Na Mwandishi Wetu -Dar es Salaam
SHIRIKA la Umeme Tanzania (Tanesco), limesema usambazaji umeme vijijini umebadilisha maisha ya wananchi na umekuwa ni kichocheo kikubwa katika kutimiza azma ya Serikali kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati na wa viwanda ifikapo 2025.
Akizungumza wakati wa mahojiano katika kipindi kilichorushwa na kituo kimoja cha runinga Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Dk. Tito Mwinuka alisema Tanesco imekuwa
ikishirikiana kwa karibu na Wakala wa Usambazaji Umeme Vijijini (REA) kupeleka umeme vijijini.
Aliishukuru REA kwa ushirikiano huo na kueleza kuwa umeongeza ujenzi wa viwanda
vya kati ambavyo vimeinua uchumi wa wananchi.
Dk. Mwinuka alisema katika kipindi cha miaka minne iliyopita, Tanesco imeunganisha zaidi ya vijiji 300 na umeme wa gridi.
“Tunawashukuru wenzetu wa REA kwa namna tunavyoshirikiana kusambaza umeme katika vijiji vya Tanzania.
“Kuwapo kwa umeme kumewafanya wawekezaji wajenge viwanda vya kati na jambo hilo limeinua uchumi wa wananchi,” alisema.
Alitaja mafanikio makubwa ya shirika katika miaka minne iliyopita kuwa ni kuiunganisha mikoa ya Njombe na Ruvuma katika gridi ya taifa.
“Tanesco imejitahidi kuunganisha maeneo mengi na gridi ya taifa.
“Kuunganisha mikoa ya Njombe na Ruvuma na gridi ya taifa kumeiwezesha Serikali kuokoa zaidi ya Sh bilioni 25, fedha ambayo imekuwa ikitumika kununulia mafuta mazito ya kuendesha majenereta.
“Tanesco hatutakubali kuwa nyuma kuleta mageuzi ya kiuchumi, tunataka kuona umeme unakuwa kiunganishi muhimu ujenzi wa viwanda na uchumi wa kati ifikapo 2025,” alisema.