25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

CCBRT yakabiliwa uhaba wa damu

Na AVELINE KITOMARY -DAR ES SALAAM

MENEJA Msimamizi Mkuu wa Huduma za Maabara katika Hospitali ya CCBRT, Kennedy Kalala amesema hospitali hiyo inakabiliwa na uhaba wa damu na kutoa wito kwa wananchi kujitokeza kuchangia damu ili kuokoa maisha ya wagonjwa.

Akizungumza na MTANZANIA Dar es Salaam juzi, wakati wa mahojiano maalumu, Kalala alisema hospitali hiyo kwa siku moja inatumia chupa tano za damu kwa wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji, huku idadi ya watu wanaojitokeza kuchangia ni ndogo ikilinganishwa na mahitaji.

“Hospitalini uhitaji wa damu ni mkubwa ukilinganisha na upatikanaji wake, mwitikio wa utoaji damu bado ni mdogo, hatujafikia asilimia  50 tuliyopanga, wanaojitokeza ni wachache, Watanzania bado hawajawa na mwamko au mwitikio wa kuchangia damu.

“Wito wetu kama wataalamu wa afya, Watanzania wawe na tabia ya kuchangia damu ili kuokoa maisha ya watu wengine, hii ni ishara ya upendo, pia damu unapotoa unaokoa maisha ya watu wengine,” alisema Kalala.

Alisema ili mgonjwa aweze kufanyiwa upasuaji, ni lazima kwanza wahakikishe kuwa kuna damu ya kutosha kwani bila damu hakuna upasuaji unaoweza kufanyika. 

“Tangu Oktoba tunaendesha uchangishaji damu kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 25 tangu kuanzishwa CCBRT. 

“Hayo mahitaji yanakuja kutokana na kuwa mgonjwa hawezi kufanyiwa upasuaji bila damu, kwa hiyo tunahakikisha kwanza uwapo wake alafu ndio anafanyiwa, hivyo ni vizuri damu ikawepo,” alieleza Kalala.

 Alisema chupa moja ya damu inaweza kuwaokoa watu wanne, hivyo kutokana na uhaba wakati mwingine wanalazimika kuomba damu Kitengo cha Damu Salama.

“Kutokana na ushirikiano mzuri na Damu Salama, tunapata damu kutoka kwao, kama hawana wanatuelekeza sehemu nyingine, hivyo hatuwezi kuwategemea wao tu, lazima na sisi tuwe na damu.

 “Kitengo chetu bado hakijawa na vifaa vya kutosha kwenda sehemu mbalimbali ila tunahamasisha tukiwa hapahapa hospitalini, hivyo ni bora watu wakatoa msaada wa damu,” alisema Kalala.

Mwisho.

Mahakama yaelezwa mtuhumiwa alishawishi mapenzi kwa Sh 5,000

Na TUNU NASSOR -DAR ES SALAAM

MPELELEZI kutoka Dawati la Jinsi, Nuru Msani, ameieleza Mahakama ya Wilaya ya Ilala, kuwa mtuhumiwa Hashimu Hamis anayedaiwa kumpa mimba mwanafunzi, alitumia kishawishi cha kumpatia Sh 5,000.

Shahidi huyo wa tatu katika kesi namba 725/18, alitoa ushahidi wake mbele ya Hakimu Flora Mjaya, akiongozwa na Wakili wa Serikali, Aziza Muhina.

Nuru aliiambia mahakama kuwa mwanafunzi huyo alimwambia amefanyiwa kitendo hicho mara mbili, na mara ya kwanza ilikuwa kichakani.

Alidai alifanyiwa kitendo hicho katika kichaka kilichopo pembeni mwa reli inayopita eneo la Majohe Ilala, Dar es Salaam.

“Baada ya kumhoji mwanafunzi alinieleza ni mjamzito, alipewa na mtuhumiwa baada ya kukutana naye na kufanya naye tendo la ndoa mara mbili katika maeneo tofauti,” alidai Nuru.

Alidai mara ya pili walikutana eneo analofanyia kazi mtuhumiwa ndipo alimwingiza chooni, kisha kumbaka.

“Ushahidi wangu niliukusanya kwa kuongea na mwathirika pamoja na mama yake ambao wote walinithibitishia kuwapo kwa kitendo hicho.

“Pia niliongea na daktari aliyejaza fomu ya PF3 na kuthibitisha mwanafunzi huyo alikuwa mjamzito,” alidai Nuru.    

Wakili wa Serikali, Aziza alidai kuwa mshtakiwa alitenda makosa hayo kwa nyakati tofauti na kufanya mapenzi na mwanafunzi mara mbili.

Alidai kuwa mshtakiwa alimbaka mwanafunzi huyo kinyume na kifungu cha sheria 130 (1)(2)(e) na 131 (1) cha makosa ya jinai kilichofanyiwa marekebisho mwaka 2002 na kosa la kumpa mimba kinyume cha kifungu cha 60 (a) kifungu kidogo cha (3) cha Sheria ya Elimu namba 353 ya mwaka 2002 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2016.

Hakimu Mjaya aliiahirisha kesi hiyo hadi Novemba 8, itakaposikilizwa tena na mshtakiwa yupo nje kwa dhamana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles