Na Justine Damian – Dar es Salaam
RIPOTI ya nusu mwaka ya hali ya kiuchumi iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), imeonyesha kupungua kwa deni la nje, huku deni la ndani likiongezeka kwa asilimia 4.5.
Ikiwa na kurasa 66, ripoti hiyo inaonyesha deni hilo limeshuka kwa Dola za Marekani milioni 123.5, kutoka milioni 18,619.1 zilizorekodiwa Juni 2016, hadi kufikia Dola 18,495.5 zilizorekodiwa mwishoni mwa Desemba 2016.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, sababu za kushuka kwa deni hilo ni pamoja na malipo yaliyofanyika na sera za kubadilisha fedha za kigeni.
Ripoti hiyo inafafanua kuwa deni la nje likijumuisha la sekta binafsi, limepungua kwa asilimia 1.1 hadi kufikia Dola za Marekani milioni 16,986.2 mwishoni mwa Desemba 2016 ukilinganisha Dola milioni 17,180.9 zilizorekodiwa mwishoni mwa Juni 2016. Hata, hivyo, asilimia 81 ya deni hilo ni la umma.
Serikali hutoa dhamana kwa sekta binafsi inapotaka kukopa nje kutekeleza miradi mikubwa.
“Uchambuzi uliofanywa kwenye suala la deni la taifa kwa mwezi Novemba 2016 unaonyesha kuwa thamani ya sasa ya deni la nje kwa Pato la Taifa (GDP) ni asilimia 19.9 ambayo ni chini ya kiwango cha kimataifa cha asilimia 40 na hii inaonyesha kuwa deni hili linaweza kubebeka,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo.
Hata hivyo, ripoti hiyo inaonyesha kuwa deni la ndani la Serikali limeongezeka kwa asilimia 4.5 kufikia Sh bilioni 10,468.2 mwishoni mwa Desemba 2016 kutoka Sh bilioni 10,012.7 iliyorekodiwa Juni 2016. Deni hilo limesababishwa na dhamana ambayo Serikali imetoa kupata fedha za kugharamia bajeti.
SEKTA YA SANAA NA BURUDANI YAONGOZA
Katika hali ambayo si ya kawaida, sekta ya sanaa na burudani imeongoza kuchangia ukuaji wa Pato la Ndani (GDP) katika kipindi cha Januari hadi Septemba, huku ikiziacha nyuma sekta nguli kama fedha, ujenzi na madini.
Taarifa hiyo inaonyesha sekta ya sanaa ikiongoza kwa asilimia 17, huku ikifuatiwa na sekta ya fedha na bima.
Ripoti inaonyesha sekta hiyo kuibuka kidedea baada ya kuwa namba tatu kwa kipindi kama hicho kwa mwaka 2015, ikichangia kwa asilimia 19.2.
Mwaka 2015, sekta ya sanaa na shughuli za kitaaluma, sayansi na ufundi iliongoza katika kuchangia ukuaji wa GDP kwa asilimia 32, huku ikifuatiwa na sekta ya ujenzi ambayo ilichangia kwa asilimia 26.4 ikifuatiwa na sekta ya sanaa na burudani.
PATO LA TAIFA LAONGEZEKA
BoT katika ripoti hiyo inaonyesha Pato la Taifa (GDP) limeongezeka kufikia wastani wa asilimia 6.5 katika kipindi cha robo tatu ya mwaka 2016 ukilinganisha na hali ilivyokuwa mwaka 2015 ambapo lilikua kwa asilimia 6.3.
Ripoti hiyo imefafanua kuwa ongezeko hilo limetokana na maboresho kwenye sekta ya miundombinu, uwepo wa nishati ya uhakika, uwekezaji mkubwa katika huduma za kifedha, hasa simu za mkononi, na pia kupungua kwa viwango vya bei za mafuta duniani.
Imechanganua kuongezeka huko pia kumechangiwa na mambo mbalimbali yakiongozwa na sekta ya usafirishaji na kuhifadhi kwa asilimia 15.4, ujenzi kwa asilimia 11, sekta ya habari na mawasiliano asilimia 9.5, biashara ya jumla na rejareja asilimia 9 na sekta ya madini asilimia 7.9.
MAUZO YA NJE YASHUKA
Ripoti inaonyesha mauzo ya nje ya bidhaa na huduma yakishuka kwa asilimia 1.6 ukilinganisha na kipindi cha mwaka wa fedha 2015/16.
Mauzo mazuri ya nje yalirekodiwa kwenye bidhaa kama dhahabu, pamba, kahawa (traditional crops), usafiri na utalii.
Thamani ya dhahabu iliyosafirishwa nje iliongezeka hadi kufikia Dola za Marekani milioni 807.1 kutoka milioni 601.0 ikiwa imechangiwa na kuongezeka kwa kiasi kilichosafirishwa, huku bei ya bidhaa hiyo ikianguka katika soko la dunia.
Usafirishaji nje wa bidhaa zilizozoeleka uliongezeka kwa asilimia 28.3 kufikia Dola za Marekani milioni 549.1 huku kiasi kilichosafirishwa kwa bidhaa za kundi hili kama chai, mkonge na karafuu kikiongezeka mara dufu.
Kuongezeka kwa thamani ya mauzo ya nje ya bidhaa kumechangiwa na hali nzuri ya hewa na matumizi sahihi na ya wakati ya dawa za kilimo.
SEKTA YA BENKI
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, sekta ya benki imeendelea kuwa imara, isiyotetereka na yenye kutengeneza faida.
Ripoti inasema sekta hiyo imekuwa na mtaji wa kutosha na uwezo wa kifedha zaidi ya kiasi ambacho inatakiwa kuwa nacho kisheria.
Sheria inazitaka benki kuwa na si chini ya asilimia 10, lakini benki zilikuwa na asilimia 18 ambayo ni juu ya kiasi kinachotakiwa kisheria kufikia Desemba 2016.
MAENDELEO YATEGEMEA WAFADHILI
Katika kipindi cha mwaka 2016/17, jumla ya matumizi ya Serikali yalifikia Sh bilioni 282.1 ikiwa ni asilimia 1.1 ya makadirio yaliyowekwa, huku matumizi yasiyo ya maendeleo yakichukua asilimia 79.7 ya matumizi yote, huku matumizi ya kimaendeleo yakiwa ni asilimia 40.3.
MIAMALA YA SIMU
Uwezekano wa kutuma fedha moja kwa moja kwa mitandao tofauti ya simu, umesaidia kuongezeka kwa miamala kutoka mtandao mmoja hadi mwingine kwa urahisi zaidi.
Katika nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha 2016/17, miamala milioni 20.1 yenye thamani ya Sh bilioni 989 ilifanyika ambapo ni asilimia 4.4 ya miamala juu ya miamala yenye thamani ya Sh bilioni 178.1 iliyofanyika mwaka mmoja nyuma.
THAMANI YA SHILINGI
Thamani ya shilingi dhidi ya Dola ya Marekani iliendelea kuwa imara katika kipindi chote.
Kiwango cha ubadilishaji fedha kilishuka kutoka Sh 2,194 hadi kufi kia Sh 2,180 kwa Dola ya Marekani dhidi ya shilingi ya Tanzania, ikilinganishwa na Sh 1,984 kwa Sh 2,227 kwa dola moja katika kipindi kama hicho kwa mwaka wa fedha 2015/16.
Katika kipindi hicho, amana za benki zilikua na kufi kia asilimia 79.8 ya jumla ya madeni yote. Ripoti inaeleza kuwa Benki Kuu inaendelea kuangalia
ongezeko la mfumo wa taarifa za wakopaji.
Utumiaji wa mfumo huu unatarajia kuwafanya wakopaji kuwajibika zaidi katika kukopa.
MFUMO WA MALIPO
Kipindi cha 2016/17 mifumo ya malipo iliendelea kufanya kazi kwa ufanisi na kuonyesha ukuaji wa kuendelea katika upatikanaji na matumizi kutokana na kuongezeka matumizi ya teknolojia katika utoaji huduma za kifedha.
Katika sheria mpya ya malipo, malipo yasiyo ya kibenki yanatakiwa kupata leseni ya kutoa huduma za malipo.
MAPATO YA MIPAKANI
Malipo ya shughuli za mpakani kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki, yaliongezeka kwa kiwango kikubwa ambapo Tanzania na Kenya malipo 1,055 yalifanyika ambayo yalikuwa na thamani ya Sh za Kenya bilioni 1.6 ikilinganishwa Tanzania na Uganda ambapo malipo 122 yenye thamani ya Sh za Uganda bilioni 6.4 yalifanyika.