiki mbili baada ya upasuaji huo kufanyika mgonjwa huyo aliweza kusimama, kutembea na kula chakula mwenyewe bila kusaidiwa na mtu.

Upasuaji huo wa aina yake ulifanywa katika taasisi hiyo na madaktari bingwa upasuaji wa ubongo, uti wa mgongo na mishipa ya fahamu, Nicephorus Rutabasibwa na Laurent Lemery.

Dk. Rutabasibwa alisema upasuaji huo kitaalamu unaitwa Craniocervical Stabilization and Fussion.

“Ni upasuaji mkubwa unaohusisha kuunganisha mishipa ya fahamu iliyovunjika ya mgonjwa, alikuwa amevunjika mno katika pingili za mifupa ya kichwa hasa eneo la kichogo inapoungana na uti wa mgongo,” alisema Dk. Rutabasibwa.

Daktari huyo alisema kutokana na kuvunjika kwa uti wa mgongo ndiko kulisababisha mgonjwa huyo kupooza mikono na miguu yake.

“Tulipompokea alikuwa hawezi kushika kitu chochote hata kutembea, alikuwa analala tu kitandani muda wote baada ya kufanikisha upasuaji huo aliweza kuinuka na kufanya kila kitu pasipo kusaidiwa,” alisema.

Alisema ni upasuaji ghali na kwamba walimuwekea vipandikizi nane, na kila kimoja kinauzwa Dola 1,000 sawa na Sh milioni 2, imegharimu takriban zaidi ya Sh milioni 10 kumtibu,” alisema.

Alisema iwapo mgonjwa huyo angepelekwa nje ya nchi kufanyiwa upasuaji huo ingegharimu zaidi ya Sh milioni 25 ikiwa ni gharama za tiba, usafiri na gharama za daktari msindikizaji.

“Zaidi ya asilimia 50 ya wagonjwa tunaowahudumia hapa MOI ni wa ajali hasa za bodaboda, ni muhimu wakafuata sheria za usalama barabarani kuepuka ajali,” alisema.

TEZI DUME

Saratani ya tezi dume ni miongoni mwa magonjwa yanayowatesa wanaume wengi nchini.

Mwishoni mwa mwaka jana, Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) ilifunga mashine mbili zenye uwezo wa kutibu ugonjwa huo.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Saratani wa ORCI, Mark Mseti, alisema wanatarajia kuanza kutoa matibabu hayo Januari mwaka huu baada ya mafundi kukamilisha kazi hiyo.

“Ni mashine zenye uwezo wa hali ya juu mno ambazo zinatumika katika mataifa makubwa duniani katika kutoa matibabu dhidi ya saratani ya tezi dume.

“Hizi ni tofauti na zile tulizonazo ambazo zilifungwa kwa muda mrefu, hizi zinazofungwa sasa zina uwezo wa kutibu kabisa tatizo la saratani ya tezi dume,” alidema Dk. Mseti.

Dk. Mseti alisema pamoja na maboresho hayo changamoto kubwa ni wanaume kuwa waoga kujitokeza kufanya uchunguzi kujua iwapo wanakabiliwa na tatizo hilo au la.

“Wengi wanaogopa kipimo cha kidole, lakini niwatoe hofu kwamba siku hizi tunacho kipimo maalumu cha damu kinaitwa kitaalamu PSA, tunakitumia kufanya uchunguzi wa awali.

“Hivyo nawasihi wajitokeze, saratani inapogundulika mapema matibabu yake yanakuwa rahisi na kwa kuwa mgonjwa anapewa matibabu sahihi huwezekano wa kupona ni mkubwa ikilinganishwa na akichelewa matibabu.

UPANDIKIZAJI VIFAA VYA USIKIVU

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma na Huduma kwa Wateja MNH, Aminiel Aligaesha, alisema Januari mwaka huu wanatarajia kufanya upasuaji huo kwa awamu ya pili.

Julai mwaka jana, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alizindua rasmi huduma ya upasuaji na upandikizaji kifaa cha usikivu kwa watoto waliozaliwa na tatizo hilo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Mkurugenzi wa Muhimbili, Profesa Lawrence Museru, alisema tatizo la usikivu limekuwa likiongezeka katika jamii ya Watanzania kama ilivyo kote duniani.

Alisema utafiti wa makadirio ya hospitali hiyo unaonesha kwa mwaka takribani watoto 200 watahitaji huduma hiyo nchini.

“Utaalamu ambao umeendelezwa takribani miaka 20 ya karibuni unaonyesha kuwa watoto wakigundulika mapema na kuwekewa vifaa vya usikivu wataishi kama kawaida, wasipopata huduma hii watakuwa viziwi,” alisema Profesa Museru.

Alisema kwa mara ya kwanza mwaka 2003, Muhimbili ilipeleka mgonjwa mmoja kwenda kutibiwa nchini India na tangu hapo wagonjwa wanaohitaji huduma hiyo wamekuwa wakiongezeka huku huduma hiyo ikiwa na gharama kubwa kati ya Sh milioni 80 hadi Sh milioni 100 kwa mgonjwa mmoja.

Hadi kufikia 2016 ni wgonjwa 50 tu waliokuwa wamefaidika kupata huduma hiyo ya ufadhili kutoka Serikalini.

Alisema kuanzishwa  kwa huduma hiyo nchini Serikali itapunguza gharama kwa asilimia 60 na kufikia wastani wa Sh milioni 36 kwa mgonjwa mmoja hivyo, hatua hiyo itasaidia wagonjwa wengi kufanyiwa upasuaji huo nchini.

Kutokana na kuanza kutolewa kwa huduma hiyo nchini, Waziri Ummy alisisitiza kwamba serikali haitagharamia tena matibabu ya huduma hiyo nje ya nchi na ikiwa kuna mtu atahitaji kwenda nje atakwenda kwa gharama zake mwenyewe.

UPANDIKIZAJI FIGO

Novemba 21, 2017 Madaktari Bingwa wa Magonjwa ya Figo wa Hospitali ya Taifa Muhimbili wakishirikiana na wenzao wa Hospitali ya BLK ya New Delhi, India kwa mara ya kwanza walifanikiwa kufanya upasuaji wa kihistoria wa upandikizwaji wa figo.

Walimfanyia upasuaji huo mwanamke mwenye umri wa miaka 29 ambaye alipatiwa figo na ndugu yake na alikuwa katika hatua ya tano ya ugonjwa huo.

Waziri Ummy alisema kwamba upasuaji huo wa kihistoria ni kielelezo cha juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano za kuboresha huduma za afya nchini zikiwemo zile za ubingwa wa daraja la juu.

“Upasuaji huu ni juhudi zinazofanywa na serikali za kupunguza rufaa za wagonjwa wanaohitaji huduma hizo nje ya nchi na hivyo, itaokoa fedha ambazo zingelipwa nje ya nchi kugharamia matibabu hayo. Badala yake fedha hizo zitatumika katika maendeleo kwenye maeneo mengine,” alisema.

Zaidi ya mwaka mmoja hospitali hiyo ilijikita kuwekeza katika kuongeza ujuzi wa wataalamu wa aina mbalimbali ambapo ilipeleka nchini India wataalamu wa upasuaji wa kupandikiza figo kwa mafunzo ya vitendo na wataalamu wawili walipelekwa nchini Norway.

Alisema kuanza kutolewa kwa huduma hiyo nchini, kutawezesha serikali kuokoa fedha na kupunguza gharama ya kupeleka wagonjwa nje ya nchi kufuata matibabu hayo.

Alisema kwa mwaka iligharamia matibabu ya wagonjwa 35 ambapo gharama kwa kila mmoja ilikuwa Sh milioni 80 hadi Sh milioni 100 hivyo kwa huduma hiyo kutolewa nchini itagharimu Sh milioni 21 pekee.

HOSPITALI YA KISASA

Novemba 25, 2017, Rais Dk. John Magufuli, alizindua rasmi Hospitali ya Rufaa ya Taaluma na Tiba (MAMC) ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) iliyoko Mloganzila, jijini Dar es Salaam.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Mpoki Ulisubsya, alisema hospitali hiyo imeanza kutoa huduma za matibabu.

Dk. Ulisubsya alisema inapokea wagonjwa waliopewa rufaa kwa ajili ya matibabu ya magonjwa ya ndani (internal medicine).

Alisisitiza hospitali hiyo ina uwezo wa kutoa huduma za kibingwa kwa kiwango kama kile ambacho kinatolewa Muhimbili na kwamba, MAMC inashirikiana na wataalamu mabingwa kutoka MNH katika kuhudumia wagonjwa.

“Wizara inawahakikishia wananchi na wadau wote kuwa, huduma zinazotolewa na MAMC zinajumisha pia huduma za daraja la ubingwa wa ngazi ya juu (super specialized services) na zenye ubora stahiki,” alisema.

UPANDIKIZAJI INI

Mwishoni mwa mwaka jana, Muhimbili ilipeleka nchini India wataalamu saba kwa ajili ya kujifunza jinsi ya kufanya upasuaji wa kupandikiza ini na kutibu magonjwa ya mfumo wa chakula.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma MNH, Aligaesha alisema mafunzo hayo yatachukua muda wa miezi mitatu.

Anasema timu hiyo ya wataalam inajumuisha madaktari bingwa wanne wa magonjwa ya mfumo wa chakula na ini, wauguzi wawili wanaosimamia mifumo ya hadubini na mhandisi wa vifaa tiba anayesimamia mitambo ya hadubini.

“Lengo la Hospitali ni kuendelea kutekeleza azma ya serikali kwa vitendo ya kupunguza rufaa za nje ambazo serikali ilikuwa ikigharamia fedha nyingi kutokana na kutokuwapo kwa wataalam wa kutibu magonjwa hayo.

‘’Utekelezaji huu unasaidia wagonjwa kupata huduma sahihi wakiwa hapa hapa nchini na kupunguza vifo visivyo vya lazima kwani wakati mwingine ililamizimika wagonjwa hawa kusubiri kwa muda mrefu,’’ alisema Aligaesha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles