27.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 22, 2024

Contact us: [email protected]

Tanesco yaidai Serikali Sh bilioni 125

Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Felchesmi Mramba
Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Felchesmi Mramba

Na SARAH MOSES, DODOMA

SHIRIKA la Umeme Tanzania (Tanesco), limeiambia Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), kwamba linaidai Serikali zaidi ya Sh bilioni 125 kutokana na huduma za umeme linazotoa katika taasisi za umma pamoja na Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO).

Hayo yalielezwa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Felchesmi Mramba, wakati akijibu hoja za wajumbe wa kamati hiyo waliotaka kujua juu ya ripoti ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) inayoishia Juni 2015 kuhusu hesabu za shirika hilo.

Akiendelea kufafanua kuhusu hoja hiyo ya madeni, Mramba alisema tayari shirika hilo limeanza kufanya mikutano kadhaa na ZECO kwa ajili ya kuweka mikakati itakayofanikisha deni hilo la tangu mwaka 2013, kulipwa.

“Katika mikutano ile, tulibaini kuwa ZECO inashindwa kulipa kwa sababu inatoza gharama ndogo kwa watumiaji wa umeme Zanzibar tofauti na gharama za ununuaji umeme kutoka Tanesco,”alisema Mramba.

Kuhusu mikakati iliyoanza kuchukuliwa na shirika hilo ili kukabiliana na hali hiyo, Mramba alisema kwa sasa wameanza kuondoa mita zote za kawaida na kuweka mita za LUKU.

“Katika hilo, hadi sasa tumefanikiwa kuondoa mita za kawaida kwa takribani asilimia 99 kwa wateja wa kawaida ikiwa ni pamoja na kufungia taasisi kubwa za Serikali kama vile polisi, Jeshi la Wananchi wa Tanzania na Jeshi la Magereza.

“Hili la Luku, tunatarajia hadi Aprili mwakani, tutakuwa tumelikamilisha kwa taasisi zote za Serikali,” alisema Mramba.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya PAC, Naghejwa Kaboyoka, aliiagiza Serikali ihakikishe inalipa madeni hayo ndani ya miezi sita.

“Ni wakati sasa shirika hilo liachwe lijiendeshe lenyewe kibiashara kwani kwa hali ya sasa ilivyo, haileti maana mwananchi wa kawaida abanwe ili alipie bili yake ya umeme, wakati taasisi kubwa za Serikali zikiachwa na mlundikano wa madeni wa bili hizo za umeme,”alisema Kaboyoka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles