Na Mwandishi wetu, Zanzibar
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme la Tanzania (Tanesco ),Mhandisi Gissima Nyamo-hanga, ameelezea maendeleo ya Shirika hilo ndani ya miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar katika jukwaa la wakuu wa taasisi lililofanyika Januari 13, 2024 Unguja, Zanzibar
Katika jukwaa hilo Mhandisi Nyamo-hanga amesema kwa mara ya kwanza mwaka 1980 TANESCO ilijenga njia ya kusafirisha Umeme za ardhini zenye ukubwa wa kilometa 37.14 kutoka Rati kilomoni , Tegeta -Dar es Salaam mpaka eneo la Rati Fumba – Zanzibar, kiasi cha Umeme wa Megawati 45.
Ameongeza kuwa mwaka 2013 baada ya kuongezeka kwa matumizi ya umeme Zanzibar, shirika hilo lilijenga njia nyingine ya kusafirisha umeme ya ardhini kupeleka Zanzibar Megawati 100, njia hizo mbili ndizo zinazoendelea kutumika hadi sasa.
Akizungumzia Pemba,Mhandisi Nyamo-hanga amesema kuwa mwaka 2010 , Pemba iliunganishwa na Tanzania Bara kupitia Majani Mapana, Tanga, ambapo ilijengwa njia ya umeme ya megawati 20, umbali wa kilometa78 chini ya bahari njia ambayo bado inaendelea kutumika kufikisha umeme Pemba.
Aidha amesema matumizi ya umeme Zanzibar yanaongezeka siku hadi siku hivyo mpango uliowekwa na shirika ni kujenga njia kubwa za zitakazokuwa na uwezo zaidi ili kuendana na mahitaji ya wananchi wa Unguja na Pemba.