25.8 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

TANROADS IMEKUJA NA SULUHU YA TATIZO LA MSONGAMANO WA MAGARI DAR

Na ISMAIL NGAYONGA -MAELEZO

JIJI la Dar es Salaam ni miongoni mwa miji inayokua kwa kasi kubwa duniani, huku ukuaji huo ukiathiri sekta mbalimbali za kijamii na kiuchumi ikiwemo ya usafirishaji.

Tangu miaka ya 1990 kumekuwa na mipango mbalimbali ya kuboresha usafiri katika Jiji la Dar es Salaam, ikiwemo kuanzisha barabara za njia moja, kuanzisha maegesho ya magari ya kulipia na kuhamasisha kujengwa kwa majengo yenye maegesho ya magari.

Pamoja na jitihada za Serikali ya jiji hilo la kuboresha usafiri jijini humo, bado kuna kero kubwa ya usafiri wa abiria hasa wakati wa saa za asubuhi na jioni ambapo ilimlazimu mwananchi kuchukua takribani saa tatu, kwa mfano kutoka Mbezi Juu hadi katikati ya jiji.

Katika kukabiliana na changamoto hiyo, tangu mwaka 2008 Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kupitia Tanroads imekuwa ikitekeleza miradi maalumu ya ujenzi wa barabara za kupunguza msongamano wa magari katika barabara kuu za Jiji la Dar es Salaam.

Mhandisi Miradi wa Ofisi ya Tanroads Mkoa wa Dar es Salaam, Julius Ngusa, anasema mradi wa ujenzi wa barabara za pembezoni mwa jiji hilo awamu ya tatu ni moja ya mikakati ya Serikali ya kushughulikia tatizo sugu la msongamano wa magari, ambapo utekelezaji wake ulianza tangu mwaka wa fedha 2008/2009.

Mhandisi Ngusa anasema miradi hiyo inajengwa katika awamu tatu za utekelezaji, ambapo hadi sasa awamu ya kwanza ya miradi hiyo iliyohusisha ujenzi wa barabara zenye jumla ya kilomita 19.42 tayari imekwishatekelezwa na kukamilika tangu mwaka 2008.

Anaitaja miradi iliyokamilika ni pamoja na barabara ya Ubungo-Kigogo-Kawawa iliyokamilika mwaka 2010 kwa gharama ya Sh bilioni 11.44, barabara ya Kigogo-Msimbazi-Jangwani iligharimu kiasi cha Sh bilioni 7.64 ambayo ilikamilika mwaka 2017 pamoja na barabara ya Jet Corner-Vituka-Devis Corner iliyokamilika mwaka 2011.

Kwa mujibu wa Ngusa, katika awamu hiyo mwaka 2016 Serikali pia ilikamilisha ujenzi wa Barabara ya Tegeta Kibaoni-Wazo Hill-Goba-Mbezi Mwisho (km 20), kwa gharama ya Sh bilioni 6.7.

Akifafanua zaidi, Ngusa anasema miradi mingine iliyokamilika ni pamoja na barabara ya Kilungule (Maji Chumvi)- External/Mandela km 3.3, ambapo mradi huo ulikamilika mwaka 2015 kwa gharama ya Sh bilioni 4.4.

Anasema mradi wa barabara ya Kimara Baruti-Msewe (km 2.6) uliopaswa kukamilika mwaka 2016, umeshindwa kukamilika kwa wakati kutokana na kutokuwepo kwa nafasi ya kujenga barabara, ambapo hata hivyo hadi kufikia Septemba 30, mwaka huu, mradi huo umefikia asilimia 80 ya utekelezaji wake.

Mhandisi Ngusa anasema awamu ya tatu ya utekelezaji wa miradi hiyo ulioanza kutekelezwa mwaka 2016 na 2017, unahusisha ujenzi wa barabara za Kifuru-Msigani, Goba-Makongo na Goba-Madale zenye urefu wa kilomita 14.1 na unatarajia kukamilika mwanzoni na mwishoni mwa mwaka 2018.

“Miradi ya barabara ya Goba-Madale na Goba-Makongo hadi kufikia Septemba 30, mwaka huu imekamilika kwa asilimia 50-52 wakati ule wa Kifuru-Msigani umekamilika kwa asilimia 87, malengo ni kuhakikisha kuwa miradi hii inakamilika kwa wakati kwa kuzingatia ubora na viwango tulivyojiwekea,” anasema.

Anasema baadhi ya changamoto inayokabili miradi hiyo ni pamoja na baadhi ya nyumba zinazohitaji fidia, ambapo hata hivyo Tanroads kwa kushirikiana na Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (Tarura), zimeanza zoezi la uthamini na malipo yatalipwa na Ofisi ya Rais-Tamisemi.

Anasema Serikali pia inaendelea na ujenzi wa barabara za Msongola-Mbande (km 1), Ununio-Mbweni (km 1), Kitunda-Kivule (km 3.2), Dege-Gomvu (km 1) na inatarajia kuanza awamu ya nne ujenzi wa barabara za Msigani-Mbezi mwisho (km 2) na Makongo-Ardhi (km 5) wakati wowote kutoka sasa kutegemeana na upatikanaji wa fedha.

Kukamilika kwa miradi hiyo kutasaidia kuongeza tija na ufanisi katika kuchochea kasi ya maendeleo katika Jiji la Dar es Salaam na Taifa zima kwa ujumla, hasa tukizingatia zaidi ya asilimia 80 ya pato la ndani la Taifa linachangiwa na Jiji la Dar es Salaam.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles